Mbunge wa
Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amezindua kampeni ya uhamasishaji wa
uvaaji wa barakoa, unawaji mikono wa mara kwa mara na uchukuaji wa tahadhari
dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 unaoenezwa na kirusi cha Corona kwa madereva wa
daladala, makondakta na abiria katika mkoa wa Mwanza.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika ofisi za chama cha
madereva mkoa wa Mwanza (MWAREDDA) Mhe Dkt Mabula amekipongeza chama hicho kwa
kuunga mkono jitihada za Serikali inayoongozwa na Rais Mhe Dkt John Magufuli
katika kupambana na ugonjwa wa Covid-19 unaosumbua dunia kwa sasa, Na kuongeza
kuwa Serikali inatambua changamoto wanazokutana nazo na itaendelea kuzitafutia
ufumbuzi moja baada ya nyengine huku akiwataka madereva na makondakta hao kuendelea kuwa wamoja
‘.. Siku zote unapopigania haki mkiwa wengi mnakuwa na nguvu tofauti na
mnapokuwa mmoja mmoja, Tutumie vyama vyetu kuiomba Serikali na taasisi zake
mfano idara ya kazi kutukutanisha na waajiri wetu kumaliza kero zinazotukabili
..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula akaunga mkono juhudi za chama hicho katika mapambano dhidi
ya ugonjwa wa Covid-19 kwa kukabidhi barakoa 400 zitakazovaliwa na madereva na
makondakta ili kujikinga na ugonjwa wa Covid-19, Pamoja kutoa
kompyuta moja kwaajili ya utekelezaji wa shughuli za kila siku za chama
hicho.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha madereva (MWAREDDA) mkoa wa Mwanza
Ndugu Mjalifu Kezilaabi Manyasi
amemshukuru mbunge huyo kwa kujitoa kwake katika kutekeleza shughuli za
maendeleo na utatuzi wa kero za wananchi huku akimuomba kuendelea kufanya
hivyo, Wakati katibu wa chama hicho Ndugu Samson Matayo akitaja changamoto
mbalimbali zinazokabili chama chao ikiwemo ukosefu wa bima ya afya, mshahara
mdogo, kuachishwa kazi bila kufuata taratibu za kisheria, ukosefu wa mikataba
ya kazi na upungufu wa vitendea kazi kama kompyuta na shajara.
Uzinduzi wa kampeni ya uvaaji barakoa kwa wasafirishaji na wasafiri mkoa wa
Mwanza ulipambwa na shughuli ya ugawaji bure barakoa zaidi ya 1,200 kwa
wananchi na wasafirishaji zoezi lililoongozwa na mbunge huyo wa jimbo la
Ilemela akishirikiana na wauzaji wa mafuta kutoka kituo cha mafuta Munuo.
0 comments:
Post a Comment