Mnufaika wa TASAF III kutoka kijiji cha Migato wilaya ya Itilima akichota maji katika moja ya visima vilivyochimbwa na TASAF kupitia programu ya kazi za ajira za muda katika kijiji hicho.
Mmoja
wa wanufaika wa TASAF III katika Kijiji cha Migato akipokea fedha katika zoezi
la uhawilishaji lililofanyika kijijini hapo
Baadhi ya wanufaika wa TASAF III wa Kijiji cha
Migato wakiimba wimbo maalum wa kuwakaribisha wataalam kutoka TASAF Makao
Makuu, Benki ya Dunia na wadau wengine wa maendeleo (wadau washiriki wa mradi)
ambao ni UNDP, UNFPA, ILO na Umoja wa Nchi za Ulaya(EU) waliofika kufanya
tathmini ya utekelezaji wa mradi wa TASAF III Wilayani Itilima.
Na Stella Kalinga, Simiyu
Wanufaika
wa Mradi wa Mpango wa Kunusuru kaya maskini TASAF III hususani wanaopewa ruzuku
ya utimizaji wa masharti ya elimu na afya wamehimizwa kuwapeleka watoto kliniki
na kuhakikisha watoto wao wanahudhuria shuleni.
Wito huo
umetolewa na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani kutoka TASAF Makao Makuu, Ndg.
Christopher Sanga katika kijiji cha Migato wilayani Itilima wakati wa ziara ya
tathmini ya utekelezaji mradi wa TASAF wilayani humo.
Sanga amesema Serikali ina mpango mzuri kwa wananchi
wa kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapelekwa shule na pia
watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano wanapelekwa kiliniki na kupata huduma za afya zinazotakiwa, hivyo akawaasa
kutorudisha nyuma juhudi za Serikali.
Aidha, amesema lengo kuu la Serikali ni kuhakikisha
nguvu kazi inajengwa kwa kutoa elimu na kuangalia afya za watoto wakiwa bado
wadogo ili watakapobainika kuwa na matatizo ya kiafya wapatiwe matibabu mapema kwa
lengo la kuimarisha afya na kutoathiri
ukuaji wao.
Ameongeza kuwa utafiti uliofanyika kuhusu
utekelezaji wa awamu zilizotangulia za Mpango wa TASAF ulionesha kuwa, kumekuwa
na miundombinu mingi ya elimu na afya lakini kaya maskini zimekuwa hazipeleki
watoto katika huduma hizo, hivyo Serikali ikatoa ruzuku ya elimu na afya na
kuwawekea masharti wazazi ili kuhakikisha wanawapeleka watoto katika huduma
hizo.
Amesisitiza kuwa Mpango wa TASAF unafuatilia
mahudhurio ya watoto wanaopata ruzuku ya utimizaji wa masharti ya elimu na ili
ruzuku hiyo iendelee kutolewa kwa wanafunzi hao ni lazima mahudhurio yao yasiwe
chini ya asilimia 80 kwa muhula, wasipohudhuria kuna adhabu inayotolewa ikiwa
ni pamoja na kupunguzwa kwa ruzuku hiyo.
“ Miongoni mwa madhara ya watoto kutohudhuria masomo
katika muhula husika kwa kaya zinazonufaika na TASAF kwa kupata ruzuku ya elimu
ambayo inasaidia kaya hizo, ni kupungua kwa ruzuku na inapopungua uwezo wa kaya
katika kujikimu na kufanya mabadiliko ya kiuchumi unaathirika” amesema Sanga.
Kwa upande wake Bibi. Ngolo Buzenganwa mkazi wa
kijiji cha Migato ambaye ni mnufaika wa Mpango wa TASAF III amewataka wazazi
wenzake kufuatilia maendeleo ya watoto wao na kukagua daftari zao mara kwa mara
ili ruzuku inayotolewa isipunguzwe na iwasaidie kuwawezesha kupata mahitaji
muhimu ya shule kwa ajili ya watoto wao.
Katika hatua nyingine wanufaika wa Mpango wa TASAF
III wameshukuru mpango huo kwa kutatua changamoto ya upungufu wa maji kwa
kuwachimbia visima vya maji kupitia programu ya kazi za ajira za muda na kuomba
kuongezewa idadi ya visima hivyo katika awamu nyingine ya utekelezaji wa mradi.
“Tunaishukuru sana TASAF kutuletea maji kwa visima
hivi, tulikuwa tunatembea muda mrefu sana zaidi ya saa moja kufuata maji,
lakini sasa hivi maji yapo karibu tena ni maji safi na salama” amesema Maila
Limbu mkazi wa Migato.
Naye Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Itilima,Goodluck Masige amesema Serikali Wilayani humo imeweka mpango wa
kuviwekea pampu visima vyote 194 vilivyochimbwa kupitia mradi wa TASAF ili
kuwarahisishia wananchi kupata maji kwa urahisi zaidi kuliko teknojia
inayotuika sasa ya kuvuta kwa kamba.
Wilaya Itilima ni moja ya Wilaya tano zinazofanyiwa
tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru kaya Maskini (TASAF III) katika
awamu hii, tathmini inayofanywa na wataalam kutoka TASAF Makao Makuu, Benki ya
Dunia na wadau wengine wa maendeleo (wadau washiriki wa mradi) ambao ni UNDP,
UNFPA, ILO pamoja na Umoja wa Nchi za Ulaya(EU).
0 comments:
Post a Comment