METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, April 1, 2024

BAADA YA UKAGUZI KIDATU, DKT. BITEKO ATUA KITUO CHA KUPOZA UMEME CHA ZUZU DODOMA


Baada ya ukaguzi wa matengenezo ya mitambo ya umeme Kidatu Mkoani Morogoro leo tarehe 1 Aprili, 2024 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko ametembelea na kukagua Kituo cha kupoza umeme cha Zuzu kilichopo Jijini Dodoma.

Kituo cha kupoza Umeme cha Zuzu kilipata hitilafu kubwa baada ya Gridi ya Taifa kupata hitilafu kwenye mfumo wa kudhibiti kiwango cha maji kwenye mitambo na kusababisha mitambo kujizima kwa ghafla ili kujilinda jambo lililopelekea athari kwenye mfumo mzima wa Gridi ya Taifa na maeneo mbalimbali kukosa huduma ya umeme katika kipindi hiki cha mapumziko ya sikukuu ya Pasaka.

Dkt Biteko amewapongeza wataalamu kwa kazi kubwa ya kuendelea kufanya matengenezo ya haraka katika kituo cha kupoza Umeme cha Zuzu na maeneo yote yaliyokumbwa na kadhia hiyo kote nchini huku akisisitiza wataalamu kuendelea kukamilisha matengenezo kwa haraka ili umeme urejee maeneo yote ya nchi.

MWISHO
Share:

Wednesday, March 6, 2024

KADA WA CCM NEEMA MGHEN ACHANGIA MIFUKO 50 UJENZI WODI YA WAZAZI USHETU

Ushetu, Shinyanga...!

Kada wa Chama Cha Mapinduzi Wilayani Bi Neema Mghen amechangia mifuko 50 ya Saruji yenye thamani ya shilingi milioni 1,150,000/= Kwaajili ya ukamilishaji wa Jengo la wodi ya wazazi katika Zahati ya Sabasabini Halmashauri ya Ushetu.

Akizungumza wakati wa sherehe ya wanawake Duniani ambayo imeadhimishwa katika kijiji cha Sabasabini na jukwaa la Wanawake Halmashauri ya Ushetu huku ikiwa imeambatana na Harambee maalumu kwaajili ya ukamilishaji wa wa wodi hiyo.

Amesema kuwa mkakati huo ni kumuunga mkono Mhe. Rais katika utekelezaji wa miradi ya Maendeleo.

Mgheni amesema, lengo la maadhimisho hayo ni kutoa fursa kwa wanawake na wadau wengine kutafakari changamoto na mafanikio ili kuweka mikakati ya kuwainua wanawake kwa kuwekeza katika miradi mbalimbali ikiwemo Afya Elimu na Miundombinu.

Sambamba na hayo Mgheni amesema ni wajibu wa serikali kupitia Halmashauri kutunga sheria ndogo za kukabiliana na ukatili kwa wanawake na watoto lakini pia kuwaelimisha wanawake juu ya fursa za kiuchumi na wajibu wao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu Hadija Kabojela amesema, Jukwaa la Wanawake Ushetu kwa kutambua umuhimu wa wodi ya wazazi wameona ni vyema kusherehekea siku ya wanawaje dunia kwa kufanya harambee itakayo saidia upatikanaji wa fedha milioni 50 inayohitajika kukamilisha ujenzi wa wodi hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Sabasabini Diwani wa viti maalumu Felista Nyerere amesema, wodi hiyo ikikamilika itaondoa usumbufu kwa wanawake ambao wanahangaika sehemu ya kupumzika baada ya kujifungua kwakuwa hakuna sehemu nzuri ya kujifungulia hali inayofanya wakazi wa eneo kwenda umbali mrefu katika kata za Lowa na Bulungwa kutafuta usalama wa mazingira ya kujifungulia.

