Na Nuru Juma na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Shirika la usafiri wa Anga Tanzania
(ATCL) limetoa fursa kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora)
kuzungumza na mashirika ya ndege ya nchi wanazoishi ili kuunganisha
watanzania kufanya kazi na nchi hizo.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam
na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Mhandisi Ladislaus Matindi alipokuwa
akizungumza na wajasiriamali na wananchi katika mdahalo wa Diaspora
uliofanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa.
Mhandisi Matindi alisema kuwa Diaspora
wanatakiwa kuanza kutumia fursa zinazopatikana katika usafiri wa anga
ili kusaidia watanzania kufaidika na shirika hilo kwani ni sekta
inayotoa ajira kwa Watanzania wengi.
“Shirika la ndege linahitaji wauza
tiketi, wauza chakula, wasafirishaji na wapokeaji wa mizigo pamoja na
wauzaji wa spea za ndege, hivyo Watanzania walioko nchini pamoja na
DIASPORA wanatakiwa kushirikiana ili kupata watu wenye taaluma
mbalimbali watakaofanya kazi na shirika hilo,” alisema Matindi.
Mhandisi Matindi ameongeza kuwa ATCL ipo
tayari kushirikiana na Diaspora katika kujenga uchumi wa nchi kwa
kuangalia fursa ambazo wengi hawafahamu kama zipo nchini Tanzania.
Aidha, Mtendaji Mkuu huyo aliwataka
Watanzania wanaomaliza masomo ya masuala ya ndege nje ya nchi kurudi
nyumbani ili waweze kuajiriwa na shirika hilo kwa ajili ya kuongeza
wataalamu nchini na kukuza uchumi wa Nchi.
Vile vile amewataka watanzania kuelewa
kuwa ununuzi wa ndege ni kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi na si
ufujaji wa fedha kama Watanzania wengi wanavyodhani pia ametoa rai kwa
Watanzania kutumia usafiri wa shirika hilo kwani unatoa huduma sawa na
mashirika mengine tena kwa gharama zinazokidhi mahitaji ya Mtanzania.
Mnamo mwaka 2016, Serikali ilianza
kuwekeza katika kufufua Shirika la Usafiri wa Anga Tanzania kwa kuanza
kununua ndege mbili mpya. Aidha Serikali ina mpango wa kuongeza ndege
mbili za saizi ya kati zenye uwezo wa kubeba abiria 132 na moja kubwa
yenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 264 ifikapo mwaka 2018.
0 comments:
Post a Comment