Thursday, December 8, 2016

MGOGORO LIPUMBA NA MAALIM SEIF KUIDHOOFISHA CUF UCHAGUZI MDOGO ZNZ

Mgogoro wa uongozi unaoendelea ndani ya chama cha CUF huenda ukaathiri ushiriki wake kwenye uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Januari 27 baada ya pande zote mbili zinazosigana kujiandaa kuteua wagombea.

Mbali ya mgogoro huo kuhofiwa kukiathiri chama pengine hadi kusababisha wagombea wake kuzuiwa, pia unaweza kuudhoofisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Habari kutoka ndani ya chama hicho zinasema upande wa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na Msajili wa vyama vya siasa uko kwenye maandalizi ilhali ule wa Katibu Mkuu, Seif Sharrif Hamad unatarajiwa kukutana na watendaji wa chama kujadili ushiriki wao.PROF IBRAHIM LIPUMBA

Profesa Lipumba aliyeiongoza CUF tangu mwaka 1995, alijiuzulu kwa hiari uenyekiti wake Agosti 2015 lakini siku chache kabla ya CUF kuitisha mkutano Agosti mwaka huu wa kujadili barua yake, aliandika barua ya kutengua kujiuzulu na akarejea kazini.

Siku ya mkutano mkuu uliofanyika Ubungo Plaza, wajumbe waliridhia kujiuzulu kwake lakini walipoingia kuchagua mrithi wake, wafuasi wa Profesa Lipumba walivamia mkutano na kuuvuruga hali iliyosababisha baadaye kusimamishwa kwake.

Alipoulizwa jana namna CUF yenye mgogoro itakavyoshiriki uchaguzi wa madiwani katika kata 22 Bara na ubunge wa Jimbo la Dimani, Zanzibar, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF, Julius Mtatiro alisema wapo katika mikakati kuhakikisha wanashiriki kikamilifu.

Mtatiro alisema muda wowote kuanzia sasa Katibu Mkuu, Maalim Seif atakutana na watendaji wa chama kujadili kwa kina suala hilo na kutoa maelekezo.

“Tutashiriki vizuri na niwaweke wazi Watanzania kuwa shughuli za chama zinaendelea kama kawaida hivyo kamati za utendaji zitatimiza wajibu wake wa kuwapitisha wagombea watakaojitosa kwenye kinyang’anyiro,” alisema.

Kuhusu Profesa Lipumba, Mtatiro alisema, “Hatuwezi kufanya kazi na mtu wa CCM kumsogeza karibu yetu ni kumleta atuharibie chama jambo ambalo hatuwezi kuliruhusu. Ingekuwa lile suala la kujiuzulu aliteleza tungemwelewa na kumsamehe lakini inavyoonekana yupo kwenye mipango yake katu hatuwezi kumuweka karibu.”

Lakini Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF anayemuunga mkono Lipumba, Abdul Kambaya alisema, “Tuna kikao leo (jana) upande wa Bara chini ya Mwenyekiti Profesa Lipumba kujadili suala hilo la uchaguzi, kuhusu upande wa Zanzibar sifahamu chochote.”

Akizungumzia uchaguzi huo mdogo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu alisema Ukawa utakuwa bega kwa bega na CUF katika uchaguzi huo kwani wanaitambua kuwa iko moja si mbili kama inavyotengenezwa na watu wasiopenda maendeleo ya chama hicho.

No comments:

Post a Comment