Thursday, September 28, 2017

WATUMISHI WA UMMA SINGIDA WATAKIWA KULIMA KOROSHO

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akisisitiza jambo wakati akikagua shamba la korosho la mkulima Juma Patrick wa Kijiji cha Sanjaranda halmashauri ya Wilaya ya Itigi.
 Displaying 2.JPG
Mkulima Juma Patrick wa Kijiji cha Sanjaranda halmashauri ya Wilaya ya Itigi akimuonyesha Mkuu wa Mkoa wa Singida mikorosho iliyostawi katika shamba lake.
 Displaying 3.JPG
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Miraji Jumanne Mtaturu wakiwa katika shamba la korosho la mkulima Juma Patrick wa Kijiji cha Sanjaranda halmashauri ya Wilaya ya Itigi.
 
Mkuu wa Mkoa wa Singida amewataka watumishi wa umma wote mkoani hapa kulima ekari moja ya korosho ili kutunza mazingira, kujiongezea kipato pamoja na kuonyesha mfano kwa wananchi wengine ili waweze kulima zao hilo kwa ufanisi.

Dkt Rehema Nchimbi ametoa agizo hilo mapema wiki hii mara baada ya kutembelea na kukagua shamba la mkulima wa zao hilo Juma Patrick katika kijiji cha Sanjaranda halmashauri ya wilaya ya Itigi.

Dkt Nchimbi amesema kuongoza ni kuonyesha njia hivyo watumishi wa umma wanatakiwa kuonyesha njia kwa kulima vizuri hasa katika mazao ya biashara yanayopewa kipaumbele kitaifa ambapo kwa mkoa wa Singida ni korosho, pamba na tumbaku.

“Watumishi hamuwezi kuwaambia wakulima walime korosho au pamba wakati wewe haujalima wala haufahamu changamoto na faida za kilimo hicho, naagiza kila mtumishi alime ekari moja ya korosho ili muwe mabalozi wazuri wa zao hilo mkoani hapa”, amesisitiza Dkt Nchimbi.

Aidha Dkt Nchimbi ametoa wito kwa wananchi wote kuchangamkia fursa ya kilimo cha korosho kwakuwa ndio mkombozi wa kutunza mazingira kwa mkoa huu pamoja na kuinua pato lao.

Amesema pembejeo na miche ya zao hilo inatolewa bure hivyo mwananchi hataingia gharama nyingine zaidi ya kuandaa shamba lake ambalo atavuna mara baada ya miaka mitatu tangu kupanda na kuendelea kuvuna kwa zaidi ya miaka 50.

“Wananchi korosho ni zao zuri sana, serikali ya awamu ya tano inatoa mbegu na pembejeo bure, nyie andaeni mashamba yenu tu lakini pia ukianza kuvuna korosho yako hiyo baada ya miaka mitatu utaendelea kuvuna kwa zaidi ya miaka hamsini, hii ni faida kubwa sana.

Dkt Nchimbi amefafanua kuwa Mkoa wa Singida umejipanga kuifanya korosho kuwa zao la kudumu la biashara mkoani hapa na kuwa mzalishaji mkubwa nchini wa korosho.

Kwa upande wake mkulima Juma Patrick wa kijiji cha Sanjaranda halmashauri ya wilaya ya Itigi amesema anamiliki ekari 11 za korosho ambapo kwa msimu wa mwaka  2015/2016 alivuna kilo 410 na msimu wa mwaka 2016/2017 alivuna kilo 826.

Patrick amesema mavuno yamekuwa ni kidogo kutokana na kutopata elimu ya kilimo hicho huku akiwa hafahamu namna ya kupata soko la korosho yake licha ya kuwa ardhi na mazingira ya Singida yanastawisha korosho vizuri.

Aidha amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kukagua shamba lake na kwa agizo lake la kuwataka watendaji wa halmashauri kuwatembelea wakulima ili wawape pembejeo na elimu ya kilimo bora cha korosho.

Patrick ametoa wito kwa wananchi wote hasa vijana kuchangamkia kilimo cha korosho kwa kuwa ni zao ambalo linastawi vizuri, linatunza mazingira na kukuza uchumi pamoja na kutohitaji uangalizi mkubwa hivyo kutoa nafasi ya kuendelea na shughuli nyingine huku ukiwa umepanda korosho.

No comments:

Post a Comment