METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, January 6, 2026

VYUO VIKUU VYAZINDUA MRADI WA KIMKAKATI KUKABILI MSONGO WA MAWAZO KWA VIJANA

 

‎Na. Meleka Kulwa- Dodoma.

‎Katika hatua inayotajwa kuwa mwanga mpya kwa vijana wanaokabiliwa na changamoto za afya ya akili, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimezindua rasmi mradi wa u’GOOD TevuAfya, unaolenga kushughulikia kwa vitendo matatizo ya afya ya akili kwa vijana, hususan wanaoishi mijini na pembezoni mwa miji.

‎Uzinduzi wa mradi huo umefanyika Januari 6, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Afrika Mashariki, ukihusisha viongozi wa chuo, watafiti, wadau wa maendeleo pamoja na wanafunzi.

‎Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Mkuu wa UDOM, Profesa Lughano Kusiluka, amesema mradi wa u’GOOD TevuAfya ni miongoni mwa miradi 23 ya kimataifa inayotekelezwa chini ya programu ya Good Life, huku miradi minane ikitekelezwa Tanzania.

‎“Takwimu hizi zinaonesha wazi kuwa Tanzania inaendelea kujijengea heshima na nafasi muhimu katika ramani ya utafiti wa kisayansi duniani,” amesema Profesa Kusiluka.

‎Ameeleza kuwa ushindani wa kupata ufadhili wa miradi ya utafiti ni mkali, hivyo mafanikio ya watafiti wa Tanzania kupata miradi hiyo yanaonesha ubora wa kazi na umuhimu wa tafiti zinazolenga kutatua matatizo halisi ya jamii.

‎Kwa mujibu wa Profesa Kusiluka, changamoto za afya ya akili kwa vijana zimeongezeka kwa kasi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo hali ngumu za kiuchumi, mabadiliko ya mifumo ya kifamilia, msongo wa mawazo, matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii pamoja na kasi ya maendeleo ya teknolojia za kidijitali.

‎“Afya ya akili si tatizo la vijana pekee, ni suala la jamii nzima. Familia, wazazi na mazingira yanayowazunguka vijana vina mchango mkubwa,” amesema, akisisitiza umuhimu wa tafiti shirikishi zitakazosaidia kupata suluhisho endelevu.

‎Aidha, ametoa wito wa kuimarishwa kwa elimu ya uraia kwa vijana ili kuwajengea uzalendo, kujiamini na kuiona Tanzania kama nchi ya fursa na matumaini, akibainisha kuwa misingi ya maadili na utambulisho wa kitaifa ina mchango mkubwa katika ustawi wa afya ya akili.

‎Kwa upande wa wanafunzi, Akley Omary wa UDOM amesema afya ya akili ni uwezo wa mtu kukabiliana na mawazo chanya na hasi yanayotokana na changamoto za maisha na mazingira ya kijamii.

‎Amesema wanafunzi wengi hukumbwa na msongo wa mawazo unaotokana na changamoto za kifedha, matatizo ya kifamilia na mazingira magumu ya masomo, huku kukosa mahitaji muhimu kama chakula, vifaa vya masomo na fedha za matumizi vikizidi kuathiri ustawi wao wa kisaikolojia.

‎Naye David Julius, mwanafunzi wa Shahada ya Business Information System, amesema dhana potofu kwamba afya ya akili ni sawa na wazimu imekuwa kikwazo kikubwa kwa vijana kutafuta msaada.

‎“Afya ya akili ni uwezo wa mtu kufanya maamuzi sahihi na kuchanganua mambo kwa ufanisi, kufeli masomo na kushindwa kufanya maamuzi sahihi mara nyingi hutokana na msongo wa mawazo,” amesema.

‎Kwa upande wake, Rebeca Omari Kabanda, mwanafunzi wa Information Security Engineering, amesema ukosefu wa ajira ni moja ya changamoto kubwa zinazowaathiri vijana kisaikolojia, hasa pale matarajio ya maisha baada ya kuhitimu yanapogonga mwamba.

