MAITI
sita ambazo hazijatambulika zimekutwa zikielea katika Mto Ruvu eneo la
Bagamoyo, Mkoa wa Pwani zikiwa zimehifadhiwa kwenye mifuko ya sandarusi
maarufu viroba vya uzito wa kilogramu 200, huku zikiwa zimeharibika
vibaya.
Akizungumza jana, Diwani wa Kata ya
Makurunge, Paul Kabile alisema maiti hizo ambazo ni za jinsia ya kiume
ziligunduliwa na wavuvi.
Kabile alisema maiti tano ziligunduliwa
Desemba 6, majira ya alfajiri kwenye Kitongoji cha Kitopeni wilayani
Bagamoyo, ambako wavuvi hao waligundua miili hiyo wakati wakiendelea na
shughuli zao za uvuvi kwenye mto huo.
“Maiti hizo kila moja ilikuwa
imehifadhiwa kwenye kiroba huku zikiwa zimewekewa mawe na mifuko hiyo
ikiwa imeshonwa juu kama vile yamehifadhiwa mahindi au mchele,” alieleza
Kabile na kuongeza kuwa wavuvi hao baada ya kuziona maiti hizo
walizizika kutokana na kuharibika sana na kushindwa kuzipeleka hospitali
kuzihifadhi.
“Wavuvi hao walizizika maiti hizo huku
kukiwa hakuna taarifa yoyote juu ya kuwa zimetokea wapi na ni watu gani
waliofanya tukio hilo,” alisema Kabile na kubainisha kuwa maiti nyingine
moja iligundulika jana.
Mwandishi wa Habari wa Jeshi la Polisi
Mkoa wa Pwani, Hassan Mtengevu alithibitisha kutokea tukio hilo, na
kueleza kuwa wanafanya uchunguzi kwa kushirikiana na daktari ili
kufahamu watu hao walikufa kwenye mazingira gani.
0 comments:
Post a Comment