METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, September 14, 2016

UN Ban Ki Moon New York
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema anakatishwa tamaa na viongozi wengi duniani ambao hujali zaidi kusalia madarakani badala ya kuboresha maisha ya watu wao.

Akikaribia kuhitimisha miaka 10 ya utawala wake katika Umoja wa Mataifa, Ban amezungumzia waziwazi hali ya kidunia, mafanikio, kushindwa kwake na kukatishwa tamaa kama mkuu wa taasisi hiyo katika mahojiano aliyoyafanya na shirika la habari la Associated Press. Miongoni mwa mambo aliyoyagusia ni suala la haki za binadamu ambalo amekuwa akilalamikiwa kwamba hajafanya ya kutosha katika kulizungumzia. Amenukuliwa akisema kwamba "nina matumaini kwamba katika kipindi cha mrithi wangu, nchi wanachama watakuwa na umoja zaidi na kuonyesha mshikamano juu ya haki za binadamu na masuala ya kibinadamu na kwa dhamira yetu tutaweza kukomesha vurugu kwa kasi zaidi."

Kiongozi huyo pia amekosoa namna Umoja wa Mataifa unavyofanya kazi akisema ni suala lisilowezekana kwa katibu mkuu yoyote "kuwa mtu kamilifu" kwasababu yeye amekuwa mtekelezaji wa maamuzi yanayopitishwa na mhimili wa taasisi hiyo. Anasema Umoja wa Mataifa ungekuwa na ufanisi zaidi kama kungekuwepo na mchakato wa kufanya maamuzi na siyo ule unaoihitaji maafikiano kwa masuala mengi mbele ya Baraza la Usalama na tamko kutoka katika baraza hilo.

Anasema suala hili uipatia nguvu nchi moja kuzuia kitu ambacho mataifa yote wamekubaliana, akiuliza kwamba Je hii ni sawa? katika karne ya 21 ambapo una mataifa 193 wanachama? alisema Ban.

Mtazamo wake dhidi ya ule wa magharibi

Akilinganisha mtazamo wake na viongozi wa kimagharibi, Ban amesema mara nyingi wamekuwa wakizungumza kupitia matamko, ambalo ni jambo jepesi na wakati mwingine wamekuwa wakimshinikiza kutozungumza au kutembelea nchi. Lakini anasema alifanya vile alivyotaka kwasababu anaamini mikutano ya ana kwa ana na viongozi wa dunia ni muhimu katika kupata uungwaji mkono wao wa kumaliza migogoro au masuala ya mabadiliko ya tabia ya nchi na kutokemeza umaskini.

Kwa viongozi wengi, cha muhimu ni kuchaguliwa kwa njia yoyote na wakishachaguliwa wanatawala watu na wengi hupotoshwa na hawaheshimu sauti za wananchi. Kuhusu Syria Ban anasema hajui kwanini wameshindwa kumaliza mgogoro huo. Masuala mengine aliyoyagusia ni pamoja na vitendo vya udhalilishaji ngono vinavyofanywa na walinda amani dhidi ya wanawake na wasichana.

Baada ya kumaliza uongozi wake katibu mkuu huyo atarejea nchini mwake Korea Kusini " nitajaribu kuona kitu gani ni bora naweza kuchangia katika maendeleo ya nchi yangu kama katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa" amesema kiongozi huyo.

Ban Ki Moon aliyemrithi Koffi Annan 2007 atamaliza uongozi wake mwezi Disemba na katika kipindi chake atakumbukwa kwa jitihada zake za kupigania masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, malengo mapya 17 endelevu ya Umoja wa Mataifa, kuhamasisha usawa wa kijinsia ambapo alifanikiwa kuanzisha chombo maalumu cha Umoja huo cha kuyashughulikia masuala ya wanawake.

DW
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com