‎Ameongeza kuwa matumizi sahihi ya TEHAMA na mitandao ya kijamii yanaweza kuwa nyenzo muhimu ya kutoa elimu na msaada wa kisaikolojia kwa vijana, akisisitiza umuhimu wa kujiepusha na tabia hatarishi na mahusiano yasiyo rasmi yanayoweza kuathiri afya ya akili na maendeleo ya kielimu.

‎Mradi wa u’GOOD TevuAfya unatarajiwa kutoa mapendekezo ya kisera pamoja na mbinu za vitendo zitakazosaidia kuboresha afya ya akili kwa vijana na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla hatua inayotajwa kuwa muhimu katika kujenga taifa lenye vijana wenye afya njema ya mwili na akili.

Share:

Friday, January 2, 2026

Wednesday, December 31, 2025

EWURA YAWANOA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU ELIMU YA UDHIBITI WA HUDUMA

 

Na Mwandishi Wetu- Dodoma 

Wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Dodoma, leo 31 Desemba 2025, wameishukuru Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa kuwapa mafunzo kuhusu udhibiti wa huduma za nishati na maji.

‎Mwenyekiti wa klabu hiyo, Musa Yusuf, ameipongeza EWURA kwa hatua ya kutoa mafunzo hayo, akibainisha umuhimu wa mkataba wa huduma kwa wateja, uvunaji wa maji ya mvua, na utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia. Amesisitiza kuwa elimu waliyoipata wataitumia kwa kuelimisha umma.

‎“Asanteni sana EWURA kwa elimu hii, hakika imetufungua macho. Wenzangu wote ni mashahidi. Tunaomba mafunzo kama haya yaendelee,” amesema Bw. Yusuf.

‎Kwa upande wake Kaimu Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Wilfred Mwakalosi, amesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kuelewa masuala yanayodhibitiwa na EWURA, kwani yanagusa huduma ambazo kila mwananchi kwa namna moja au nyingine anazitumia.

‎“Ninyi waandishi wa habari ni daraja kati ya EWURA na wananchi, tuendelee kushirikiana katika kuelimisha umma ili kila mtumiaji wa huduma tunazodhibiti ajue haki na wajibu wake”. Amesisitiza Mwakalosi.


Share:

MAKAMU WA RAIS ATOA POLE MSIBA WA BI LAURENCIA MABELLA

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amefika nyumbani kwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu. Leonard Qwihaya, Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam, kutoa pole kufuatia kifo cha Mama mzazi wa Qwihaya Bi. Laurencia Shija Mabella.



Share:

DKT. NATU APONGEZA UBUNIFU NA UBORA WA JARIDA LA HAZINA YETU

 

Na. Joseph Mahumi, WF, Dar es Salaam

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amepongeza ubunifu na ubora wa Jarida la Hazina Yetu Toleo la Tano ambalo limeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Wizara ya Fedha.

Ametoa pongezi hizo wakati akipokea Jarida hilo kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mwamba alisema Jarida hilo ambalo limeendela kuwa bora na kufika kila mahali duniani kwa njia ya kidigitali ni nyenzo muhimu katika kuwasilisha taarifa sahihi, za wazi na kwa lugha inayoeleweka kuhusu shughuli, mafanikio na mipango ya Wizara ya Fedha.

Dkt. Mwamba alipongeza jitihada za Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kwa kuendelea kuboresha mawasiliano na uelimishaji kwa umma pamoja na ubunifu na weledi unaooneshwa katika uandaaji wa Jarida hilo, akibainisha kuwa limeendelea kuwa chombo muhimu cha kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika masuala ya fedha na uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake, Bw. Benny Mwaipaja alisema kuwa Jarida la Hazina Yetu linalenga kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Fedha pamoja na mchango wake katika maendeleo ya Taifa, akiahidi kuendelea kuliboresha ili liwe chombo chenye tija zaidi katika mawasiliano ya serikali.