Harambee hiyo imehudhuliwa na Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Shinyanga Lucy Mayenga aliechangia mifuko 30 ya Saruji, Mbunge wa Ushetu Emmanuel Cherehani ambae amechangia fedha shilingi Milion 1 na Laki tatu, madiwani kupitia baraza lao wamechangia milioni 2 ambapo fedha iliyopatikana kwenye harambee hiyo ni shilingi Milioni 6,482,600 na sarufi mifuko 95 ambapo wodi hiyo itaipewa jina la Neema Mgheni.

MWISHO
Share:

Wednesday, February 21, 2024

UTEKELEZAJI MRADI WA TANZANIA YA KIDIJITALI WAFIKIA 70%-KATIBU MKUU WHMTH, MOHAMMED KHAMIS ABDULLA








Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Khamis Abdulla amesema utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya Kidijitali umefikia asilimia 70 na utekelezaji wake ni wa miaka mitano kuanzia 2021 hadi 2026.

Amesema mradi huo una malengo ya kuchochea mabadiliko ya kidijitali nchini, uundwaji wa mfumo wa namba moja ya utambulisho (jamii namba) mbayo itatumika kufanya utambuzi kuanzia mtu anapozaliwa ili kumwezesha mwananchi kupata huduma mbalimbali zikiwepo za afya, elimu, usafiri na nyinginezo pamoja na kuunganishwa katika mifumo ya vitambulisho vya Taifa, vyeti vya kuzaliwa na vinginevyo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Mjini Zanzibar kuhusu mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Bw. Abdulla amesema pamoja na mambo mengine, mradi huo pia utawezesha uundwaji wa mfumo wa kitaifa na uunganishwaji wa mifumo (National Enterprises Service Bus) utakaounganisha mifumo ya serikali na binafsi ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Tunalenga kuendelea kuboresha mfuko wa anwani za makazi na postikodi ili kuwezesha watoa huduma mbalimbali nchini, kuweza kutambua wateja wao kielektroniki na kuondoa adha ya mwananchi ya kwenda kila mara kuomba utambulisho kwenye serikali za mitaa, pia mradi huu utawezesha kupeleka mawasiliano ya mtandao wa simu kwenye maeneo ambayo hayakuwa na mawasiliano ambapo kwa sasa, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inaendelea na ujenzi wa minara mipya ya simu 438 na upandishaji wa hadhi minara 304” amesema Bw. Abdulla.

Aidha amebainisha kuwa mradi huo utawezesha kuunganisha taasisi za Serikali 891 na mtandao wa mawasiliano ya Serikali (GovNet), ili kufikisha mawasiliano ya kimtandao kwenye ofisi hizo, zinazojumuisha hospitali, vituo vya afya, shule, mahakama, vituo vya polisi, vituo vya halmashauri, na taasisi za serikali.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Bi Khadija Khamis Rajab amesema Zanzaibar itanufaika na mradi huo kupitia marekebisho ya kanuni, sheria na sera ya TEHAMA ili kuendana na mabadiliko yake ambapo kwa sasa kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF) tayari wamepata minara 42 ya mawasiliano.

“Kupitia mradi huu tutaweza kupata minara mingine ya nyongeza katika maeneo ambayo bado hayajaweza kufikiwa vizuri kwa upande wa mawasiliano, na hii tutafanya kutokana na ripoti ambazo tutazipata kupitia kwa wenzetu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wao watatuambia ni minara mingapi na ni kwenye maeneo gani inahitajika, pia tutaweza kuimarisha minara ya mawasiliano ili iweze kuwa bora zaidi, na maeneo yote yaweze kufikiwa na huduma za mawasiliano mijini na vijijini” amesema Bi. Rajab. 

Amesema pia kutakuwa na mifumo 17 ambayo wataweza kunufaika nayo kupitia mradi huo kupitia vituo 159 ambavyo vitajumuisha shule, vituo vya afya, halmashauri na maeneo mengine ikiwemo taasisi za serikali.

Nae Afisa Mwandamizi wa Maendeleo ya kidijitali kutoka Benki ya Dunia Bw. Paul Seaden amesema lengo la Benki hiyo la kutoa Dola za Kimarekani milioni 150 ni kusaidia kuwezesha mradi huo ambao utaiwezesha Tanzania kuendelea katika mifumo ya mawasiliano ya kidijitali.

