Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji,
Mhandisi Anthony Sanga (wa pili kushoto) akikagua moja ya tenki la maji
la mradi wa Same-Mwanga linalojengwa na Kampuni ya Badr East Africa
Enterprises.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji,
Mhandisi Anthony Sanga (wa pili kushoto) akitembelea kituo cha tiba ya
maji cha mradi wa Same-Mwanga kinachojengwa na Kampuni ya M.A Kharafi
& Sons.
…………………
Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa maji wa Same-Mwanga wametakiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wake ili ukamilike kwa wakati.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji,
Mhandisi Anthony Sanga ametoa maelekezo hayo Septemba 28, 2019 wakati wa
ziara yake iliyolenga kukagua hatua ya ujenzi iliyofikiwa na
Wakandarasi wanaotekeleza mradi huo ambao ni kampuni ya M.A Kharafi
& Sons na kampuni ya Badr East Africa Enterprises.
Mara baada ya kujionea shughuli
zilizokuwa zikiendelea na kupokea taarifa ya mradi kutoka kwa
wakandarasi hao, Mhandisi Sanga alieleza kutoridhishwa na kasi ya
utekelezwaji wake na aliwasisitiza kuhakikisha kuwa mradi unakamilika
kwa wakati.
Mhandisi Sanga aliwataka
Wakandarasi kuwa wepesi kwenye kufanya mawasiliano na Wizara kila
wanapokutana na changamoto yoyote ambayo ipo nje ya uwezo wao ili
ufumbuzi upatikane haraka bila kuchelewesha shughuli za ujenzi wa mradi.
“Sijaridhishwa na kasi yenu ya
ujenzi wa mradi. Kama kuna changamoto mnakutana nazo zilizo nje ya uwezo
wenu mhakikishe mnawasiliana na Wizara mapema iwezekanavyo ili tupate
ufumbuzi,” alisema Mhandisi Sanga.
Aliongeza kwamba Serikali
inachohitaji ni kuona matokeo na haipo tayari kumvumilia mkandarasi
ambaye anachelewesha mradi bila ya kuwa na sababu za msingi.
“Wanachohitaji wananchi ni maji,
Serikali haitomvumilia Mkandarasi ambaye atashindwa kwenda na kasi
inayokubalika,” alibainisha Mhandisi Sanga.
Mhandisi Sanga vilevile
aliwakumbusha wakandarasi hao kuhakikisha manunuzi ya vifaa
vinavyohitajika kwenye ujenzi wa mradi huo yanafanyika hapa nchini
badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi hasa ikizingatiwa kwamba vingi
vinapatikana hapa hapa Nchini.
Wakandarasi hao kwa nyakati
tofauti walimuahidi Naibu Katibu Mkuu Sanga kuongeza kasi ya utekelezaji
wa mradi sambamba na kuzingatia maelekezo aliyoyatoa.
Mradi wa Same-Mwanga ni miongoni
mwa miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali kwa lengo la kuondoa kero
ya maji kwa wakazi wa Miji ya Same na Mwanga, Mkoani Kilimanjaro na
baadaye Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga.
Ziara hiyo ya Naibu Katibu Mkuu
Sanga kwenye mradi huo ni ya kwanza tangu ameteuliwa na kuapishwa
kushika wadhifa huo Septemba 22, 2019
0 comments:
Post a Comment