Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Ummy A.
Mwalimu anapenda kutoa ufafanuzi kuhusu Tamko la Shirikisho la Watu
Wenye Ulemavu nchini (SHIVYAWATA) kuhusu makundi ya wananchi
wanaostahili kupata msamaha wa matibabu. Aidha, baadhi ya Vyombo vya
habari vimenukuu maelezo ambayo yametolewa na mwenyekiti wa SHIVYAWATA
kuhusu Makundi yanayostahili kupata msamaha wa Matibabu nchini.
Kutokana
na Maelezo hayo, napenda kutoa ufafanuzi ufuatao; Sera ya Afya ya Mwaka
(2007) inatambua kuwa wapo wananchi ambao wanakabiliwa na changamoto
mbalimbali katika kuzifikia huduma za Afya wakiwemo watu Wenye
Ulemavu. Aidha, Kwa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na.9/2010 ambayo,
pamoja na mambo mengine, Sheria inabainisha kuwa Watu Wenye Ulemavu wana
haki ya kuondolewa vikwazo katika kupata huduma za Afya.
Kwa
kuzingatia maelekezo ya Sera ya Afya (2007) na Sheria ya Watu Wenye
Ulemavu(2010) Wizara yangu inatambua na itaendelea kuhakikisha kwamba
Watu Wenye Ulemavu Wasio na Uwezo wa kugharamia huduma za Matibabu
wanapatiwa Msamaha wa Matibabu katika Ngazi zote kuanzia Zahanati, Vituo
vya Afya, Hospitali za Mikoa na Hosptali za Rufaa. Pia kwa kutambua
umuhimu wa huduma ya Afya kwa Wananchi wote, Serikali kupitia Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ipo katika mchakato wa
kutungwa kwa sheria itakayowezesha wananchi wote wakiwemo Watu Wenye
Ulemavu kupata Kitambulisho cha Bima ya Afya. Hatua hii itawaondolea
vikwazo, wananchi wote wakiwemo watu Wenye Ulemavu katika kuzifikia
huduma za Afya pasipo kikwazo cha ukosefu wa fedha.
Naomba
kuchukua fursa hii kuwahakikishia ndugu zangu Wenye Ulemavu kuwa wanayo
haki ya kupata huduma za matibabu katika ngazi zote. Aidha, Serikali
itaendelea kusimamia na kuhakikisha makundi maalum wakiwemo watu Wenye
Ulemavu ambao hawana uwezo wa kuchangia huduma za Matibabu wanapata
msamaha wa matibabu katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya.
Natoa
maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwatambua Watu Wenye
Ulemavu Wasio na Uwezo wa kuchangia huduma za matibabu na kuimarisha
Kitengo cha Huduma za Ustawi wa Jamii katika vituo vya kutolea huduma
za Afya ili viweze kuwatambua na kutoa msamaha kwa watu wenye ulemavu
wasio na uwezo ili waweze kupatiwa matibabu bila ya vikwazo vya ukosefu
wa fedha.
Aidha,
ni marufuku kwa Mtumishi yeyote wa Sekta ya Afya kuonesha vitendo
vyovyote vya unyanyapaa na unyanyasaji kwa Watu Wenye Ulemavu wanaofika
katika vituo vya kutolea huduma za afya. Mtumishi atayethibitika
kuonesha kwenda kinyume cha maadili ya utumishi wa umma na taaluma za
Afya kwa kufanya vitendo vya vya unyanyapaa na unyanyasaji kwa makundi
maaalum ikiwemo watu wenye ulemavu atachukuliwa hatua za kinidhamu
ikiwemo kufukuzwa kazi.
Wizara yangu inafanya jitihada kuhakikisha kuwa inaondoa vikwazo vyote vinavyowanyima watu wenye ulemavu kupata huduma za afya wanazohitaji ikiwemo kuhakikisha kuna mazingira mazuri yanayowawezesha kufika hospitali kwa kuweka miundo mbinu rafiki kwa watu wenye ulemavu. Vile vile, ninawataka watoa huduma wote kuwapa kipaumbele watu wenye ulemavu wanapofika hospitali. Wapatiwe huduma haraka ili kuwapunguzia usumbufu kutokana na mahitaji yao ya kimwili. Kama ambavyo tumefanya kwa Wazee niwaagiza kila kiongozi ahakikishe anaweka utaratibu mzuri wa kuwapa nafasi ya kwanza watu wenye ulemavu tukijifunza kwa jinsi tulivyofanya na kufanikiwa katika eneo la kuhudumia wazee.
Watu
wenye ulemavu ni wenzetu, watoto wetu, ndugu na jamaa zetu. Tuwahudumie
kwa upendo na kuhakikisha wanapata fursa sawa na wengine
Imetolewa na
MHE. UMMY A. MWALIMU (Mb.)
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto
15/10/2016
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto
0 comments:
Post a Comment