METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, July 27, 2020

NAIBU WAZIRI DKT MABULA: ‘MNAOPIMIWA ARDHI, MSIKWEPE KUMILIKISHWA’


Wananchi wanaopimiwa viwanja na kisha upimaji ukaidhinishwa wametakiwa kutokwepa kumilikishwa kwani kufanya hivyo ni kutenda kosa kisheria.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa zoezi la ugawaji hati 1300 kwa wananchi wa manispaa ya Ilemela jijini Mwanza ambapo amesema kuwa ipo tabia kwa baadhi ya wananchi kuomba kupimiwa viwanja vyao na baada ya hapo kukwepa kulipa kodi kwa kukataa kuomba kumilikishwa maeneo yao kitendo ambacho kimekuwa kikiikosesha Serikali mapato hivyo kuamua kuanzisha sheria namba 8 ya fedha ya mwaka 2020 ili kukabiliana na changamoto hiyo

‘..  Kuanzia Julai 1, 2020 mwananchi yeyote aliyepimiwa eneo lake na upimaji ukaidhinishwa anatakiwa aombe kumilikishwa ili alipe kodi ya pango la ardhi tangu pale alipomilikishwa, Lakini ukishindwa kufanya hivyo ndani ya miezi 3 utatakiwa kulipa kodi hiyo kuanzia mwaka 1990 mpaka sasa ..’ Alisema

Aidha Dkt Mabula akasisitiza kuwa zoezi la urasimishaji si endelevu na halina fidia kwani limetokana na msamaha wa Rais Mhe Dkt John Magufuli kwa wananchi wake baada ya kuona wamejenga bila kufuata utaratibu hivyo kuamua kuwarasimishia makazi yao ili waishi kwa amani na utulivu bila ghasia yoyote ikiwemo kuvunjiwa.

Akimkaribisha mgeni rasmi, Kamishina wa ardhi mkoa wa Mwanza Ndugu Makwasa Musase Biswalo amesema kuwa zoezi la ugawaji hati kwa wananchi litakuwa likiendeshwa kwa kuwafata wananchi katika maeneo yao badala ya kuwasumbua kwa kila siku kuzifuata katika ofisi za ardhi za mkoa na halmashauri ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya wizara huku akimshukuru waziri huyo kwa ushirikiano anaoutoa kwa ofisi yake.
Kwa upande wake afisa ardhi mteule wa manispaa ya Ilemela Bi Grace  Isaac Masawe akasema kuwa manispaa yake kwa kipindi cha 2020/2021 imepanga kuandaa hati 5000 na mpaka sasa zimeshaandaliwa hati 3327 zikiwemo zile za mradi wa viwanja kwaajili ya walimu na hati 331 za urasimishaji makazi

Bwana Julius Peter ni moja ya wananchi waliokabidhiwa hati miliki katika zoezi hilo ambapo ameishukuru Serikali kwa kuruhusu zoezi la urasimishaji makazi na kuwataka wananchi wengine kutumia fursa hiyo kikamilifu.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com