
Mratibu wa Tamasha la Simiyu Jambo
Festival Bi. Zena Mchujuko(kulia) akizungumza na waandishi wa habari na
kutoa taarifa ya tamasha hilo ambalo linatarajiwa kufanyika Juni 30,
2019 Mjini Bariadi.

Kiongozi wa Ngoma za Asili, Bw.
Buhimila Shala (kushoto) akizungumza katika Mkutano wa Waandishi wa
Habari na kueleza namna ngoma za asili zitakavyopamba Tamasha la Simyu
Jambo Festival ambalo linatarajiwa kufanyika Juni 30, 2019.

Katibu wa Chama cha Baiskeli Mkoa
wa Simiyu, Bw. Samwel Richard(kulia) akizungumza na waandishi wa habari
juu ya namna chama hicho kilivyojiandaa na mashindano ya baiskeli katika
Tamasha la Simiyu Jambo Festival, linalotarajiwa kufanyika Juni 30,
2019
********************
Na Stella Kalinga, Simiyu
Tamasha kubwa la michezo ambalo
hufanyika kila mwaka Mkoani Simiyu (Simiyu Jambo Festival) linatarajiwa
kufanyika Juni 30, mwaka huu katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa
Bariadi huku takribani shilingi milioni 32 zikishindaniwa.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo Juni 25, Mratibu wa tamasha hilo Bi. Zena Mchujuko amesema
Mgeni rasmi katika Tamasha hili anatarajiwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson.
Amesema katika Tamasha hilo
kutafanyika mashindano ya mbio za baiskeli wanaume na wanawake, mbio
fupi kilometa tano wanaume na wanawake na mashindano ya mdahalo kwa
wanafunzi wa shule za sekondari.
“Jumla ya shilingi milioni 32
zitashindaniwa kwa michezo yote, mshindi wa kwanza mbio za baiskeli kwa
wanaume atapata 1,000,000, Wanawake 700, 000, walemavu 500, 000 na
tutatoa zawadi mpaka kwa mshindi wa 25; ngoma za asili mshindi atapata
1,000,000” alisema Bi. Zena
Aidha, amesema fomu za ushiriki zinapatikana kataika ofisi ya Chama cha Baiskeli Mkoa wa Simiyu Mjini Bariadi na katika Tovuti: www.simiyutalent.co.tz
kwa gharama za shilingi elfu tano(5000) kwa mashindano ya baiskeli na
shilingi elfu mbili (2000) kwa ajili ya mashindano ya mbio fupi.
Katika hatua nyingine Bi.
Mchujuko amesema kupitia Tamasha la Simiyu Jambo Festival jamii ya watu
wa Simiyu itapata ujumbe wa kupinga mimba za utotoni jambo
litakalopelekea watoto wa kike waweze kutimiza ndoto zao kupitia Kauli
Mbiu ya Tamasha ambayo ni :-WEZESHA MTOTO WA KIKE ATIMIZE NDOTO ZAKE, INAWEZEKANA KUZUIA MIMBA KATIKA UMRI MDOGO”
Mratibu wa Shirika la Umoja wa
Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu Duniani(UNFPA) Mkoa wa Simiyu,
Dkt. Amir Batenga amesema shirika hilo limekuwa likishirikiana na
Serikali katika jitihada za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, ambapo
waathirika wakubwa ni wasichana wenye umri mdogo, hivyo anaamini kupitia
Tamasha hilo wananchi watapata ujumbe mahususi wa kukabiliana na mimba
katika umri mdogo.
Naye Katibu wa Chama cha Mbio
za Baiskeli Mkoa wa Simiyu, Bw, Samwel Richard washiriki takribani 260
kutoka mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara, Mwanza, Geita na Kagera
wanatarajia kushirikia mashindano ya baiskeli, huku akiwahakikishia
wananchi kuwa wachezaji wao wamejiandaa vizuri na wamekuwa kambi kwa
takribani wiki mbili.
Kwa upande wake Kiongozi wa
Ngoma za Asili Mkoa wa Simiyu, Bw. Buhimila Shala amesema kupitia ngoma
za wagika na wagalu watatoa ujumbe uliobebwa na Kauli mbiu ya Tamasha
kwa lengo la kuwaokoa wasichana kupata mimba katika umri mdogo.
Tamasha la Simiyu Festival
mwaka 2019 limedhaminiwa na Jambo Food Products Company, Shirika la
Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani-UNFPA, NGM Gold
Mine Limited, NGS Petroleum, Alliance Ginneries Limited, Busega Mazao
Limited, Maswa Standard Chalk, Ms Hotel na Vetreces Company Limited.
0 comments:
Post a Comment