Na Munir Shemweta, WANMM
Serengeti
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mhe. Angeline Mabula ameagiza zoezi la kupima upya
mipaka ya vijiji vya Kono na Ketembere vilivyopo kata ya Nata na Rigicha
wilaya ya Serengeti mkoa wa Mara kuanza mara moja na kufikia Desemba 2018 ramani
ya mipaka ya vijiji hivyo iwe imetoka.
Agizo la mhe. Mabula
linafuatia mgogoro wa muda mrefu uliokuwepo baina ya mipaka ya vijiji hivyo
jambo linalosababisha shughuli za maendeleo ikiwemo mpango wa matumizi bora ya
ardhi kushindwa kufanyika.
Akiwa katika ziara yake ya
kutatua mgogoro huo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
alisema mgogoro wa mpaka baina ya vijiji hivyo ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na
wataalamu kutoka Wizara ya ardhi kushindwa kufuata taratibu za kupima mipaka kwa
kuwashirikisha wananchi wa pande zote mbili.
"Makosa yaliyofanywa na
ofisi hayawezi kuleta ugomvi katika vijiji hivyo na ramani ya eneo hili
itarekebishwa kulingana na dira na wizara itaangalia namna ya kushughulika na
waliokwepesha mipaka ili kujua walikuwa na maana gani" alisema Mabula.
Kwa mujibu wa mhe. Mabula
lengo la kupima mipaka ni kuwezesha kuwepo mpango wa matumizi bora ya ardhi
ambapo kupitia mpango huo wananchi wataweza kupatiwa hati miliki ikiwemo hati
za kimila kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi na kusisitiza kuwa ardhi ndiyo
mtaji pekee kwa wananchi wa vijiji hivyo.
Awali Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwapa nafasi wananchi wa vijiji vya pande
zote mbili kueleza jinsi wanavyoifahamu mipaka ya vijiji vya Kono na Ketembere
ambapo wengi waliutambua mto Masara kama mpaka wa vijiji hivyo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kono
Michael Oyatason alisema, vijiji hivyo awali havikuwa na mgogoro wowote ila
tatizo lilianza mara baada ya uwekaji alama za mipaka ambao haukushirikisha
pande zote mbili kinyume kabisa na utaratibu wa kuainisha mipaka.
Mpima Ardhi Kanda ya Simiyu
Godwin Saiguran alimuahidi Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi kuwa zoezi la uanishaji mipaka ya vijiji vya Kono na Ketembere kwa
kushirikisha wananchi wa pande zote mbili litakamilika ndani ya siku nne na
kufikia tarehe 25 Oktoba 2018 zoezi litakuwa limekamilika.
Katika hatua nyingine Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi mhe. Angeline Mabula
ametatua mgogoro mkubwa baina ya vijiji vya Kazi na Rwamchanga vilivyopo katika
kata ya Manchira wilaya ya Serengeti mkoa wa Mara.
Mgogoro katika eneo hilo
unachangiwa na msuguani wa wananchi wanaotaka kuwa na vijiji viwili kama
ilivyoainishwa katika mipaka ya kiutawala ama kuwa na kijiji kimoja ambapo awali
kabla ya kuzungumza na wananchi wa vijiji hivyo mhe Mabula alizungumza na
wajumbe wa serikali ya vijiji ambapo alipowahoji viongozi wanaotaka kuwepo
kijiji kimoja ama viwili ni wajumbe wawili kati ya nane waliokuwa wakihitaji
kijiji kimoja.
Ilielezwa katika kikao baina ya
mhe. Mabula na wananchi wa vijiji vya Kazi na Rwamchanga kuwa,
mgogoro katika kijiji hicho unachangiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya viongozi
waliokuwa wakiwashawishi wananchi kutokubaliana na mipaka ya kiutawala iliyokuwepo
kwa sababau walizokuwa wakizijua wenyewe.
Kwa mujibu wa Mpimaji wa Ardhi
Kanda ya Simiyu Godwin Saiguran, tatizo kubwa katika eneo hilo ni uhakiki wa
mipaka ambayo awali ilikuwa haikuwekwa sawa na tayari sasa timu ya
kubainisha mipaka hiyo iko tayari kuanza kazi na kwa sasa timu hiyo iko
Wilaya ya Rorya mkoà wa Mara na inatarajia kuwasili eneo la vijiji hivyo muda
wowote.
-------------MWISHO-------------
0 comments:
Post a Comment