Jarida la “Hazina Yetu Toleo la Tano” limesheheni maarifa mbalimbali kupitia Makala bora kabisa, habari, matukio ya picha na matangazo mbalimbali na linapatikana kwa njia ya nakala ngumu (hard copies) na nakala tete (soft copies) kupitia mitandao ya kijamii ya Wizara na wadau wengine wa habari pamoja na Tovuti ya Wizara ya Fedha www.mof.go.tz 


Share:

Saturday, December 20, 2025

DKT. MWIGULU AKAGUA HALI YA BANDARI YA BARAZANI MKOANI LINDI

 

Na Mwandishi Wetu- Lindi

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Mchemba leo Desemba 21, 2025 amekagua hali ya bandari ya Barazani mkoani Lindi na kuiagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania kukamlisha kwa haraka michakato ya awali ya kitaalam ya ujenzi wa mradi wa Bandari ya Ngongo wilayani Lindi mkoani Lindi.‎

‎Amesema kukamilika kwa bandari ya Ngongo kutasaidia kuwaondolea adha watumiaji wa bandari inayotumika sasa ya Barazani ambayo hali yake haiendani na mahitaji ya sasa.‎

‎Dkt. Mwigulu ameongeza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa bandari ya Ngongo kutaleta chachu ya maendeleo mkoani humo kwani bandari ya Lindi imeanza kuchangamkiwa na wafanyabiashara, wakiwemo wa nchi jirani.

Share:

Tuesday, December 16, 2025

MRADI WA SHILINGI MILIONI 120 WA VYOO VYA KISASA KUBORESHA USAFI NA AFYA MINADA YA BAHI NA KIGWE

 

 Na Meleka Kulwa – Dodoma

‎Mkurugenzi wa Miradi wa Habitat for Humanity Tanzania, John Massenza, amesema ujenzi wa vyumba vya vyoo vya kisasa katika minada ya Bahi na Kigwe utakapokamilika, utaimarisha mazingira ya biashara, afya, na usafi kwa wafanyabiashara pamoja na wananchi wanaotumia minada hiyo wilayani Bahi, jijini Dodoma.

‎Ziara ya kukagua na kukabidhi maeneo ya ujenzi ilifanyika Desemba 16, 2025, ambapo John Massenza amekabidhi rasmi maeneo ya miradi hiyo kwa wahandisi watakaotekeleza ujenzi wa vyumba vya vyoo katika minada ya Bahi na Kigwe.

‎Amesema kuwa katika mradi huo, kutajengwa majengo ya vyoo pamoja na miundombinu rafiki kwa wanawake, ikiwemo jengo maalumu litakalowawezesha wakina mama kujisitiri wanapokuwa na mahitaji maalumu.

‎Aidha, amesema kuwa katika minada ya Bahi na Kigwe kutajengwa jumla ya vyumba 26 vya vyoo, vikiwemo vyumba 10 kwa wanaume na 16 kwa wanawake, pamoja na tanki la maji kwa kila mradi. Miradi hiyo pia itajumuisha chumba maalumu cha mahitaji ya wanawake, bafu, chumba cha wakina mama wanaonyonyesha, pamoja na ofisi ya wasimamizi wa huduma.

‎Amebainisha pia kuwa vyumba viwili kwa kila mradi vitajengwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu katika minada ya Bahi na Kigwe.

‎Aidha, amebainisha kuwa mradi wa ujenzi wa vyumba vya vyoo katika Mnada wa Bahi utagharimu shilingi milioni 60, huku mradi wa Mnada wa Kigwe ukigharimu shilingi milioni 60 pia. Miradi hiyo inatarajiwa kunufaisha zaidi ya watu 4,000 pindi itakapokamilika.

‎Katika mpango wa uendeshaji wa huduma hizo, amesema kuwa watumiaji wa vyoo watalipia huduma hiyo kwa lengo la kugharamia matengenezo, uendeshaji wa mradi pamoja na kuboresha makazi ya wananchi na kuinua vipato vyao.

‎Amebainisha kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kuboresha afya na ustawi wa jamii, kuongeza kipato, na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja kupitia mazingira bora ya biashara na huduma.‎

‎Habitat for Humanity inafanya kazi katika nchi 70 duniani, huku makao makuu yake yakiwa nchini Marekani. Aidha, Massenza amesema kuwa mradi huo ni sehemu ya jitihada za taasisi hiyo katika kuboresha huduma za vyoo na usafi wa mazingira katika maeneo ya minada na jamii kwa ujumla.

