Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akisisitiza jambo wakati akikagua
shamba la korosho la mkulima Juma Patrick wa Kijiji cha Sanjaranda halmashauri
ya Wilaya ya Itigi.
Mkulima Juma Patrick wa Kijiji cha Sanjaranda halmashauri ya Wilaya ya
Itigi akimuonyesha Mkuu wa Mkoa wa Singida mikorosho iliyostawi katika shamba
lake.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya
Manyoni Miraji Jumanne Mtaturu wakiwa katika shamba la korosho la mkulima Juma
Patrick wa Kijiji cha Sanjaranda halmashauri ya Wilaya ya Itigi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida amewataka watumishi wa umma wote mkoani
hapa kulima ekari moja ya korosho ili kutunza mazingira, kujiongezea
kipato pamoja na kuonyesha mfano kwa wananchi wengine ili waweze kulima
zao hilo kwa ufanisi.
Dkt Rehema Nchimbi ametoa agizo hilo mapema wiki hii mara baada ya
kutembelea na kukagua shamba la mkulima wa zao hilo Juma Patrick katika
kijiji cha Sanjaranda halmashauri ya wilaya ya Itigi.
Dkt Nchimbi amesema kuongoza ni kuonyesha njia hivyo watumishi wa
umma wanatakiwa kuonyesha njia kwa kulima vizuri hasa katika mazao ya
biashara yanayopewa kipaumbele kitaifa ambapo kwa mkoa wa Singida ni
korosho, pamba na tumbaku.
“Watumishi hamuwezi kuwaambia wakulima walime korosho au pamba wakati
wewe haujalima wala haufahamu changamoto na faida za kilimo hicho,
naagiza kila mtumishi alime ekari moja ya korosho ili muwe mabalozi
wazuri wa zao hilo mkoani hapa”, amesisitiza Dkt Nchimbi.
Aidha Dkt Nchimbi ametoa wito kwa wananchi wote kuchangamkia fursa ya
kilimo cha korosho kwakuwa ndio mkombozi wa kutunza mazingira kwa mkoa
huu pamoja na kuinua pato lao.
Amesema pembejeo na miche ya zao hilo inatolewa bure hivyo mwananchi
hataingia gharama nyingine zaidi ya kuandaa shamba lake ambalo atavuna
mara baada ya miaka mitatu tangu kupanda na kuendelea kuvuna kwa zaidi
ya miaka 50.
“Wananchi korosho ni zao zuri sana, serikali ya awamu ya tano inatoa
mbegu na pembejeo bure, nyie andaeni mashamba yenu tu lakini pia ukianza
kuvuna korosho yako hiyo baada ya miaka mitatu utaendelea kuvuna kwa
zaidi ya miaka hamsini, hii ni faida kubwa sana.
Dkt Nchimbi amefafanua kuwa Mkoa wa Singida umejipanga kuifanya
korosho kuwa zao la kudumu la biashara mkoani hapa na kuwa mzalishaji
mkubwa nchini wa korosho.
Kwa upande wake mkulima Juma Patrick wa kijiji cha Sanjaranda
halmashauri ya wilaya ya Itigi amesema anamiliki ekari 11 za korosho
ambapo kwa msimu wa mwaka 2015/2016 alivuna kilo 410 na msimu wa mwaka
2016/2017 alivuna kilo 826.
Patrick amesema mavuno yamekuwa ni kidogo kutokana na kutopata elimu
ya kilimo hicho huku akiwa hafahamu namna ya kupata soko la korosho yake
licha ya kuwa ardhi na mazingira ya Singida yanastawisha korosho
vizuri.
Aidha amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kukagua shamba lake na kwa agizo
lake la kuwataka watendaji wa halmashauri kuwatembelea wakulima ili
wawape pembejeo na elimu ya kilimo bora cha korosho.
Patrick ametoa wito kwa wananchi wote hasa vijana kuchangamkia kilimo
cha korosho kwa kuwa ni zao ambalo linastawi vizuri, linatunza
mazingira na kukuza uchumi pamoja na kutohitaji uangalizi mkubwa hivyo
kutoa nafasi ya kuendelea na shughuli nyingine huku ukiwa umepanda
korosho.
0 comments:
Post a Comment