METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, April 25, 2017

TAARIFA YA UMOJA WA VIJANA WA CHAMA CHA KWA VYOMBO VYA HABARI



Ndugu Waandishi wa Habari.

Kwa heshima kubwa tumelazimika kuwaita hapa ili kuzumgumza nanyi masuala kadhaa muhimu yanayohusu maendeleo ya nchi yetu na masuala mengine kadhaa.

Tumekuwa tukipata faraja kubwa mno kuendelea kushirikiana nanyi bega kwa bega katika shughuli zetu mbalimbali za kuihabarisha, kuielimisha na kupatia taarifa sahihi jamii yetu kila inapobidi.

Ushirikiano huu kati yetu na vyombo vyenu vya habari katu haupaswi kupuuzwa na kubezwa badala yake unahitaji kuendelezwa, kuimarishwa na kudumishwa kizalendo .

*MIAKA 53 YA MUUNGANO WETU*

Ndugu Waandishi wa habari,

Wakati huu tunapokutana hapa, imetimia miaka 53 tokea mataifa mawili huru ya Tanganyika na Zanzibar yalipopitisha uamuzi wa kihistoria, hatimaye nchi mbili zikaungana na kuunda dola moja, Taifa jipya linaloitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaniaambalo halikuachwa na wakoloni waliotutawala.

Kitendo cha waasisi wa mataifa yetu mawili Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume na wenzao kuamua kuunganisha nchi zetu, kimelipa heshima Taifa letu, kumewaunganisha wananchi wetu, kimejenga misingi ya umoja wa kitaifa, upendo na mshikamano.

Muungano wetu kama nilivyosema umeleta tija na manufaa makubwa tokea kuundwa kwake April 26 mwaka 1964 Umeishangaza dunia kudumu kwake kwa sababu wakati wa harakati za kupigania uhuru viongozi kadhaa wa Afrika na vyama vya ukombozi walipitisha maazimio katika vikao vya umajumui na kuazimiwa nchi za kiafrika siku moja zikijitawala wenyewe zitaunda dola moja.

Azimio hilo kimsingi lilishindikana kufikiwa viongozi pekee wa kiafrika ambao walioonyesha kiu ya uzalendo na kutanguliza maslahi ya Afrika na watu wake ni Marehemu Mwalimu Nyerere toka upande wa iliyokuwa Tanganyika na mwenzake aliyekuwa Rais wa Zanzibar huru hayati Mzee Abeid Amani Karume .

Viongozi hawa hawakutazama kiu za madaraka na tunu za kupata vyeo, walichokitazama ni shauku ya kujiletea umoja wa wananchi wa Afrika na mataifa yao ikiwemo kusimamamia vyema na kutekeleza dhana ya maendeleo kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Zipo nchi kadhaa katika Afrika ambazo ziliunda miungano ila kwa bahati mbaya miungano hiyo ikaishia njiani. Mataifa ya Misri, Syria na Libya yaliunda Muungano ulioitwaArab Republic huku Mataifa ya Senegal na Gambia yakaunda Muungano uliojulikana Senegal Gambia .

Miungano hiyo miwili ilikwama pengine si kwa sababu ya viongozi wake kuwaza vyeo, huenda walishindwa kwa kutotazama mbele na kufikiria maslahi mapana ya wananchi, Afrika na umoja wake.

Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi, tutaendelea kuwaenzi, kuwaheshimu na kuwathamini waasisi wa Muungano wetu huku siku zote tukimuomba Mwenyezi Mungu awaweke viongozi hao mahali pema peponi.

Ndugu Waandishi wa habari.

Tanganyika na Zanzibar hazikufanya dhambi kuungana hatimaye kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yapo mataifa makubwa duniani tena yenye nguvu za kivita, kiuchumi na kimaendeleo, yameungana na sasa yanaendeleza umoja.

Kwa mfano Uingereza muungano wake umeundwa kutokana na ridhaa ya nchi nne zikiwemo, England, Scotchland, Wales na Norhern Island. Muungano huo umedumu kwa miaka mingi sasa na nchi zote hizo ziko chini ya utii wa kifalme.

Marekani wamekubali kuuuganisha nchi 52 na kuundwa dola moja iitwayoUnited State of America (USA). Maendeleo yao na nguvu zao kiuchumi, kiteknolojia na kiufundi, wamezipata kutokana na kuwa kwao na nguzo imara ya umoja. Mara zote ieleweke kuwa umoja ni nguvu na utengano huwa ni udhaifu.

Aidha katika aina au muundo na mfumo wa Muungano wowote lazima ziwepo changamoto, kujitokeza kwa kero mbalimbali na kuwa sehemu ya mchakato wa kuyafikia maendeleo kwa sababu maendeleo yasiokabiliana au kukumbwa na changamoto huwa si maendeleo halisi.

