WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameagiza kukamatwa na kuwekwa ndani viongozi wa kamati ya watumiaji maji
wa mradi wa maji wa Matunguru uliopo katika Kijiji cha Tungamalenga
wilayani Iringa kwa tuhuma za ubadhilifu wa sh. milioni saba.
Ametoa agizo hilo jana jioni
(Jumamosi, Septemba 28, 2019) baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa
wananchi wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji
cha Idodi wilayani Iringa.
Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa
Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela afuatilie suala hilo kwa kuwa kamati
nyingi za watumiaji maji zimekuwa na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha
zinazokusanywa kutoka kwa wananchi jambo ambalo si sahihi.
Alisema ifikapo saa 4.00
asubuhi ya leo watuhumiwa wote wanaohusika na ubadhilifu huo wawe
wameshakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola kwa ajili ya kwenda
kujibu tuhuma zinazowakabili.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu alisema kwamba Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya
kutoka Iringa hadi Ruaha yenye urefu wa kilomita 104 ili kuboresha
huduma za usafiri kwa wakazi wa maeneo hayo na kuinua uchumi.
Waziri Mkuu aliyasema hayo
baada ya kupokea malalamiko ya ubovu wa barabara hiyo kutoka kwa mbunge
wa jimbo la Ismani, William Lukuvu ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi.
Mbunge huyo alisema licha ya
Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo katika jimbo ikiwemo ya maji, afya na umeme, lakini
wanakabiliwa na tatizo la ubovu wa barabara ambapo aliomba Serikali
iwasaidie.
Baada ya Waziri Mkuu kusema
kuwa Serikali itahakikisha barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami
wananchi walifurahi na kuishukuru Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa
na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuwajali wananchi wake.
Awali, Waziri Mkuu alikagua na
kuzindua majengo matano ya kituo cha afya Idodi ambayo yamegharimu sh.
milioni 400. Pia Serikali iliongeza sh. milioni 300 kwa ajili ya ununuzi
wa vifaa tiba. Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na ujenzi wa mradi huo.
Kwa upande waobaadhi ya
wagonjwa waliolazwa katika wodi ya Mama na Mtoto ambao walikuwa
wajifungua kwa njia ya upasuaji waliishukuru Serikali kwa kuboresha na
kusogeza huduma za afya karibu na makazi ya wananchi.
Mmoja wa wagonjwa hao, Agusta
Nyagawa alisema awali walikuwa wanalazimika kwenda hadi Iringa mjini kwa
ajili ya kufuata huduma za afya lakini kwa sasa huduma hizo zikiwemo za
kujifungua pamoja na vipimo wanazipata kituoni hapo.
Naye, Chipe Ngugi alisema
anaishukuru Serikali kwa kuwa huduma za afya zimeboreshwa katika
hospitali yao ya kata, hivyo hawatalazimika tena kusafiri umbali mrefu
hadi Iringa kwa ajili ya kufuata huduma za afya zikiwemo za upasuaji.
Alisema yeye alijifungua kwa
njia ya upasuaji na anawashuwashukuru madaktari na wauguzi kituoni hapo
kwa huduma nzuri ambazo zimeokoa Maisha yake na mtoto. Aliiomba
Serikali iendelee kuboresha huduma kwa kuwa wapo mbali na mjini.
0 comments:
Post a Comment