Mwisho.
Share:

Monday, February 19, 2024

TUNATEGEMEA MAFANIKIO MAKUBWA REA – BODI MPYA



Na Veronica Simba – REA

Bodi ya Nishati Vijijini (REB) inayosimamia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imesema inategemea mafanikio makubwa katika kuiwezesha Wakala hiyo kutimiza azma yake ya kuwafikishia wananchi walioko vijijini nishati bora za umeme, mafuta na gesi.

Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Balozi, Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu baada ya kikao cha kwanza cha Bodi hiyo mpya kilicholenga kutambuana na kupanga majukumu.

“Kikao chetu kimeenda vizuri, tumechagua Kamati na kupangiana majukumu. Tunaamini na tunaahidi kuwa tutatekeleza majukumu yetu sawasawa na Sheria iliyoanzisha Wakala wa Nishati Vijijini inavyoelekeza,” amesema.

Aidha, Balozi Kingu amemshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi na amemshukuru Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ndiye Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko kwa kukamilisha mchakato wa uteuzi wa Wajumbe wa Bodi, jambo ambalo limeiwezesha kuwa Bodi kamili.

Akieleza zaidi kuhusu majukumu waliyojipangia, Balozi Kingu amesema mapema Mwezi Machi, Bodi itakutana katika kikao cha dharura kupitia na kujadili masuala mbalimbali ya Wakala ambayo yalikuwa yakisuburi baraka za Bodi ili kuyatolea maamuzi yatakayowezesha utekelezaji wake kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Katibu wa Bodi hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amepongeza Mamlaka za Uteuzi, kuteua watu makini, hodari na wachapakazi ambao amesema ni muhimu kuwa nao katika kuisimamia Wakala hiyo yenye majukumu makubwa yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

“REA ina jukumu kubwa ambalo linagusa maisha ya watu lakini pia linahusisha kiasi kikubwa sana cha fedha za Serikali. Kwahiyo, kuwa na Bodi nzuri iliyosheheni watu makini, kwetu sisi ni jambo la faraja,” amefafanua.

Mkurugenzi Mkuu, kwa niaba ya Menejimenti na Wafanyakazi wote wa REA, ametoa ahadi ya ushirikiano kwa Bodi hiyo mpya ili kuhakikisha malengo ya Serikali kupitia majukumu yaliyokasimiwa kwa Wakala yanatekelezwa.

“Tunatamani kuona Watanzania wenzetu wanaoishi vijijini wanapata nishati bora kama ilivyo kwa wenzao wanaoishi mjini,” amesisitiza.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wajumbe wa Bodi wamezishukuru Mamlaka za Uteuzi kwa kuwaamini na kuwapa jukumu hilo kubwa la kuisimamia REA ili kuendelea kuleta matokeo chanya.

Aidha, wamepongeza Bodi zilizotangulia kabla yao, Menejementi pamoja na Wafanyakazi wote kwa kazi nzuri waliyofanya tangu kuanzishwa kwa Wakala na kuahidi kuendeleza yote mazuri yaliyofanyika ili kuongeza tija.

Kikao hicho pia kilishirikisha Menejimenti ya Wakala ambapo Wakuu wa Idara na Vitengo waliwasilisha kwa Bodi taarifa za utekelezaji wa majukumu katika maeneo wanayosimamia kwa lengo la kuijengea Bodi uelewa na ufahamu kuhusu Taasisi hiyo waliyopewa jukumu la kuisimamia.

Januari 26 mwaka huu, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko aliwateua Florian Otman Haule, Lucas Charles Malunde, Mwantum Issa Sultan, Stephen Menard Mwakifamba, James Issack Mabula, Ahmed Martin Chinemba, Sophia Shaban Mgonja na Balozi Radhiya Naima Msuya kuwa Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini, wakiungana na Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Gideon Kingu aliyeteuliwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Septemba 2023 kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo.

