METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, June 16, 2020

WATAALAMU WAHIMIZWA KUTENGENEZA SERA BORA YA WAJASILIAMALI WADOGO (SME POLICY) ILI ZITUMIKE KUTATUA CHANGAMOTO ZA WAFANYABIASHARA NCHINI: PROF. RIZIKI SHEMDOE



Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe amefungua kikao kazi cha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi ambao wamekutana kwa ajili ya mapitio ya Sera ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo (SME Policy 2003).

Prof. Shemdoe amesema kwamba Wizara ya Viwanda na Biashara kwa sasa inatekeleza andiko la kuboresha mazingira ya Biashara nchini “Blue print”  ambayo imeondoa vikwazo vya kibiashara na kuweka mazingira mazuri kwa wajasiliamali, wawekezaji na wafanyabiashara wote kwa ujumla hivyo kikosi kazi hiki kitasaidia Wizara kuwa na Sera bora ambayo itazingatia hali ya sasa kwani Sera iliyopo ambayo ni ya mwaka 2003 mambo mengi yamepitwa na wakati hivyo kushindwa kutatua changamoto nyingi zinazowakabili wajasiliamali wadogo nchini ambao ndio chachu ya kuchochea uchumi wa nchi.

"Nafasi za ajira nyingi zipo kwa wajasiriamali wadogo hivyo Sera hii itasaidia kutatua changamoto za wafanyabiashara wetu hasa katika suala la upatikanaji wa mikopo yenye riba na masharti nafuu ili kuwawezesha kufanya biashara katika masoko ya ndani na nje ya nchi yakiwemo masoko ya COMESA, SADC, EAC n.k ," alisisitiza Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe amepongeza jitihada zinazofanywa na Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Nchini (FSDT) hapa nchini kwani ndio waliofanikisha kikosi kazi hiki kukutana na kufanya kazi hii ya mapitio ya maandiko mbalimbali ili kurejea Sera ya Viwanda Vidogo na Biashara ndogo. Pia ameipongeza Sekta binafsi katika kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara katika marejeo ya sera hii kwani sekta binafsi ndio nguzo ya kusaidia wajasiliamali wadogo nchini kujikwamua. kwa ushirikiano huu tunatarajia kupata Sera bora na wezeshi kwa wafanyabiashara wadogo ambao ndio kundi kubwa lililojiali.

Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye amesema kuwa yeye na taasisi anayoiongoza ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kuja na mapitio ya Sera hii ambayo ni ya mwaka 2003 hivyo Sera mpya itakayopatikana itatoa mwongozo wa Wafanyabiashara wadogo.

Aliongeza kwa kusema kuwa Sera hii ina umuhimu mkubwa kwa mstakabali wa maendeleo ya nchi yetu kwani Wafanyabiashara wadogo ndio nguzo ya uchumi ya taifa letu hivyo Sera mpya inatakiwa kuwa wezeshi kusaidia Wajasiriamali wote nchi nzima.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Nchini (FSDT) Bw. Sostenes Kewe amesema Wafanyabiashara wadogo ndio injini ya uchumi wan chi hii na mitaji ndio changamoto kubwa ya kuwafanya kuendelea kibiashara, ujio wa sera mpya itasaidia kutengeneza mazingira bora kwa wajasiliamali, Napongeza Juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania za kuboresha na kujenga miundombinu hasa ya barabara, Afya, maji na Umeme zimesaidia sana wajasiriamali kusogea kutoka eneo moja kwenda eneo jingine kimaendeleo.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara Ludovick Nduhiye akimkaribisha Katibu Mkuu katika Ufunguzi wa Kikao kazi hiki cha mapitio ya Sera ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo (SME Policy) ameishukuru Sekta binafsi (TPSF) pamoja na Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Nchini (FSDT) kwa kusema kuwa “hiki kinachofanyika leo ni matokeo mazuri ya ushirikiano uliopo na unaoendelea kati ya Serikali na Sekta binafsi katika kutatua changamoto kwa Wajasiriamali nchini”.

Kikao kazi hiki kinafanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Nashera Mkoani Morogoro.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com