Wabunge wapinga kodi vifaa vya ujenzi
WABUNGE wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika vifaa vya ujenzi, lengo likiwa kuwawezesha wananchi wakiwemo wa kipato cha kawaida, kuweza kumiliki nyumba bora.
Wamesema kwa kuanzia, wanaweza kuliondolea kodi hizo Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambalo nyumba zake, licha ya kuitwa za bei nafuu, zinauzwa kwa bei kubwa, jambo linaloibua malalamiko kutoka kwa wananchi.
Kilio cha wabunge hao kuhusu gharama za nyumba za NHC ni cha muda mrefu, kwani hata kwenye bajeti ya wizara hiyo mwaka jana, wengi wa wabunge hao walilalamikia suala hilo la VAT kuwa ndio chanzo cha nyumba hizo kuwa na gharama kubwa, ambayo wananchi wa kawaida hawawezi kuimudu.
Akichangia katika mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ya Mwaka wa fedha 2017/18 bungeni juzi, Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, Abdallah Bulembo (CCM), alisema gharama za nyumba hizo kamwe wananchi wa kipato cha chini hawawezi kuzimudu.
“NHC sitaki kuharibu mipango yenu, lakini nyumba zenu ni za bei ya juu, sasa sisi wanyonge tuna nafasi gani kwenye nyumba hizo. Mbona Rais John Magufuli ameweza kujenga kupitia Wakala wa Majengo (TBA), kule Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa bei nafuu? alihoji.
Alisema Serikali ni lazima itambue kuwa bado Watanzania hasa wanaoishi mijini, wana shida ya nyumba na ni wachache wenye uwezo wa kupanga na kwamba kila mtu ana haki ya kukaa kwenye nyumba za Serikali.
Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Makilagi (CCM), alipongeza miradi ya nyumba inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini na kuelezea kuwa pamoja na hatua hiyo, bado gharama za nyumba hizo ni kubwa.
“Nyumba za NHC ni mradi mzuri, lakini tatizo ni gharama. Kuna nyumba pamoja na kuisha siku nyingi mpaka sasa hivi hazina watu kwa sababu ya gharama. Mheshimiwa Waziri waangalieni watu wa chini kwenye nyumba hizi,” alisisitiza.
Mbunge wa Chambani, Yussuf Salim Hussein (CUF), aliomba Serikali iangalie kodi ya VAT inayotozwa kwenye vufaa vya ujenzi vya nyumba hizo za NHC na kuindoa ili gharama za nyumba hizo ipungue na mwananchi wa kawaida aweze kumudu kuzinunua.
Wakati akijibu hoja za wabunge hao wakati wa kupitisha bajeti hiyo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema kilio hicho cha gharama za nyumba za NHC Serikali imekipokea na itakifanyia kazi.
Hata hivyo, alifafanua kuwa tayari Rais Magufuli alishatoa maelekezo kuhusu nyumba hizo, ambapo katika nyumba za gharama nafuu kupitia mpango mpya, wananchi wanaotaka kununua nyumba wanatakiwa kuanza kulipia asilimia 20 ya gharama na baadaye kulipa kodi hadi pale watakapomaliza deni na kukabidhiwa nyumba zao.
Alisema mpango huo unalenga kuwawezesha wasio na uwezo wa kulipia gharama yote ya nyumba, kulipa kidogo, kwani hata mwenye nyumba hiyo akifariki ndugu au watoto wake, wanaweza kulipa kodi hiyo na baadae deni likiisha watakabidhiwa nyumba husika.
Lukuvi alisema hadi sasa shirika hilo limekamilisha ujenzi wa miradi 29 kati ya miradi 54 ya nyumba iliyokuwa inatekelezwa zikiwemo nyumba za gharama nafuu, kati na juu, majengo ya biashara na matumizi mchanganyiko.
Alisema kwa sasa NHC ina nyumba 1,686 na jumla ya miradi 14 yenye nyumba za gharama nafuu 492, miradi 10 ni ya nyumba za gharama ya kati na juu yenye nyumba 881, miradi minne ya nyumba za biashara 229 na jengo moja la matumizi mchanganyiko lenye nyumba 84.
“Pia miradi 25 yenye jumla ya nyumba 4,126 inaendelea kujengwa kati ya miradi hiyo, miradi 14 ni nyumba za gharama nafuu yenye jumla ya nyumba 1,002, miradi mitatu ni ya nyumba za gharama ya kati na juu yenye nyumba 760, miradi mitano ni ya nyumba za biashara na ina nyumba 203 na miradi minne ya nyumba za matumizi mchanganyiko yenye nyumba 2,161,”alisema. Alisema hadi Mei mwaka huu, shirika hilo lilikuwa limekusanya jumla ya Sh bilioni 39 kutokana na mauzo ya nyumba.
0 comments:
Post a Comment