Share:

Serikali, Benki ya Dunia wakutana kujadili mradi wa Tanzania ya Kidijitali

Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia-WB, wanaendelea na majadiliano ya namna ya utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya kidijitali, ambapo wataalam kutoka katika Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Zanzibar pamoja na taasisi mbalimbali za Umma, wamekutana mjini Zanzibar kwa ajili ya majadiliano hayo.

Mradi huo unatarajia kutekelezwa kwa gharama ya dola za kimarekani milioni 150 sawa na shilingi Bilioni 348 za kitanzania na unatazamiwa kuboresha na kuimarisha huduma za mawasiliano nchini. 

Ni katika mkutano wa tatu wa kikao cha utekelezaji wa Tanzania ya Kidijitali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ulioanza februari 19 hadi 23 mwaka huu mjini Zanzibar, ambapo pamoja na mambo mengine, mkutano huo utajadili malengo ya kuongeza upatikanaji wa huduma za mtandao wa intaneti zenye gharama nafuu na ubora wa juu kwa serikali, wafanyabiashara na wananchi sambamba na kuboresha uwezo wa serikali wa kutoa huduma za umma kidijitali.

Akizungumza wakati akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bi. Khadija Khamis Rajab, amesema matarajio ya serikali ni kwamba miradi ya kimkakati katika sekta ya mawasiliano itatekelezwa.

“Tunatarajia mradi huu utaenda kutekeleza mambo makubwa ili tuweze kutekeleza miradi mingine ya kimkakati katika sekta yetu hii ya mawasiliano, tuna maeneo mengi ya msingi ambayo yatakuwa yamegawanywa katika mradi huu wa Tanzania ya kidijitali, na katika maeneo hayo kutakuwa na maeneo makuu matatu ambayo ni pamoja na kupitia na kuhuisha sheria miongozo na taratibu za kisheria za TEHAMA ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia” amesema Ndugu. Rajab.

Meneja wa mradi huo wa Tanzania ya Kidijitali Bw. Bakari Mwamgugu amesema pia kutakuwa na maboresho ya miundombinu ya TEHAMA, ikiwepo kuunganisha taasisi za serikali katika mkongo wa mawasiliano taifa, kuboresha vituo vya kuhifadhia kanzidata, na kupeleka mawasiliano katika maeneo ambayo hakuna mawasiliano ikiwa ni pamoja na kuboresha mawasiliano kutoka 2G kwenda 4G.

“Lengo la tatu ni kuboresha na kutekeleza mifumo mbalimbali itakayosaidia kutoa huduma bora kwa wananchi na kwa wakati, ukiwepo mfumo wa jamii namba, ambao kila mtanzania atatakiwa kuwa na namba moja tu ya kupata huduma” amesema Bw. Bakari.

Mradi huo una malengo ya kuongeza upatikanaji wa huduma za mtandao wa intaneti zenye gharama nafuu na ubora wa juu kwa serikali, wafanyabiashara na wananchi, sambamba na kuboresha uwezo wa serikali wa kutoa huduma za umma kidijitali.

Mradi wa ‘Tanzania ya Kidijitali' unaofadhiliwa na Benki ya Dunia unatekelezwa kwa usimamizi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Pamoja na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali zinazohusika na TEHAMA kwa upande wa Tanzania Bara na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Mwisho.
Share:

Friday, February 16, 2024

MBUNGE OLE LEKAITA AKABIDHI MAGARI MAWILI YA WAGONJWA KITUO CHA AFYA SUNYA-KITETO

Na Mathias Canal, Kiteto-Manyara

Kituo cha afya cha Sunya kilichopo katika Wilaya ya Kiteto kimekabidhiwa magari mawili ya wagonjwa (Ambulance) kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi magari hayo jana tarehe 16 Februari 2024 Mbunge wa jimbo la Kiteto mkoani Manyara Mhe Edward Ole Lekaita amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan ametoa magari hayo ili kupunguza adha wanazozipata wananchi.

Amesema Rais Samia ametoa magari matatu ambapo mawili kati ya hayo yamewasili mjini Kiteto, magari mawili yatakuwa kwaajili ya wagonjwa na moja kwaajilia ya madaktari.