Miaka 53 kwa kweli ni mingi ndani ya Muungano wetu kuna kizazi kipya, damu mpya na watu wengi ambao wakati Muungano ukiundwa baadhi yetu hapa hatukuwepo, tumezaliwa sasa tunaishi katika dola iliyoasisiwa na wazazi wetu. Hili si jambo dogo ni la kujivunia na ni fahari kubwa kwetu kwa kizazi chetu na kijacho.

Hata hivyo tokea Muungano wetu uundwe viongozi wanane wamefanikiwa kushika madaraka ya uongozi wa dola na kuondoka kidemokrasia, Alianza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Mzee Benjamin Willium Mkapa, Dk Jakaya Kikwete na awamu ya tano inaongozwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli.

UVCCM inachukua nafasi hii kuwapongeza kwa dhati marais wetu wote wastaafu na kumsifu zaidi Rais aliyepo madarakani kwa kuongoza nchi kwa busara na hekima huku akiwa ni muumini wa kweli wa kuendelza na kudumisha misingi ya Muungano.

Rais Dk Magufuli tokea aapishwe kikatiba na kisheria ili kuongoza nchi yetu, amekuwa shupavu, mahiri ambaye hayumbi katika kuhakikisha hakuna kikundi au mtu anayegusa au kujaribu kuitikisa misingi ya Muungano .

Katika miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Taifa letu limeendelea na kubaki katika mikono salama, tumedumisha misingi ya amani, mshikamano, umoja na kupata mafanikio makubwa ya kimaendeleo.
Vijana na Maadhimisho ya Sherehe za Muungano Mkoani Dodoma
Ndugu Waandishi wa habari

Sherehe za miaka 53 ya Muungano kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu tokea kuundwa Muungano wetu, mwaka huu zitaadhimishwa katika Makao Makuu ya nchi yetu mkoani Dodoma.*

Nachukua nafasi hii kwa unyenyekevu mkubwa kuwaomba vijana wote wa mkoa wa Dodoma na Mikoa mengine ya jirani, kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika maadhimisho hayo ya Muungano wetu unaofikisha miaka 53.

Huu ni wakati wa Vijana nchini kutembea kifua mbele, kujivunia na kujitokeza kwa wingi ili kushiriki katika maadhmisho hayo kwasababu wao/sisi sasa ndiyo wenye muungano huu, tumezaliwa katika mazingira ya kuundwa na kuzaliwa muungano kwa miaka yote hiyo.

UVCCM inawaomba pia kuwasihi vijana wote nchini bila kujali itikadi zao za kisiasa, wajitokeze mapema kwani wanapaswa kushiriki , kujionea mambo yaliotayarishwa na serikali ambayo yatawapa ufahamu na mafunzo ndani yake.

*Mabadiliko ya Kimuundo ndani ya UVCCM*
Ndugu Waandishi wa habari
Dhana ya kuundwa Jumuiya ya vijana na malengo yake ya msingi ni kuwaoka vijana, kuwaandaa kifikra, kifalsafa, kiitikadi na kimaadili.

UVCCM ni tanuri, benki na jiko linalowapiga msasa vijana wake ili
kuja kuwa warithi wa madaraka ya kiserikali na kisiasa, hakuna kijana anayejiunga UVCCM kuanzia ngazi ya tawi, kata, jimbo, wilaya, mkoa hadi Taifa akiwa ni mjuzi aliyekamilika na mwenye ufahamu mpana wa kila jambo, yote huyapata siku baada ya siku ndani ya UVCCM.

Aidha kujua kuelewa kwake, kujifunza, kufunzwa, kupikwa kisiasa, kimaadili na kinidhamu pia huyapata masomo hayo anapokuwa mwana jumuiya huku akiwa hakurupuki au kutoa shutuma zisizo mashiko. Anayesema kila anayeshika nafasi UVCCM anajua na bingwa sana hiyo ni hoja dhaifu.

UVCCM ni taasisi kubwa ambayo karibuni inatimiza miaka 40 tokea kuundwa kwa mwaka 1978, tokea ilipoundwa hadi leo inaongozwa na kanuni, taratibu, miongozo na kusimamiwa na katiba ya Chama cha Mapinduzi sehemu ya nne, Ibara ya 129 (1)a

Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM iliyokutana katika kikao chake cha tarehe 11/03/2017 Dodoma ilipitisha mabadiliko ya kumi ya kanuni ya UVCCM toleo la 2017 ambayo pamoja na mambo mengine yamegusa marekebisho makubwa ya muundo wa UVCCM.

Kufuatia mabadiliko hayo imelazimu matakwa ya kikanuni yafuatwe katika maeneo nyeti ikiwemo uwepo wa Wakuu wa Idara za Makao Makuu pamoja na utaratibu wa utumishi ndani ya jumuiya ili kuendana na matakwa ya Katiba ya Chama Cha Mapinduzi.

Awali kulikuwa na Idara nne za makao makuu ya UVCCM baada ya mabadiliko idara zimekuwa 5 na baadhi ya idara zimepunguziwa vitengo na kuhamishiwa katika idara nyengine, wakati huo huo baadhi ya wakuu wa idara waliokuwa wakishikilia nafasi hizo hivi karibu wameteuliwa kuwa makatibu CCM wa wilaya hivyo kufanya idara kuwa wazi.

Kamati ya utekelezaji ya UVCCM Taifa iliyokutana katika kikao chake cha tarehe 18/04/2017 Upanga jijini dar Es Saalama pamoja na mambo mengine kwa mamlaka waliyonayo kikanuni Ibara ya 88,Idara za Umoja wa Vijana wa CCM na Ibara ya 89 Uteuzi wa Wakuu wa Idara za Makao Makuu Uk 116ilikaimisha nafasi zote za Idara ili kukamilisha Muundo wa Kamati Tendaji ya UVCCM (Sekretariet) kama ifuatavyo:

*Ndg Dorice H. Obeid* – *Idara Uchumi, Uwezeshaji na Fedha.*
*Ndg Daniel M. Zenda*– *Idara ya Vyuo na Vyuo Vikuu*
*Ndg Jokate U. Mwegelo - Idara Uhamasishaji na Chipukizi*
*Ndg Mohamed A. Abdalla - Idara ya Organization, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.*
  Ndg Israel Sostenes
Idara ya Usalama na Maadili
UPOTOSHAJI NA UZUSHI DHIDI YA UVCCM.

Jamii inatambua, kuelewa na kufahamu sana kazi nzuri zinazofanywa na vyombo vya habari nchini. Kazi ya uandishi wa habari inaheshima, thamani na daraja ya pekee kwa sababu kazi hiyo kikanuni huwa haiegemei upande mmoja, haionei, haizui wala kupakazia watu kwa kuwavunjia staha na heshima zao.

Inapotokea mtu anayejigamba ni mwandishi wa habari mwenye taaluma, anayetegemewa katika jamii na chombo chake, akaanza ufundi wa kutunga uongo na kuufanya ni sehemu ya habari, akauamini na kuanza kuueneza aina ya mwandishi huyo hujipotezea sifa, hadhi na kuviza heshima yake na wengine.

Kalamu ya mwandishi aliyesomea taaluma ya habari akafuzu vyema haigeuki na kuwa msumari wa moto ili kuwadhuru, kuadhibu, kutesa na kudhalilisha watu wengine kwa sababu binafsi, amekosa jambo alilolihitaji, kuomba au kuandika habari kwa makusudi ya kufanya vitisho, nafikiri huko ni kupofuka kitaaluma na kukiuka maadili ya uandishi.

Kazi ya uandishi ni ngumu na nzito. Ni kazi yenye changamoto nyingi lakini pale inapofanyika kwa kufuata taratibu za kitaaluma, miiko na kanuni zake, kazi hiyo huwa rahisi, nyepesi na yenye kumjengea mwandishi haiba njema na kujikuta akipata heshima na taadhima.

Kwa takribana majuma mawili sasa Gazeti la Tanzanite limeibuka na kuusakama Umoja wa Vijana wa CCM kwa kuandika taarifa za uongo, uchochezi na upotoshaji ili kuichafua jumuiya na Chama Cha Mapinduzi mbele ya Watanzania walio wengi.

Katika toleo la Jumatatu 10-16/04/2017 toleo la 06 lenye kichwa cha habari “UVCCM isafishwe” habari kamili UK 5 na gazeti hilo hilo la Jumatatu 24-30/2017 toleo la 07 kichwa cha habari “Kashfa nzito UVCCM” habari Uk 4.

Umoja wa Vijana wa CCM wakati tunatafakari hatua stahiki za kuzichukua tunamtaka mhariri wa gazeti hilo kuomba radhi ndani ya siku 7 akitumia ukurasa wake wa mbele na maandishi yale yale aliyoyatumia kuichafua taasisi yetu. UVCCM ni taasisi kubwa kisiasa hatuwezi kuona genge la watu wenye nia ovu wakitumia uhuru uliopitiliza kuharibu taswira njema iyodumu kwa miaka 40 sasa.

Ndugu Waandishi wa habari

Mwisho ni vyema watanzania wote wakafahamu sasa kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Mwenyekiti wa CCM Dk John Pombe Magufuli ndani ya Serikali kurudisha nidhamu ya matumizi na kudhibiti mapato ya Serikali ndio kazi hiyo hiyo inayoendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi na jumuiya zake na sasa kumekuwa na heshima na nidhamu katika masuala ya mapato na matumizi ya fedha za chama na jumuiya zake.

UVCCM inampongeza kwa dhati Mwenyekiti Dk Magufuli kwa dhamira yake njema ya kuimarisha Chama kimfumo, kiutendaji na udhibiti wa mapato na matumizi.

Kidumu Chama Cha Mapinduzi
Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU (UVCCM)
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com