Naibu
Waziri Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack A. Kamwelwe na Mkuu wa Mkoa
wa Singida wakisoma kwa umakini taarifa ya Sekta ya maji Mkoa wa Singida wakati
wa kikao na wakuu wa idara mbalimbali.
Naibu
Waziri Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack A. Kamwelwe akisisitiza
jambo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ughandi A halmashauri ya
Wilaya ya Singida alipotembelea eneo la mradi wa maji kijijini hapo.
Naibu
Waziri Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack A. Kamwelwe akisikiliza
taarifa ya mradi wa maji wa Ughandi kutoka kwa Mhandisi wa Maji wa Halmashauri
ya Wilaya ya Singida Edward Kisalu.
Naibu Waziri Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack A.
Kamwelwe amezitaka halmashauri za Mkoa wa Singida kuongeza ujenzi wa
mabwawa, utakaosaidia kilimo cha umwagiliaji ili kuzalisha chakula cha
kutosha na kwa ajili ya makao makuu ya nchi, Dodoma.
Mhandisi Kamwelwe ametoa maelekezo hayo wakati wa mkutano
uliojumuisha wakuu wa idara zote pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Singida ili
kujadili hali ya Sekta ya Maji kabla ya hajaendelea na ziara yake katika
halmashauri za Mkoani hapa.
Amesema ardhi ya Singida pamoja na kiwango cha mvua cha milimita 500
mpaka 800 kwa mwaka vinatosha kuzalisha chakula kwa ajili ya matumizi ya
mkoa lakini ujenzi wa mabwawa utaongeza uzalishaji wa chakula hasa kwa
lengo la kulisha mkoa wa Dodoma.
“Mkuu wa Mkoa wa Singida una malengo makubwa na mazuri kwa mkoa huu,
mpango wako wa kuifanya Singida iilishe Dodoma ni mzuri na utafanikiwa
hasa mkiongeza bidii katika uzalishaji na kuweka kipaumbele katika
kilimo cha umwagiliaji”, amesema Mhandisi Kamwelwe.
Ameongeza kuwa Singida inapata mvua za wastani lakini imekuwa
ikizalisha kwa wingi mazao ambayo yamekuwa yakitumika katika mikoa yote
nchini kwa mfano alizeti, viazi vitamu, vitunguu na asali ambapo mazao
hayo yamekuwa yakipendwa kutokana na ubora wake.
Mhandisi Kamwelwe ameongeza kuwa hali ya upatikanaji wa maji kwa Mkoa
wa Singida bado inatakiwa kuboreshwa zaidi kutokana na kuwa kila mwaka
serikali imekuwa ikitenga fedha nyingi lakini asilimia ya upatikanaji wa
maji haiongezeki kwa kasi inayotakiwa.
Aidha amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Singida kusimamia matumizi ya fedha
za serikali zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maji ili ziweze kufanya
kazi iliyokusudiwa na kwa ubora mkubwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amesema
kuwa Singida sio kame kwakuwa hakuna mazao yanayoweza kumea katika ukame
isipokuwa Singida imejikita katika mazao yanayotumia maji kwa ufanisi.
Dkt Nchimbi amesema Singida inazalisha mazao ya mahindi, alizeti,
vitunguu, viazi vitamu na mazao mengine kwa wingi kutokanana na kuwa
mvua zinazonyesha zinatosheleza kustawisha mazao hayo.
Ameongeza kwa kuwataka wakuu wa idara zote kusimamia matumizi bora ya
fedha za serikali zinazotolewa kwa ajili ya maji kwakuwa suala la maji
ni la kila mmoja na sio kuwategemea watumishi wa idara hiyo pekee katika
kusimamia fedha na miundominu ya maji.
Dkt Nchimbi amesema Mkoa unahamasisha uchimbaji wa mabwawa kwa
halmashauri, taasisi na hata makundi mengine kwakuwa mabwawa hayo
yatasaidia kuinua kilimo cha umwagiliaji Mkoani Singida pamoja na kukuza
uchumi.
Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Singida Buhacha Kichinda amesema
hali ya upatikanaji wa maji kwa Mjini ni asilimia 50.6 huku vijijini
ikiwa ni asilimia 44 na kuongeza kuwa wastani huo ni mdogo kwakuwa
unarudisha nyuma jitihada za kuinua uchumi.
Kichinda amesema Mkoa umejipanga kushirikisha wadau zaidi ili
kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi ya maji ya visima virefu pamoja na
ujenzi wa mabwawa pamoja na kusimamia fedha zote za serikali
zinazotolewa kwa ajili ya sekta ya maji zinatumika ipasavyo.
Amesema ili kuhakikisha mvua zinaendelea kunyesha vizuri pamoja na
kutunza vyanzo vya maji, mkoa umeweka mkakati wa “ Achia shoka Kamata
Mzinga” ili kuwahamasisha wachoma mikaa waache kukata miti bali wajikite
katika kutundika mizinga itakayotunza mazingira.
0 comments:
Post a Comment