Mgogoro
wa uongozi unaoendelea ndani ya chama cha CUF huenda ukaathiri ushiriki
wake kwenye uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Januari 27 baada ya
pande zote mbili zinazosigana kujiandaa kuteua wagombea.
Mbali ya mgogoro huo kuhofiwa
kukiathiri chama pengine hadi kusababisha wagombea wake kuzuiwa, pia
unaweza kuudhoofisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Habari kutoka ndani ya chama hicho
zinasema upande wa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
anayetambuliwa na Msajili wa vyama vya siasa uko kwenye maandalizi
ilhali ule wa Katibu Mkuu, Seif Sharrif Hamad unatarajiwa kukutana na
watendaji wa chama kujadili ushiriki wao.
Profesa Lipumba aliyeiongoza CUF tangu
mwaka 1995, alijiuzulu kwa hiari uenyekiti wake Agosti 2015 lakini siku
chache kabla ya CUF kuitisha mkutano Agosti mwaka huu wa kujadili barua
yake, aliandika barua ya kutengua kujiuzulu na akarejea kazini.
Siku ya mkutano mkuu uliofanyika Ubungo
Plaza, wajumbe waliridhia kujiuzulu kwake lakini walipoingia kuchagua
mrithi wake, wafuasi wa Profesa Lipumba walivamia mkutano na kuuvuruga
hali iliyosababisha baadaye kusimamishwa kwake.
Alipoulizwa jana namna CUF yenye
mgogoro itakavyoshiriki uchaguzi wa madiwani katika kata 22 Bara na
ubunge wa Jimbo la Dimani, Zanzibar, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya
Uongozi CUF, Julius Mtatiro alisema wapo katika mikakati kuhakikisha
wanashiriki kikamilifu.
Mtatiro alisema muda wowote kuanzia
sasa Katibu Mkuu, Maalim Seif atakutana na watendaji wa chama kujadili
kwa kina suala hilo na kutoa maelekezo.
“Tutashiriki vizuri na niwaweke wazi
Watanzania kuwa shughuli za chama zinaendelea kama kawaida hivyo kamati
za utendaji zitatimiza wajibu wake wa kuwapitisha wagombea watakaojitosa
kwenye kinyang’anyiro,” alisema.
Kuhusu Profesa Lipumba, Mtatiro
alisema, “Hatuwezi kufanya kazi na mtu wa CCM kumsogeza karibu yetu ni
kumleta atuharibie chama jambo ambalo hatuwezi kuliruhusu. Ingekuwa lile
suala la kujiuzulu aliteleza tungemwelewa na kumsamehe lakini
inavyoonekana yupo kwenye mipango yake katu hatuwezi kumuweka karibu.”
Lakini Naibu Mkurugenzi wa Habari na
Uenezi wa CUF anayemuunga mkono Lipumba, Abdul Kambaya alisema, “Tuna
kikao leo (jana) upande wa Bara chini ya Mwenyekiti Profesa Lipumba
kujadili suala hilo la uchaguzi, kuhusu upande wa Zanzibar sifahamu
chochote.”
Akizungumzia uchaguzi huo mdogo, Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu alisema Ukawa
utakuwa bega kwa bega na CUF katika uchaguzi huo kwani wanaitambua kuwa
iko moja si mbili kama inavyotengenezwa na watu wasiopenda maendeleo ya
chama hicho.
0 comments:
Post a Comment