Mbunge Ole Lekaita amewataka wahudumu wa afya pamoja na wananchi wote kuhakikisha wanayatunza magari hayo ili yaweze kutumika kuwahudumia kama serikali ilivyokusudia.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Mbunge wa Jimbo la Msalala Mhe Iddy Kassim pamoja na Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini Mhe Priscus Tarimo ambao kwa pamoja wamempongeza Mbunge huyo kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya ya kuwatumikia wananchi kwa ufasaha.

Wamewasihi wananchi kuendelea kumuunga mkono na kumuombea mbunge wao ili aendelee kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

MWISHO
Share:

MBUNGE NYONGO AIGEIKUIA SERIKALI KUNUNUA PAMBA SOKO LINAPOPOROMOKA


SERIKALI ipo katika hatua za awali za uanzishwaji wa Mfuko wa Kinga ya bei ya Pamba utakaotumika kumfidia mkulima wakati bei inaposhuka kwa kiasi kitakachokubalika kwa mujibu wa sheria ya kuanzishwa kwake.

Hayo yamesemwa bungeni leo na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde wakati akijibu swali la Mbunge wa Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo (CCM).

Katika swali lake, Mbunge huyo ametaka kujua ni lini Serikali itaanza kununua Pamba toka kwa wakulima pindi bei ya Pamba inapoporomoka katika soko la Dunia.

Akijibu swali hilo, Silinde amesema biashara ya pamba nchini hufanyika kwa kuzingatia hali halisi ya soko ilivyo.

Amebainisha kuwa Serikali imekuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa bei inayotolewa kwa wakulima inaakisi uhalisi wa bei katika soko la dunia kwa wakati huo.

“Kutokana na kutokuwiana kati ya uzalishaji na mahitaji ya pamba duniani, bei ya pamba hupanda na kushuka kulingana na hali ya wakati huo. “

Mathalani, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita bei ya pamba kwa ratili katika soko la dunia mwaka 2020 ilifikia Senti 50 za Dola ya Marekani na mwaka 2021, bei ilipanda hadi kufikia Dola 1.5 kwa ratili.

“Mwaka 2023 hadi mwanzoni mwa 2024 bei ilikuwa wastani wa Senti 84.”amesema Silinde.

“Kwa kutambua athari ya mabadiliko ya bei kwa wakulima wa pamba nchini, Serikali ipo katika hatua za awali za uanzishaji wa Mfuko wa Kinga ya Bei utakaotumika kumfidia mkulima wakati bei inaposhuka kwa kiasi kitakachokubalika kwa mujibu wa Sheria ya kuanzishwa kwake,”amesisitiza.
Share:

Thursday, February 15, 2024

JE, SERIKALI INAMKAKATI GANI WA HARAKA KUHAKIKISHA MIUNDOMBINU YA TAZARA INAKUWA KIWANGO CHA SGR?"MBUNGE NJEZA"



Na Saida Issa, Dodoma

Mbunge wa Mbeya Vijini Oran Njenza ameuluza kuwa Je, serikali inamkakati gani wa haraka kuhakikisha miundombinu ya tazara inakuwa kiwango cha SGR?

Swali hilo ameuliza bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu ambapo ametaka kujua mkakati wa Serikali. 

Akijibu swali la Mbunge huyo Naibu Waziri wa uchukuzi David Kihenzile amesema mpango wa Serikali wa kuiboresha vizuri Tazara Tayari viongozi wameanza mazungumzo pindi yatakapokuwa tayari yataanza kutekelezwa mwaka huu huu 2024. 
Share:

SERIKALI INAENDELEA NA UPEMBUZI YAKINIFU NA USANIFU BONDE LA BUYUNGU.



Na Saida Issa, Dodoma

SERIKALI kupitiaTume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na kazi za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika bonde la Buyungu linalojumuisha Skimu za Katengera, Muhwazi, Ruhwiti, Ruhuru, Mgunzu, Kayonza, Lukoyoyo, Chulanzo, Asante Nyerere na Kilimo Kwanza.

Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri kilimo David Silinde alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Buyungu Aloyce kamamba alipouliza 
Je,ni lini Skimu za Umwagiliaji za Katengera, Muhwazi, Gwanumbu na Ruhwiti katika Wilaya ya Kakonko zitakarabatiwa. 

Kazi za upembuzi yakinifu na usanifu zinatarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2024.

"Kukamilika kwa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika skimu hizi kutawezesha kupatikana kwa gharama halisi za ujenzi na ukarabati, hivyo kuwekwa kwenye mpango wa ujenzi na bajeti,

Mheshimiwa Spika, Mradi wa umwagiliaji Gwanumbu umeendelezwa kwa kujengewa mfereji mkuu, mradi huu unahitaji kufanyiwa usanifu wa miundombinu ambayo haijakamilika,"amesema.

Aidha amesema kuwa Katika mwaka wa fedha 2024/2025 Mradi wa umwagiliaji Gwanumbu utaingizwa kwenye mpango wa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kujua gharama halisi za ukarabati kabla ya kuingizwa kwenye mpango wa ujenzi na bajeti.
Share:

Wednesday, February 14, 2024

TANZANIA KUWA NCHI YA 22 AFRIKA KUFANYA UTAFITI WA GHARAMA ZA UTAPIAMLO NCHINI-MHE UMMY NDERIANANGA


Na Mathias Canal, Dodoma

Tanzania itakuwa nchi ya 22 barani Afrika kufanya utafiti wa gharama za utapiamlo nchini pindi utakapokamilika. 

Mwaka 2024, takribani nchi 6 (ikiwemo Tanzania) zimeonesha utayari wa kufanya utafiti huo ili kuwezesha nchi kupanga malengo ya kupunguza upotevu wa pato ghafi itokanayo na utapiamlo na kuwekeza katika maeneo ya maendeleo. 

Hayo yamebainishwa leo tarehe 14 Februari 2024 na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) wakati akizindua zoezi la utafiti wa gharama za utapiamlo nchini.

Mhe Nderiananga amesema kuwa tafiti hizo zinazofanyika hapa nchini ni moja ya jitihada za kutafuta shahidi za kisayansi zinazoweza kuisaidia Serikali kuboresha harakati zake za kuondokana na athari za utapiamlo (hasa udumavu kwa watoto pamoja na uzito uliozidi au kiribatumbo kwa watu wenye miaka 15-49). 

“Hivyo basi, ni jukumu letu sote kama Serikali na wadau kuhakikisha tunafanya tafiti nyingi zinazogusa changamoto zilizo katika jamii zetu. Lengo ni kupata taarifa sahihi zitakazochagiza harakati za kuelekea maendeleo endelevu na kuimarisha ustawi wa Taifa letu kupitia nguvukazi ya watu wenye afya njema, ufahamu mzuri na wenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi” Amesisitiza Mhe Nderiananga

Amesema kuwa ameridhika na taarifa zote zilizotolewa kuhusu chimbuko, msingi na umuhimu wa kufanya zoezi la utafiti huu pamoja na maelezo ya jinsi ilivyopangwa kulitekeleza. 

Mhe Ummy amewashukuru wataalamu wa Chakula na Lishe kwa kuishauri vyema Serikali juu ya umuhimu wa utafiti huo katika nchi inapokwenda kuandaa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050. 

Kadhalika amewashukru wadau wakiwemo Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) ambao tayari wameshatoa fedha ambazo zitasaidia katika hatua muhimu za utafiti huo. 

