Magufuli aungwa mkono Chadema
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetoa msimamo wake juu ya sakata la mchanga wa dhahabu uliokuwa ukisafirishwa kwenda nje ya nchi, na kusema hakioni ulazima wa kufanya hivyo, kwani inawezekana kujenga nchini mtambo wa kuchenjua makinikia ya mchanga huo.
Msimamo huo unaonekana kuunga mkono hoja ya Rais John Magufuli, aliyezuia usafirishaji huo, huku akiunda kamati iliyotoa ripoti yake hivi karibuni na kuibua `madudu’ katika sakata zima la usafirishaji wa mchanga huo.
Mara baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa watendaji wote wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA) na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwa kile kilichodaiwa kushindwa kujenga kinu cha kuchenjulia makinikia tangu mwaka 2010, licha ya Sera ya Madini ya mwaka 2009 kuagiza.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho mjini hapa jana, Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema suala la kujenga mtambo wa kuchenjua makinikia ya mchanga wenye madini ni muhimu kwa sasa na kwamba hilo linawezekana.
Aidha, alisema Chadema haiungi mkono kupotea kwa rasilimali za Watanzania, hivyo kutaka waliohusika kusaini na kuingia mikataba iliyochangia taifa kuibiwa rasilimali zake `mchana kweupe’, wawajibishwe, badala ya kuishia kuwavua madaraka watu wachache.
Aliongeza kuwa utafiti uliofanywa na ripoti yake kuwasilishwa katikati ya wiki na Kamati ya Profesa Abdulkarim Mruma si wa kwanza, kwani mambo yaliyoibuliwa yaliwahi kuibuliwa pia na Kamati ya Jaji Mark Bomani na pia mashirika ya nje, yote yakisisitiza kuwa mikataba ya madini nchini haiifaidishi nchi.
Alisema hata wabunge wa kambi ya upinzani, kwa muda wamekuwa wakilalamikia mikataba iliyoingiwa baina ya Serikali na wawekezaji katika madini kuwa haikuwa na maslahi wala faida kwa watanzania.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema chama chake kinaamini tatizo halipo kwa wawekezaji katika kusafirisha mchanga, bali ni mikataba iliyoingiwa, hivyo ingekuwa vema kabla kiongozi wa nchi hajazuia makontena, mikataba yake ingeletwa bungeni hata kwa hati ya dharura ikabadilishwa, kama ilivyofanyika wakati wa kuisaini, ambapo kwa siku moja mikataba miwili ilisainiwa.
Alisema mikataba hiyo ndiyo inayoruhusu mwekezaji atozwe dola 200,000 (Sh milioni 420) kwenye mradi wa dhahabu, badala ya kutozwa kwa kutumia asilimia 0.14 ya mapato yatokanayo na madini yanayochimbwa na Chadema inaona suluhisho ni kuifanyia marekebisho.
0 comments:
Post a Comment