METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, June 16, 2020

CHRAGG ANGALIENI ENEO LA UNYANYASAJI WA KIJINSIA HAPA ZANZIBAR- WAZIRI RASHID



Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibari, Mhe. Hamad Rashid Mohammed amesema kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, inatekeleza kazi kubwa katika kutoa haki za binadamu kwa kutoa ripoti ambazo zinahusu masuala ya haki za watu na ameitaka kujikita zaidi kwenye masuala ya kijamii hususani unyanyasaji wa kijinsia kwani ni tatizo kwa Zanzibar.

Akizungumza na ujumbe wa watendaji wa juu wa Tume hiyo Ofisini kwake Mjini Unguja Zanzibar, Waziri Rashid alisema kuwa siku za nyuma utekelezaji wa haki za binadamu hususani masuala ya unyanyasaji wa kijinsia ilikuwa ni ngumu kwani utekelezaji wa ripoti za tume hiyo zilikuwa hazifanyiwi kazi tofauti na sasa.
 
“Siku za nyuma mlikuwa mkiandika, kutoa na kusoma ripoti lakini zilikuwa hazifanyiwi kazi, sasa hivi kidogo utekelezaji wa ripoti mnazoandika na  kuziwasilisha zimekuwa na msaada zaidi kwa jamii, kwani haki za binadamu hasa unyanyasaji wa kijinsia wananchi  wamekuwa na mwamko wa kutafuta msaada wa upatikanaji wa haki baada ya chombo chenu hiki kufanya kazi kubwa ya kuwaelimisha wapi wanaweza kupata msaada wa haki zao”, Waziri Rashid.

Alisema, kuwa kuna maeneo Zanzibar ambayo wananchi wanahitaji kupata haki zao za msingi hususani kwenye eneo la unyanyasaji wa kijinsia na ucheleweshwaji wa haki za binadamu katika baadhi ya Taasisi za kutoa na kusimamia haki nchini.

Naye, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, alisema kuwa ziara yake Zanzibar inalenga hasa kujifunza mambo mengi na kupata ushirikiano kwa Serikali na Taasisi zake katika utekelezaji wa haki za binadamu nchini.

“Katika ziara yetu hii tumejifunza mambo mengi sana na kila tulipoenda tumeambiwa mambo mengi sana na tunatakiwa kuyafanyia kazi sisi kama tume ili kuwezesha wananchi wa Zanzibar kupata haki zao za msingi kila panapohitajika”, Jaji Mstaafu Mwaimu.

Alibainisha, kuwa utekelezaji wa ripoti za tume hiyo hapo mwanzo ulikuwa mgumu lakini kwa sasa hivi mambo yemebadilika na sasa kila mtu anatenda kazi yake ipasavyo hasa akipokea ripoti hizo ambazo zimekuwa zikitolewa na tume hiyo kuhusu masuala ya haki za binadamu.

Aliongeza, kuwa tume hiyo inapita katika Ofisi za Serikali na Taasisi zinazotoa na kutekeleza haki za binadamu ili kupata uhusiano na ushirikiano mkubwa kwa Serikali na kuwezesha wananchi wote kupata haki zao katika masuala mbalimbali ya kijamii.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com