Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Dkt. Titus Kamani,
akizungumza na viongozi wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Walimu Same (Same
Teachers SACCOS).
Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Kilimanjaro, John Henjewele
akizungmza wakati wa Kikao cha Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika
Tanzania Dkt. Titus Kamani, na Wajumbe wa Bodi ya Chama cha Akiba na
Mikopo cha Walimu Same (Same Teachers SACCOS).
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Dkt. Titus Kamani,
(Wa nne kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi
ya Chama cha Akiba na Mikopo cha Walimu Same (Same Teachers SACCOS).
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Dkt. Titus Kamani,
(Wa nne kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji
wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Walimu Same (Same Teachers SACCOS).
Chama
cha Akiba na Mikopo cha Walimu Same (Same Teachers SACCOS), kinaunganisha
wafanyakazi wa Serikali wilaya ya Same ambacho kilianzishwa na wanaushirika walimu
na baadaye walikubaliana kufungua wigo wa kupokea wafanyakazi toka Idara
nyingine ambao kwa sasa fungamano lao ni
wafanyakazi wa serikali wilaya ya Same.
Same Teachers SACCOS
kimejiendeleza na kujiimarisha kwa kukuza mtaji wake wa ndani kufikia Shilingi
Bilioni moja na milioni mia saba (1.7 Bilioni) na
kuongeza idadi ya wanachama kwa kila mwaka ambapo
kufikia tarehe 30/09/2019 chama kina idadi ya wanachama 1,533 (wanaume 764 na wanawake
769). Idadi hii ya wanachama inajumuisha wanachama waliopo kazini, waliostaafu
na waliohama ambao hawajachukua hisa zao.
Taarifa
ya Same Teachers SACCOS iliyosomwa na
Mwenyekiti wa Bodi, Mwalimu Omari Mchome, kwa Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo
ya Ushirika Tanzania Dkt. Titus Kamani, ilionyesha kuwa chama hicho kimefanikiwa
kutoa huduma za kifedha kwa wanachama kama vile (ukusanyaji wa hisa, Akiba,
Amana na Viingilio) na utoaji wa mikopo mbalimbali ili kuwawezesha wanachama
wake kiuchumi.
“Chama
cha Akiba na Mikopo cha Walimu Same kimefanikisha ustawi wa jamii hasa elimu,
makazi bora, biashara kilimo na miradi mingine mbalimbali hatimaye kupunguza
umaskini kwa wanachama wake kwa kiasi kikubwa. Chama kimekuwa kikitoa elimu
kila mwaka ili kupata ufahamu zaidi juu ya ushirika na Asasi nyingine za fedha,”
alisema Mwalimu Mchome.
Dkt.
Kamani alifanya ziara ya kikazi hivi karibuni mkoani Kilimanjaro kujionea
maendeleo na changamoto za vyama vya ushirika ambapo akiwa wilayani Same
amewapongeza Walimu na Watumishi wengine wa wilaya hiyo kuanzisha na kusimamia
vizuri SACCOS yao ambayo imepata mafanikio makubwa.
“Nawapongeza
Walimu kwa kuanzisha na kusimamia vizuri SACCOS yenu na kupata mafanikio makubwa; ningeshangaa
kama SACCOS ya Walimu ambao ni Wataalam tunaowategemea kama kioo cha jamii,
mngeshindwa kuwaleta watumishi pamoja na kupata suluhisho la mtaji,” alisema
Mwenyekiti wa Tume ya Ushirika.
Jumla
ya mikopo yote iliyotolewa na Same Teachers
SACCOS tangu chama kianzishwe hadi kufikia tarehe
30 Septemba 2019 ni shilingi bilioni kumi na tano, milioni mia tisa thelathini
na tatu laki saba ishrini na saba mia nane arobaini na tano (15,933,727,845/).
Mikopo hii inalenga kuwakwamua wanachama katika shughuli mbalimbali kama vile
Kilimo na Ufugaji, malipo ya Ada za shule kwa watoto na wao wanapokwenda
kujiendeleza, Ujenzi, Biashara, Ununuzi wa vyombo vya usafiri, na kutatua
matatizo ya kijamii kama kusaidia kipindi cha ugonjwa.
Aidha, Chama hiki kimeweza kutoa misaada kwa jamii inayowazunguka
kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo ambapo kimetoa vifaa viwili vya kusaidia
kupumua (oxygen flow metre), shuka 200 na blanketi 200 kwa hospitali ya wilaya
ya Same.
0 comments:
Post a Comment