Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Songwe
Jamii imetakiwa kuachana na ulaji usiofaa badala yake kuweka msisitizo kwa ulaji wa chakula kwa kufuata kanuni bora kwani takwimu zinaonyesha kuwa magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari na shinikizo la damu yamekuwa yakiongezeka hususani kwa jamii za watu waishio mijini. Kwa mfano, kisukari kwa watu wazima ni asilimia 9.1 (STEP, 2012), wanawake wenye umri kati ya 15-49 waishio mjini asilimia 37 wanauzito uliozidi, uzito uliozidi chini ya miaka 5 ni 3.6% (THDS, 2015) na uzito uliozidi kwa watu wazima ni 29% (STEP, 2012).
Serikali kupitia Programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo-ASDPII imejipanga kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuongeza tija kwenye kilimo ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza kipato cha wananchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ameyasema hayo tarehe 16 Octoba 2020 wakati akitoa salamu kwenye kilele cha maadhimisho haya ya 40 ya Siku ya Chakula Duniani Kitaifa yaliyofanyika Mkoani Njombe huku akizipongeza kamati za maandalizi ngazi ya Taifa na Mkoa kwa maandalizi mazuri ambapo (Kesho Njema Inajengwa na Lishe Bora Endelevu) ambayo inatilia mkazo ulaji unaofaa kwa ajili ya lishe bora endelevu.
Kusaya Amesema kuwa, tarehe 16 Oktoba ya kila mwaka Tanzania huungana na nchi wanachama wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) katika kusherehekea Siku ya Chakula Duniani. Chimbuko la Siku hiyo ni Mkutano wa mwaka 1979 ambapo nchi wanachama wa FAO zilikutana Jijini Quebec nchini Canada na kujadili kiundani masuala mbalimbali kuhusu chakula. Mojawapo ya maazimio ya mkutano huo ilikuwa ni kutenga siku moja ya kila mwaka ili kuzungumzia na kutafakari njia na mbinu mbalimbali za kupata chakula cha kutosha kwa watu wote duniani na kwa wakati wote.
Amebainisha kuwa Maadhimisho haya ya Siku ya Chakula Duniani mwaka 2020 ambayo uadhimishwa kila mwaka, yanafanyika katika kipindi ambacho Dunia inatilia mkazo masuala ya lishe na usalama wa chakula ili kukabiliana na ongezeko kubwa la idadi ya watu ambapo inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 Idadi ya watu itafikia Bilioni 9.
Hivyo basi jitihada mbalimbali zinafanywa na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha kuna uwiano sawa kati ya uzalishaji wa chakula na ongezeko hili la idadi ya watu. Mfano; Azimio la Malabo linatutaka kupunguza upotevu wa mazao ya chakula kwa asilimia 50 ifikapo 2025, malengo endelevu ya millennia yanatutaka kukomesha umaskini na baa la njaa ifikapo 2030 na maazimio mengine ya kikanda na kimataifa hivyo hivyo yanasisitiza kilimo chenye tija kwa ajili ya kumkomboa mkulima hasa wa kawaida.
Katibu Mkuu Kusaya ameeleza kuwa Kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano mfululizo, Tanzania imeendelea kutekeleza maazimio haya kupitia uboreshaji wa sera, sheria na programu mbalimbali. Aidha, Wizara ya Kilimo imetekeleza mpango wa Kitaifa NMNAP, ASDP-II, mpango wa Lishe katika kilimo vile vile Wizara inaratibu na kutekeleza mradi wa kudhibiti sumukuvu-TANIPAC lengo ikiwa ni kupunguza upotevu, kuimarisha usalama wa chakula na biashara.
Kwa upande wa Lishe, Katibu Mkuu Kusaya amesema kuwa hali imeendelea kuboreka hususani kupungua kwa hali ya udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano ambapo kulingana na takwimu za Wizara ya Afya za mwaka 2018 udumavu umepungua na kufikia asilimia 32 ukilinganisha na asilimia 34 mwaka 2015.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment