Siku ya Mazingira Duniani kufanyika kitaifa Butiama
KATIKA kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, serikali imedhamiria kumuenzi mwasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kutokana na mchango wake mkubwa pamoja na misimamo yake katika kuhifadhi mazingira ya asili nchini.
Hata hivyo, imetoa siku tatu kuanzia Ijumaa ya wiki hii hadi Jumapili kwa Watanzania kuingia bure katika mbuga zote za wanyama nchini, lengo likiwa ni kuwaona wanyama na kutambua kuwa wako kama walivyo kutokana na kuwepo kwa mazingira. Kadhalika imeandaa mjadala wenye kutoa muongozo kuhusu mustakabali wa nchi kuhusu mazingira, wakishirikisha wataalamu mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini kwa ajili ya kueleza umuhimu wa kuhifadhi mazingira, kwa kuwa kwa sasa hali ni mbaya nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayotarajiwa kufanyika kitaifa kuanzia Juni Mosi hadi Juni 5 katika Kijiji cha Butiama mkoani Mara, alikozaliwa, kulilia na kuzikwa Mwalimu Nyerere.
Katika kilele cha maadhimisho hayo, Makamu wa Rais Samia Hassan Suluhu atakuwa mgeni rasmi, akiongoza kupanda miti katika shamba la Mwalimu Nyerere pamoja na kuendesha kongamano la kitaifa la mazingira likishirikisha pia viongozi wengine na wanafamilia ya Nyerere. Kaulimbiu katika maadhimisho hayo ni “Hifadhi mazingira, Muhimu kwa Tanzania ya Viwanda.”
Kuhusu maadhimisho hayo kufanyika Butiama, January alisema inatokana na mchango mkubwa wa Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake akiwa mwanamazingira wa kwanza, aliyesimama thabiti na kuwa na falsafa za kuhifadhi mazingira yanayoifanya Tanzania iwe kama ilivyo kwa sasa. Akifafanua zaidi kuhusu maadhimisho hayo, alisema Jumamosi wiki litafanyika kongamano kuhusu mazingira ambako mijadala minne inayohusu hali ya mazingira nchini, athari za uchumi kwa sekta ya mazingira nchini katika kilimo, uvuvi, ufugaji na utalii zitawasilishwa na majopo ya wataalamu mbalimbali.
Alieleza kuwa mjadala mwingine utahusu nafasi ya viongozi wa dini kutoa elimu kuhusu mazingira kwa kuwa wapo baadhi ya waumini wasiosikia pengine zaidi ya dini. Kadhalika alisema Butiama, shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwamo kupanda miti na kutangaza hatua za kuhifadhi na kuulinda msitu ambao Mwalimu Nyerere aliuhifadhi pamoja na kuendesha kongamano la viongozi kuhusu mchango wa Mwalimu Nyerere kwenye hifadhi ya mazingira, umuhimu wa mazingira na mustakabali wa nchi.
Kuhusu kutembelea mbuga za wanyama, alisema tayari wamezungumza na Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (Tanapa) ili kwamba Watanzania waingie katika mbuga hizo kwa siku tatu bure, lengo likiwa ni kuona uwepo wa wanyama na kujifunza kuwa mazingira yanahitaji kulindwa zaidi na zaidi.
0 comments:
Post a Comment