METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, April 18, 2017

KAMPENI YA 'MTI WANGU' YASHIKA KASI MANISPAA YA UBUNGO

Na Nasri Bakari, Dar es Salaam

Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kupitia idara ya Maliasili imeendelea kuunga mkono kwa vitendo kampeni ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Mh. Paul Makonda ya 'MTI WANGU' kwa  kupanda miti ya aina mbalimbali ndani ya Manispaa ya hiyo.

Kampeni hiyo imeendelea leo kwa kupanda miti 156 katika shule ya Sekondari Kibwegere iliyopo eneo la Kibwegere Kata ya Kibamba.

Kampeni hiyo yenye  kauli mbiu ya panda miti tunza miti tupate nishati (MTI WANGU) ina lengo la kuhifadhi mazingira,  kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na majanga asilia kama upepo mkali, mmomonyoko wa udongo, maporomoko ya  ardhi na mafuriko.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo Kaimu Afisa Maliasili wa Manispaa ya Ubungo Bi. Sikujua Mwapinga alisema anamshukuru Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Ndg. John Lipesi Kayombo kwa kuwezesha mradi huo na kuunga mkono kampeni hiyo pia aliwasisitiza walimu pamoja na wanafunzi wapande miti katika maeneo mbalimbali sambamba na kuihifadhi ili kufanya dunia kuwa  mahali salama kwa viumbe wote.

Wakati huo huo akizungumza kwa niaba ya walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Kibwegere mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi. Christina P. Mwita alisema wanaishukuru Manispaa ya Ubungo kwa kuwaletea miti na kuahidi kuitunza kikamilifu.

"Tunamshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Ndg. John Lipesi Kayombo kwa kutuletea miti kwani shule yetu ilikuwa kama jangwa pia tunaahidi kuitunza sambamba na  kuhakikisha shule yetu inapendeza"

Imetolewa na

Kitengo cha Uhusiano

Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com