METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, May 11, 2020

WAZIRI HASUNGA AAGIZA NFRA KUNUNUA CHAKULA MSIMU HUU NA KUKIHIFADHI KWENYE VIHENGE VIPYA VYA MJINI BABATI


 
Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga akiongea na Watumishi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA Kanda ya Arusha) jana wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa vihenge vya kisasa (Silos) pamoja na maghala eneo la Maisaka wilayani Babati mkoani Manyara kulia kwake ni Mhe. Elizabeth Kitundu Mkuu wa Wilaya ya Babati na kushoto kwake ni Mtendaji Mkuu wa (NFRA) Bwana Milton Lupa 
Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga akimsikiliza Mhandisi wa  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Imani Nzobonaliba jana wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa vihenge vya kisasa (Silos) pamoja na maghala eneo la Maisaka wilayani Babati wengine pamoja naye ni Mhandisi Radoslaw Osowieski kutoka Kampuni ya ARAJ Realizacje kutoka nchini Poland 
Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga akimsikiliza Mhandisi wa  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Imani Nzobonaliba jana wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa vihenge vya kisasa (Silos) pamoja na maghala eneo la Maisaka wilayani Babati wengine pamoja naye ni Mhandisi Radoslaw Osowieski kutoka Kampuni ya ARAJ Realizacje kutoka nchini Poland mwengine nyuma ya Waziri ni Mwakilishi wa Wakala wa Majengo (TBA) Babati Bwana Albert Timira
Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga akiwa amepanda ili kuangalia ndani ya kihenge cha kisasa pamoja na Mhandisi wa  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Imani Nzobonaliba jana eneo la Maisaka wilayani Babati
Sehemu ya vihenge vya kisasa ambavyo vimejengwa katika eneo la Maisaka mkoani Manyara ulianza rasmi Mwezi Disemba, 2018 Mradi unatekelezwa kutokana na fedha za mkopo nafuu kutoka Serikali ya Poland ambapo Kampuni ya ARAJ Realizacje kutoka nchini Poland ilishinda  kandarasi hiyo ikishirikiana na Mkandarasi wa ndani Kampuni ya ELERAI Construction ya Jijini Arusha.

Waziri wa kilimo Mhe. Japhet Hasunga amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Bwana Milton Lupa kuwa chakula kitakachonunuliwa katika Kanda ya Arusha kihifadhiwe kwenye vihenge vipya ambavyo vimekamilika kwa zaidi ya asilimia 94.

Waziri Hasunga ameyasema hayo leo (Jana) Jumamosi, tarehe 9 Mei, 2020 alipotembelea ili kukagua ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa katika makao makuu ya mkoa wa Manyara; Halmashauri ya Mjini wa Babati. 

Waziri wa Kilimo Mhe. Hasunga aliongeza kuwa NFRA inakiwa kununua mazao mchanganyiko kama mahidi, maharage na mpunga.

“Chakula si mahindi pekee yake; msimu huu wa ununuzi unaokuja jitahidini, kununua mazao mchanganyiko kama mahindi, maharage na mpunga ili kama kuna dharura inatokea, msaada wa chakula mtakaotoa, uwe ni chakula kamili kwa wenye uhitaji”. Amekaririwa Waziri Hasunga.

Waziri Hasunga ameongeza kuwa ujenzi wa vihenge vya kisasa (Silos) pamoja na maghala mawili ya kisasa wilayani Babati utaifanya NFRA – Kanda ya Arusha ambayo inahudumia mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro kuongeza akiba ya taifa ya chakula kutoka tani 39,000 hadi tani 79,000.

Katika taarifa yake; Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Bwana Milton Lupa, amesema ujenzi wa Mradi wa vihenge vya kisasa unatekelezwa kwenye viwanja vya NFRA eneo la Maisaka ambapo ulianza rasmi Mwezi Disemba, 2018 na kwamba unatekelezwa kutokana na fedha za mkopo nafuu kutoka Serikali ya Poland ambapo Kampuni ya ARAJ Realizacje kutoka nchini Poland ilishinda  kandarasi hiyo na inashirikiana na Mkandarasi wa ndani (Sub-Contractor) Kampuni ya ELERAI Construction ya Jijini Arusha.

Kanda ya Arusha ni miongoni mwa Kanda saba (7) za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula na ni kati ya Kanda 6 zinazotekeleza Mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka. Mradi huu unatekelezwa katika Mikoa minane (8) ya Tanzania Bara ikiwemo Mkoa wa Manyara.  Kanda ya Arusha kupitia mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi, unaendelea na ujenzi mpya wa vihenge 8 vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 25,000 na maghala mawili yenye uwezo wa kuhifadhi tani 15,000.  Mradi ukikamilika Wakala katika kanda ya Arusha itakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 40,000; hivyo kuongeza uwezo wa kuhifadhi wa kanda kufikia jumla ya tani 79,000.

Kazi zinazotekelezwa kwenye Mradi huo ni pamoja na usanifu na ujenzi wa vihenge nane (08) vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 25,000. Usanifu na ujenzi wa maghala mawili yenye uwezo wa kuhifadhi tani 15,000; Usanifu na ujenzi wa majengo ya utawala, maabara, kantini, stoo ya viuatilifu na vifaa, vyoo na bafu; Usanifu na ujenzi wa barabara za ndani na miundombinu ya kutoa maji (Drainage System).

Kazi zingine ni pamoja na ununuzi wa vifaaa vya maabara na stoo; Usanifu na ujenzi wa uzio wa eneo la mradi; Tanki la kuhifadhia maji lenye uwezo wa lita 10,000 pamoja na mafunzo ya kujenga uwezo kwa Wataalamu wa NFRA.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com