METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, January 16, 2017

DKT TIZEBA: NCHI HAIJAKABILIWA NA JANGA LA NJAA


Kulia ni Waziri wa kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt Charles John Tizeba akizungumza na waandishi wa habari, kushoto kwake ni Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Mhandisi Methew Mtigumwe.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt Charles John Tizeba akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa habari


Na Mathias Canal, Dar ea salaam

Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt . Charles John Tizeba amekanusha taarifa zilizozagaa kwenye vyombo vya Habari na Mitandao ya kijamii kuwa Tanzania imekumbwa na janga la njaa.

Dkt Tizeba ameyasema hayo ofisini kwake alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na  kuongeza kuwa Serikali imefanya tathimini ya uhakika  hadi ngazi ya kitongoji na kubaini kuwa kipo chakula cha kutosha katika sehemu kubwa ya nchi.

Alisema kilichotokea ni kupanda kwa bei ya nafaka ya aina ya mahindi pekee kwenye baadhi ya maeneo na  hii ilitoka na baadhi ya wakulima kuuza chakula kufuatia bei kubwa iliyotolewa na wafanyabiashara.

“ Kuna watu wamewajengea hofu wananchi kwa kudai kuwa Tanzanai ina uhaba mkubwa wa chakula lakini si kweli kama inavyodaiwa” aliongeza Dkt. Tizeba.

Alibainisha kuwa Tanzania ilikuwa na chakula cha zaidi ya tani milioni tatu kwa msimu wa mwaka 2016/2017.

Kupanda kwa bei ya mahindi si kigezo tosha kuwa nchi inakabiliwa na uhaba wa chakula kwa Taifa letu kama inavyoelezwa na kukuzwa na baadhi ya watu.

Kwa mujibu wa Dkt. Tizeba amesema kuwa   kuna baadhi ya  mikoa ya Songwe,  Mbeya, Iringa, Ruvuma, Rukwa na Katavi ina chakula cha kutosha na  ziada.

Kutonyesha kwa mvua za vuli ipasavyo sio kwamba hali hiyo imeondoa chakula kwenye maghala.

Alitoa mfano wa zao la mpunga kuwa   unauzwa kwa bei  nafuu  katika sehemu mbalimbali za nchi.

Dkt Tizeba amedai kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara wamefungia maelfu ya tani ya mahindi wakisubili wauze kwa bei ya juu.

Mhe. Tizeba amewahakikishia wananchi kuwa nchi bado ina chakula cha kutosha kwa sasa na kwa hiyo wasiwe na hofu.

Pia amewaasa wananchi kuondoa utamaduni wa kupenda kula na kutambua  baadhi ya vyakula kuwa ndo chakula kwa baadhi ya makabila na kuona vyakula vingine si vyakula katika jamii fulani.

Ametoa wito kwa wananchi wale wenye chakula cha akiba wakitumie vizuri ili kuweza kukabiliana na hali inayoweza kujitokeza hapo baadaye.

Kauli hii ya Dkt. Tizeba inakuja siku chache baada ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kulitangazia Taifa kuwa hakuna njaa hapa nchini kwa kuwa kuna chakula cha kutosha, kauli hiyo aliitoa akiwa katika ziara kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com