‎Katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Habitat for Humanity Tanzania, John Massenza, aliambatana na viongozi wa serikali ya kijiji na mtaa pamoja na maafisa mazingira kutoka Wilaya ya Bahi.

‎Awali, mhandisi wa mradi alisema kuwa tanki la maji litakuwa na ujazo wa lita 3,000, kwa Kila tank litakalokuwepo kwenye miradi hio, huku akibainisha kuwa ujenzi wa majengo hayo ukitarajiwa kuchukua wiki 8 hadi 10, na kwamba mradi mzima unatarajiwa kukamilika ndani ya siku 90.


















Share:

Sunday, December 14, 2025

WAZIRI MKUU: WATANZANIA TUNZENI AKIBA YA CHAKULA

 


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania watunze akiba ya chakula walichonacho na waepuke matumizi yasiyofaa kutokana na hali ya kuchelewa kwa msimu wa mvua.

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo jioni (Jumapili, Desemba 14, 2025) wakati akizungumza na baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.

Amewaeleza viongozi hao kutoka mikoa ya Dodoma na Singida kwamba Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa utabiri wa mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli na mvua za msimu kwa kipindi cha Oktoba 2025 hadi Desemba 2025 na kipindi cha mwezi Novemba, 2025 hadi Aprili 2026 mtawalia.

“Kutokana na utabiri huo, baadhi ya mikoa nchini inatarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani hadi wastani na kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha,” amesema.

Amesema tathmini hiyo ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaonesha hali ya kuchelewa kwa mvua inatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Dodoma, Katavi, Kigoma, Singida, Tabora, Iringa, Mbeya, Mtwara, Njombe, Songwe, Rukwa, Ruvuma pamoja na Kusini mwa Mkoa wa Morogoro.

“Pamoja na kuwa hakuna tishio la uhaba wa chakula kutokana na hifadhi ya chakula iliyopo nchini, lakini ni vema, wananchi waendelee kuzingatia matumizi sahihi ya chakula. Tuna akiba ya chakula ya kutosha lakini ninawasihi wananchi waweke akiba na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima,” amesema.

Ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wakulima waandae mashamba kwa wakati na watumie pembejeo zinazoendana na upatikanaji wa mvua chache sambamba na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo ambao kwa sasa wanazunguka nchi nzima kukutana na wakulima na kutoa elimu.

Vilevile, Dkt. Mwigulu amewataka wafugaji wote waweke mipango mizuri ya matumizi na uhifadhi wa maji na vyakula vya mifugo ili kukabiliana na hali hiyo.

Waziri Mkuu amewasisitiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wahakikishe maafisa ugani wanawatembelea wakulima na kutoa ushauri ikiwemo matumizi sahihi ya mbegu kulingana na hali ya hewa badala ya kukaa ofisini muda wote.

“Vilevile, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri endeleeni kuhamasisha wakulima wajisajili kwenye daftari la mkulima na kuhakikisha wanapata namba za usajili,” amesisitiza

Amewataka viongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) zihakikishe kuwa shehena za pembejeo zinahudumiwa kwa wakati ili usambazaji ufanyike kwa ufanisi.

Share:

NAIBU WAZIRI MARYPRISCA:ELIMU YA MAENDELEO YA JAMII NI CHACHU YA AJIRA NA KUJITEGEMEA

 

Na Jackline Minja WMJJWM, Iringa

‎Vyuo vya maendeleo ya jamii vimetajwa kuwa ni mhimili muhimu wa mabadiliko ya fikra, uundaji wa ajira na ustawi wa wananchi, hasa katika ngazi ya msingi ambako changamoto za kiuchumi na kijamii zinapoanzia ambapo mwelekeo huo umetajwa kuwa suluhisho la kupunguza utegemezi, kuongeza uzalishaji na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika maendeleo yao wenyewe.

