
Na Ismail Ngayonga,MAELEZO
DAR ES SALAAM
SEKTA ya Kilimo nchini
imeendelea kuwa ni Sekta muhimu katika maendeleo ya uchumi wa
wananchi na taifa kwa ujumla hususan katika wakati huu tunapojizatiti
kufikia uchumi wa viwanda.
Katika mwaka 2017, sekta hiyo
ilitoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 65.5, ikichangia asilimia 28.7
ya Pato la Taifa ambapo sekta ndogo ya mazao ilichangia asilimia 16.58.
Takwimu zinaonesha kuwa katika
robo ya kwanza ya mwaka 2018, ukuaji wa Sekta ya Kilimo ulifikia
asilimia 7.1, ukuaji huo ulichangiwa na hali nzuri ya hewa na jitihada
za Serikali za kuhakikisha kuwa pembejeo zinawafikia wakulima kwa
wakati.
Kutokana na matumizi
yasiyoridhisha ya pembejeo muhimu na kutozingatiwa kwa kanuni bora za
kilimo, Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa kuwezesha pembejeo muhimu
zikiwemo mbegu bora, mbolea na viuatilifu kuwafikia wakulima kwa
wakati.
Takwimu zinaonesha kwamba matumizi
ya zana bora za kilimo yanaongezeka miongoni mwa wakulima ambapo kwa
mwaka 2018 wastani wa kitaifa wa matumizi ya zana bora za kilimo
umeongezeka hadi kufikia asilimia 20 kwa matrekta na asilimia 27 kwa
wanyama kazi ikilinganishwa na asilimia 14 ya matrekta na asilimia 24 ya
wanyama kazi mwaka 2013.
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo
imeendelea kuimarisha mifumo ya masoko na kuratibu mazao makuu ya
kimkakati ikiwemo korosho, tumbaku, kahawa, chai na pamba hatua
iliyosaidia kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao hayo kutoka tani 901,641
mwaka 2016/2017 hadi tani 967,184 mwaka 2017/2018.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio
ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa Kilimo
Japhet Hasunga anasema katika msimu wa 2018/2019, Wizara ya Kilimo
ililenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara hadi kufikia tani
1,356,368 ambapo hadi kufikia mwezi Machi 2019, takribani tani 667,631
ikiwa ni sawa na asilimia 49.2 ya lengo zimezalishwa.
Kuhusu zao la korosho, Waziri
Hasunga anasema katika kuendeleza zao hilo Serikali imesambaza miche
bora 12,252,197 katika mikoa 17 inayolima zao hilo kati ya miche
13,661,433 iliyozalishwa kupitia mikataba iliyoingiwa msimu wa 2017/2018
baina ya Bodi ya Korosho na wazalishaji 678.
Hasunga anasema katika mwaka
2018/2019, mbegu za korosho kilo 47,484 ambazo zitazalisha miche
6,647,760 ya kutosheleza ekari 391,045 zimezalishwa na Kituo cha Utafiti
cha Naliendele na kusambazwa katika mikoa 20 na uzalishaji wa miche
unaendelea.
“Mwaka 2018/2019, Wizara
imesimamia ununuzi wa pembejeo za zao la korosho kwa utaratibu wa pamoja
kupitia zabuni na Vyama vya Ushirika ili kuhakikisha kuwa wakulima
wanapata pembejeo kwa wakati na kwa bei nafuu” anasema Waziri Hasunga.
Anaongeza kuwa kupitia utaratibu
huo, jumla ya tani 31,500 na lita 520,000 za salfa zimenunuliwa ambapo
wakulima wamenunua jumla ya tani 1,994.175 na lita 14,283 na bakaa ya
viuatilifu vilivyonunuliwa kwa njia ya zabuni ni tani 29,505.825 na lita
505,717 za salfa ambavyo vinaendelea kuuzwa kwa wakulima kwa ajili ya
msimu wa 2019/2020.
Akifafanuza zaidi Waziri Hasunga
anasema Wizara kupitia Bodi ya Korosho inaendelea na usajili wa wakulima
wa korosho ambapo hadi kufika Machi 2019, wakulima 200,000
wamesajiliwa, ambapo bodi hiyo pia imeandaa mfumo endelevu ambao
utawawezesha maafisa katika kila Halmashauri kukusanya na kuhuisha
taarifa kwa kutumia simu za mkononi.
Katika upande wa mafunzo, Hasunga
anasema Serikali imeendesha mafunzo ya udhibiti ubora wa korosho ghafi
kwa wataalamu 63 katika Halmashauri za Mkuranga, Kibiti, Masasi,
Ruangwa, Nachingwea na Tunduru na kuhusisha wataalamu kutoka Bodi ya
Usimamizi ya Stakabadhi za Ghala, waendesha ghala na wanunuzi.
Hadi kufikia tarehe 30 Aprili
2019, jumla ya tani 222,825 zimekusanywa kutoka kwa wakulima, kati ya
hizo tani 211,184 zimehakikiwa na tani 177,357 zenye thamani ya Tsh
Bilioni 578.5 zimelipwa kwa wakulima 379,283, na hizo kuuzwa korosho kwa
bei elekezi ya Tsh 3,300 kwa kilo ya korosho ghafi daraja la kwanza na
Tsh. 2,640 kwa kilo ya korosho ghafi daraja la pili bila makato.
0 comments:
Post a Comment