
Kaimu Balozi wa Saudi Arabia
nchini Tanzania Ahmad Saleh Ghamdi akimkabidhi Waziri wa Afya Hamad
Rashid Muhamed mashine za kusafishia Figo katika sherehe zilizofanyika
Bohari Kuu ya Dawa Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Hamza (kushoto) akiwa na Waziri
wa Afya Hamad Rashidi na Naibu wake Harusi Suleiman na Naibu Katibu Mkuu
wa Wizara hiyo Halima (kulia) wakiangali mashine za kusafishia Figo
zilizotolewa na Serikali ya Saudia Arabia katia Bohari kuu ya Dawa
Maruhubi.

Baadhi ya mashine za kusafishia
Figo zilizotlea na Serikali ya Saudi Arabia kwa ajili ya kutoa huduma
katika Hospitali za Zanzibar.

Waziri wa Afya Hamad Rashid
Muhamed akitoa shukrani baada ya kupokea mashine 17 za kusafishia Figo
zilizotolewa na Serikali ya Saudi Arabia (kulia) ni Naibu Waziri wa Afya
Harusi Suleiman na kushoto Kaimu Balizi wa Saudi Arabia nchi Tanzania
Saleh Ghamdi
*******************
Na Ramadhani Ali – Maelezo 25.6.2019
Serikali ya Saudi Arabia imetoa
msaada wa mashine 17 za kusafishia Figo (Dialysis Machines) kwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar zenye thamani ya shilingi milioni 400.
Kaimu Balozi wa Saudi Arabia
nchini Tanzania Ahmed Saleh Ghamdi alimkabidhi Waziri wa Afya Zanzibar
Hamad Rashid Muhamed msaada huo katika hafla iliyofanyika Bohari Kuu ya
Dawa Marughubi.
Kaimu Balozi Ahmed alimpongeza
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Muhamed
Shein na Serikali yake kwa juhudi kubwa wanazochukua katika kuimarisha
uchumi na sekta ya afya.
Alisema Serikali ya nchi yake
itaendelea kuunga mkono juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar hasa katika kukuza sekta ya afya na elimu ambazo
ni muhimu katika kuimarisha ustawi wa wananchi.
Aliongeza kusema kuwa Serikali ya
Saudi Arabia itafikiria kutoa nafasi za masomo kwa madaktari wa Zanzibar
hasa katika fani ambazo bado zinaupungufu wa wataalamu ili ziweze
kuimarika katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
Waziri wa Afya Hamad Rashidi
Muhamed aliipongeza Serikali ya Saudi Arabia kwa misaada mbali mbali
inayotoa kwa Zanzibar ikiwemo ya kuimarisha huduma za afya nchini.
Alisema mashine 17 za kusafishia
Figo zilizotolewa na Serikali ya nchi hiyo zitawapunguzia na
kuwarahisishia kazi watendaji na wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo
kuipata kwa urahisi.
Aliongeza kuwa Zanzibar kama
zilivyo nchi nyengine zinazoendelea, wagonjwa wa maradhi yasiyoambukiza
ikiwemo matatizo ya Figo imekuwa ikiongezeka na kunahitajika kuongeza
huduma za kuwahudumia wagonjwa wanaokabiliwa na matatizo hayo.
Alisema baada ya kupatikana msaada
wa mashine hizo 17, Wizara itapeleka mashine 10 Pemba na inakusudia
kuanzisha huduma ya kusafisha Figo
katika hospitali nyengine za Unguja ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali kuu ya Mnazimmoja.
Msaidizi Muuguzi wa Kitengo cha
Figo Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Zainab Ismail alisema kuongezeka kwa
idadi ya mashine za kusafishia Figo katika Kitengo hicho
kutawarahisishia utendaji wa kazi na wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo
kuipata kwa haraka.
Alisema kazi ya kusafisha Figo
huchukua karibu saa nne kwa mgonjwa mmoja na idadi ya wagonjwa waliopo
Zanzibar hivi sasa ni wengi hivyo kulikuwa na umuhimu mkubwa kupata
mashine nyengine kurahisisha utoaji wa huduma katika Kitengo hicho.
0 comments:
Post a Comment