‎Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati akizungumza na wanachuo pamoja na watumishi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha kilichopo mkoani Iringa tarehe 13 Desemba 2025.

‎ 

‎Mhe. Maryprisca amesema mafanikio ya Chuo hicho katika kudahili wanafunzi 2,571 ndani ya kipindi cha miaka minne yanaonesha mchango wake mkubwa katika kuandaa rasilimali watu yenye tija kwa Taifa. 

‎“Vyuo vinapaswa kuandaa wahitimu wenye uwezo wa kujitegemea, kuajiri wengine na kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii zao, huu ni ushahidi kuwa elimu inayotolewa hapa inaendana na mahitaji ya nchi na inawaandaa wahitimu kuwa waajirika, wajiajiri na wawezeshaji wa maendeleo ya jamii,” amesema Mhe. Maryprisca

‎Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha Godfrey Mafungu amesema Chuo kinaendelea kutekeleza mafunzo yanayolenga kumwandaa mwanafunzi kuwa watatuzi wa changamoto za jamii kwa kuunganisha nadharia na vitendo ambapo kupitia programu za kitaaluma, tafiti na miradi ya uzalishaji mali, Chuo kimefanikiwa kuwajengea wanafunzi ujuzi unaowawezesha kuajirika, kujiajiri na kuchangia maendeleo ya jamii wanazotoka. 

‎Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi, rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho Abasi Kibwana Jumanne, ameishukuru Wizara na uongozi wa Chuo kwa kuweka mazingira yanayowawezesha wanafunzi kupata elimu inayozingatia ujuzi wa vitendo na mahitaji ya jamii 

‎“Ziara hii imeongeza ari na motisha kwa wanafunzi katika kujifunza na kuwahudumia wananchi kwa weledi pindi watakapohitimu maana tumejipanga kusoma kwa bidii, kuzingatia maadili na kutumia elimu tunayopata hapa kuwa chachu ya maendeleo katika jamii zetu” amesema rais wa Chuo.






Share:

Saturday, December 13, 2025

RC MALIMA AIPA KONGOLE WIZARA YA ARDHI UTUNZAJI KUMBUKUMBU ZA ARDHI

 

Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Bw. Adam Malima ameipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuweka kumbukumbu za ardhi vizuri jambo alilolieleza kuwa linasaidia katika utatuzi wa migogoro ya ardhi.

‘’Mhe Waziri kwa kweli nitoe pongezi kwa wizara yako kwa kuwa na kumbukumbu nzuri za wamiliki wa ardhi jambo hili limetusaidia kama mkoa wa morogoro kutatua migogoro ya ardhi pale inapojitokeza’’ amesema Bw. Malima

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi moja ya vipaumbele vyake ni katika mwaka wa fedha 2025/2026 ni kuongeza kasi ya upangaji, upimaji, umilikishaji na usajili wa ardhi mijini, vijijini na katika maeneo ya kimkakati.

Bw. Malima amesema hayo tarehe 12 Desemba 2025 ofisini kwake alipokutana na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo aliyekuwa mkoani humo kwa ajili ya kuhudhuria mahafali ya 44 ya Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO).

Amesema, migogoro ya ardhi katika mkoa wake wa Morogoro imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na juhudi kubwa za wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa ambapo imefanya kazi kubwa ya kufikia wananchi kupitia Kliniki ya Ardhi.

Kwa upande wake Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo alimueleza mkuu wa mkoa wa Morogoro kuwa, wizara yake kwa sasa inafanya juhudi kubwa kuhakikisha migogoro ya ardhi iliyopo inatatuliwa na hakuna migogoro mipya inayozalishwa kwenye maeneo mbalimbali nchini.

‘’Nikuhakikishe RC sisi ndani ya wizara tumejiwekea mikakati ya kuhakikisha migogoro iliyopo tunaimaliza lakini pia hakuna migogoro mipya inayozalishwa’’ amesema Mhe. Dkt Akwilapo.

