
Kufuatia kutoridhishwa na thamani
ya fedha iliyotumika katika kujenga miradi miwili ya Soko la Mazao
lililopo Kata ya Makoka na Mnada wa Mifuko wa Kijiji cha Mbande wilayani
Kongwa, Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe, Deo Ndejembi ameiagiza Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU kufanya uchunguzi kwenye miradi
hiyo.
DC Ndejembi ametoa agizo hilo
wakati alipofanya ziara ya kukagua miradi hiyo inayojengwa kwa
ushirikiano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa pamoja na Ubalozi wa
Denmark nchini.

” Hatujaridhishwa na money for
value kwenye miradi hii, kiasi cha Shilingi Milioni 56 kilichotumika
kwenye mradi wa Mnada na Milioni 200 zilizotumika mpaka sasa kwenye Soko
la Mazao haziendani na hiki tulichokiona. Muonekano wa miradi hauakisi
thamani ya fedha tunayoambiwa, hivyo naagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi
mara moja na kuniletea ripoti ili tujue ukweli na kama ni hatua
tuchukue,” Amesema DC Ndejembi.
Katika ziara hiyo DC Ndejembi
ameambatana na Wawakilishi wa Balozi wa Denmark ambapo aliwaomba pia
kupitia Taasisi ya LIC kuweza kutoa sapoti yao kwenye ujenzi wa kiwanda
cha maziwa ili kiweze kukamilika na kutoa ajira kwa kundi kubwa la
vijana wa Kongwa pamoja na kuongeza mapato ndani ya Wilaya hiyo.
Nae Kiongozi wa Timu ya Maendeleo
ya Biashara kutoka Ubalozi wa Denmark, Bi Jema Ngwale amemuahidi DC
Ndejembi kuendelea kushirikiana nae katika kuwaletea maendeleo wananchi
wa Kongwa.

” Suala la kiwanda hiki cha maziwa
tumelichukua na naamini litakwisha, tunajua kikikamilika ni faida kwa
Wananchi wa hapa kwenye ajira lakini pia itakuza uchumi wa Kongwa na
hivyo kufanikisha azma ya Rais Magufuli katika kufikia uchumi wa kati
kupitia viwanda, hivyo nakuahidi tumelichukua,” Amesema Bi Jema.
0 comments:
Post a Comment