“Kwa mujibu wa maelezo ya utangulizi huu ni utekelezaji wa maazimio ya viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kupitia mpango ujulikanao kama “The Cost of Hunger Study in Africa – COHA” ambapo Mheshimiwa DKt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameridhia ufanyike” Amesisitiza na kuongeza kuwa

“Hii inatokana na nia yake ya dhati ya kuondoa utapiamlo nchini. Lengo la utafiti ni kubainisha makadirio ya gharama zinazosababishwa na matatizo ya lishe duni/utapiamlo; kijamii na kiuchumi na hususan katika nyanja za sekta ya afya, elimu na nguvu kazi”

MWISHO
Share:

Thursday, February 8, 2024

SERIKALI KUENDELEA KUWAINUA KIUCHUMI VIJANA WENYE ULEMAVU


Na; Mwandishi Wetu - DODOMA

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amesema kuwa serikali imeendelea kuwezesha vijana wenye Ulemavu kupata mafunzo ya ukuzaji ujuzi na mikopo masharti nafuu ili kuboresha hali zao kimaisha.

Amesema hayo hii leo Februari 8, 2024 Bungeni, jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Mwantatu Khamis ambaye alitaka kujua vijana wenye Ulemavu wamenufaika vipi na mafunzo na mikopo inayotolewa na serikali.

Akijibu swali hilo, Mhe. Ummy Nderiananga amesema serikali inatekeleza mikakati na programu mbalimbali kwa lengo la kukuza ushiriki wa Watu wenye Ulemavu katika shughuli za kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Ameongeza kuwa, kwa mwaka fedha 2022/23 zaidi ya vijana wenye Ulemavu wamenufaika na mafunzo ya ufundi stadi na marekebisho kupitia Programu ya Taifa ya Ukuzaji Ujuzi. Pia, kiasi cha mikopo Tsh. Bilioni 81.3 kimetolewa kwa wanufaika 640,723 ikiwemo Watu wenye Ulemavu ambayo imewasaidia kuanzisha na kuendeleza biashara zao.

Kwa upande mwengine, Mhe. Nderiananga ametoa wito kwa Watu wenye Ulemavu kuchangamkia fursa zinazotolewa na serikali.

MWISHO
Share:

SERIKALI YAOMBWA KUAJIRI WALIMU ILI KUENDANA NA IDADI KUBWA YA WANAFUNZI- MBUNGE KAKONKO KAMAMBA.




Na Saida Issa, Dodoma

MBUNGE wa Buyungu kakonko Alloyce Kamamba amesema kuwa Serikali imefanya vizuri katika ujenzi wa shule za sekondari na msingi kwa kujenga madarasa,vyoo pamoja na nyumba za walimu hali iliyopelekea idadi ya wanafunzi kuongezeka huku akiomba Serikali kuajiri walimu ili kuwapunguzia mzigo wa majukumu. 

Hayo ameyaeleza Bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akitoa maoni yake kwa kamati ya kudumu ya Bunge,ustawi na Maendeleo ya jamii. 

Alisema kuwa ongezeko la wanafunzi halikuenda sambamba na ongezeko la kuajiri walimu alisema kuwa Kwa upande wa elimu ya sekondari uhitaji wa walimu ni kwa asilimia 47 na upande wa shule za msingi uhitaji wa walimu ni asilimia 42.

Akizungumzia Mkoa wa Kigoma alisema kuwa uhitaji wa walimu sekondari no asilimia 33 upande wa shule za msingi ni asilimia 46.

"Nikichukua wilaya yangu ya kakonko uhitaji wa walimu shule za msingi ni asilimia 38 na upande wa sekondari ni asilimia 52,ukiangalia kwa jumla bado walimu waliopo na wanaohitajika ni nusu kwa nusu,

Ninachoshangaa mheshimiwa mwenyekiti ni kuona kwamba walimu wapo kwa asilimia 47 lakini wanafaulisha kwa asilimia 80 maana yake mini mheshimiwa mwenyekiti walimu wa Nchi hii wamefanya kazi ya ziada kuziba lengo la walimu ambao hawapo,hoja yangu mwenyekiti walimu waajiriwe,"alisema.

Pia aliiomba Serikali kujenga mabweni katika shule za kata ili kuwapunguzia changamoto ya jua pamoja na mvua mwanafunzi.

Alisema kuwa kuwepo kwa mabweni kutasaidia kuwa na uhakika na makazi ya mwanafunzi pindi wawapo shule pia walimu kuweza kuwafatilia wanafunzi hao.
Share:
Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com