Aidha, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amezihimiza taasisi za umma kuhakikisha zinalinda maeneo yao ili kuepuka uvamizi alioueleza kuwa ndiyo unaochangia kwa kikubwa migogoro ya ardhi katika maeneo ya umma.



Share:

Friday, December 12, 2025

SERIKALI YAJIDHATITI KUIMARISHA USTAWI WA JAMII.



 Na Jackline Minja MJJWM , Dodoma

Serikali ya Awamu ya Sita, inaendelea kuweka kipaumbele katika ajenda ya ustawi na mifumo ya ulinzi wa mtoto, kuendeleza huduma za malezi mbadala, usimamizi wa Makao ya Watoto nchini ili kuhakikisha yanatoa huduma kwa viwango vinavyotakiwa.


Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati wa ziara ya kutembelea Makao ya Watoto ya Taifa Kikombo Jijini Dodoma na kujionea huduma zinazotolewa katika Makao hayo.


Mhe. Maryprisca amesema Makao ya Taifa ya Kikombo ni mfano wa Taasisi ya Serikali inayotekeleza majukumu hayo kwa weledi, upendo na dhamira ya dhati.


“Nimetembelea miradi, miundombinu na kupokea taarifa ya mafanikio, changamoto na maeneo yanayohitaji kuimarishwa, nafurahishwa kuona jitihada kubwa zinazofanywa katika kutoa huduma ya Elimu, Afya, Lishe, ushauri nasaha pamoja na malezi kwa Watoto napenda kuwahakikishia kuwa Wizara itahakikisha Makao haya yanawezeshwa ipasavyo”. amesema Mhe. Maryprisca.


Aidha Mhe. Maryprisca ametoa rai kwa wadau wa maendeleo, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na jamii kuendelea kushirikiana na Wizara kwa kuwapa watoto fursa sawa za maendeleo kama ilivyo kwa watoto wengine wote wa Tanzania.


“Niwaombe Mashirika, wadau wa maendeleo tuendelee kuiunga mkono Serikali katika kuendeleza makazi ya watoto ili wawe na huduma nzuri na wasijione wanyonge na niwaambie kuwa ninyi ni watu muhimu, mnapendwa na Taifa linawahitaji, msipoteze matumaini, someni kwa bidii, zingatieni maadili, muwe na nidhamu na mtumie fursa mnazopata ili mkafikie ndoto zenu."

amesema Mhe Maryprisca


Katika hatua nyingine Mhe. Maryprisca ameupongeza Uongozi wa Makao ya Taifa ya Kikombo kwa kazi wanayoifanya na kuwataka kuendeleza ushirikiano ili kuhakikisha kuwa kila mtoto analelewa katika mazingira salama, yenye upendo na yenye kumjenga.


Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amesema watumishi wa Makao hayo wana weledi na uwezo mkubwa wa kutambua uwezo wa watoto licha ya changamoto wanazokuja nazo watoto katika makazi hayo.


“Hawa watumishi unaowona hapa wanauwezo wa kukaa nao, kuongea nao kwa mbinu tofauti ndio maana nasema hawa sio watu wakawaida hata mimi wakiniangalia wanasema hapo hauko sawa, lakini ni miongoni mwa watu walioaminiwa na Serikali ambao watatusaidia kukiendeleza Makao haya”. amesema Wakili Mpanju.


Awali akisoma taarifa ya huduma zinazotolewa katika makao ya Taifa ya watoto kikombo Afisa Ustawi wa Jamii Anord Fyataga amesema hadi sasa kituo kimepata mafanikio mengi ikiwemo kuimarika kwa huduma za ushauri na unasihi ambapo kila mtoto anapata ushauri wa moja kwa moja au wa makundi ,kuunganisha watoto 20 na familia zao, kuboreshwa kwa huduma za elimu ndani na nje ya makao ambapo wastani wa ufaulu wa watoto kwa shule za msingi na sekondari umeongezeka kwa asilimia mbili (2%) pamoja na kuwajengea ujuzi watoto 40 katika ujifunzaji wa stadi mbalimbali za maisha makaoni kama ushonaji wa nguo kwa kutumia cherehani.





Share:
Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com