Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Mhe. Angellah Kairuki akiwasikiliza wataalamu wa masuala ya uwekezaji wa Ofisi ya waziri Mkuu wakati wa kikao na wawekezaji toka nchini Uturuki katika Kampuni ya MNG Group of Companies (hawapo pichani), wakati walipofanya kikao ofisini kwake juu ya fursa na miradi ya uwekezaji nchini tarehe 5 Januari, 2019, jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Uwekezaji), Angellah Kairuki akimkabidhi Kitabu chenye Fursa na Miradi
yenye Uhitaji Mitaji ya Uwekezaji nchini , Mwekezaji toka nchini Uturuki ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya MNG Group of Companies mara baada
ya kufanya kikao juu ya fursa na miradi ya uwekezaji nchini tarehe 5 Januari,
2019, jijini Dodoma.
Na. OWM, DODOMA
Kampuni ya MNG Group of Companies ya nchini Uturuki
imeonesha nia ya kufanya uwekezaji mkubwa nchini katika sekta mbalimbali;
zikiwemo sekta za Uchukuzi, Utalii, Nishati na Usafiri wa Anga.
Uwekezaji huo umebainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya
MNG Group of Companies, Mehmet Gunal, wakati alipokutana na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Mhe. Angellah Kairuki (Mb), jijini
Dodoma, tarehe 5 Januari 2019.
Waziri Kairuki amebainisha kuwa nia ya serikali ya
awamu ya tano ni kuhakikisha uwekezaji wenye tija nchini, na kwa kutumia mfumo
wa sera ya Ushirikiano baina ya sekta Binafsi na Umma inahakikisha
inavutia wawekezaji zaidi nchini.
“Tunazo fursa na miradi inayohitaji mitaji ya
uwekezaji hapa nchini, jukumu letu ni kuhakikisha wawekezaji mnapata mazingira
wezeshi katika fursa na miradi mnayotaka kuwekeza ili nchi iweze kupata tija
kutokana uwekezaji huo” Amesisitiza Mhe. Kairuki.
Akiongea katika kikao hicho mwenyekiti wa Bodi ya
Kampuni ya MNG Group of Companies, Mehmet Gunal, amefafanua kuwa , Kampuni hiyo
iko tayari kuwekeza nchini katika Sekta mbalimbali, kwa kuwa wamevutiwa na
mazingira ya uwekezaji ya hapa nchini.
Aidha, Gunal alifafanua kuwa wamejipanga kutumia
fursa na miradi yenye kuhitaji uwekezaji nchini ili kuweza kufanya
uwekezaji mkubwa , pia alisema kampuni yake ipo tayari kuwekeza hata kwa mfumo
wa sera ya ushirikiano baina ya Sekta ya Binafsi na Umma au kuwekeza wao
wenyewe.
Kampuni ya MNG Group of Companies inao uzoefu
katika masuala ya uwekezaji kwa miaka 42 katika mabara matatu Duniani,
ikiwa imejikita katika uwekezaji kwenye sekta sita na tayari hadi
hivi sasa imetekeleza miradi zaidi ya mia mbili katika mabara hayo.
Baadhi ya Miradi ambayo imetekelezwa na Kampuni
hiyo ni pamoja na , Bwawa la kufua Umeme la Chief Dam la nchini Algeria,
Ujenzi wa uwanja wa Ndege wa Kimataifa KOTOKA (terminal III),
wa nchini Ghana, Ujenzi wa makao makuu ya na Benki ya Halk nchini
Uturuki.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Isack Kamwelwe, Wataalamu wa masuala ya
Uwekezaji na maendeleo ya Sekta Binafsi wa Ofisi ya Waziri Mkuu,
pamoja na wataalam kutoka Kituo cha Uwekezaji nchini.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment