
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema mahusiano kati ya Serikali na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi
wa kidini, kimila ni muhimu yakaimarishwa.
Ameyasema hayo jana (Jumanne,
Septemba 24, 2019) wakati akipokea taarifa ya mkoa wa Iringa alipowasili
kwenye uwanja wa ndege wa Iringa kwa ajili ya ziara ya kikazi.
Waziri Mkuu alisema ni lazima
mahusiano hayo yakadumishwa katika ngazi zote kwa sababu Serikali ipo
kwa ajili ya wananchi wote na inawahudumia bila ya ubaguzi.
Aliwataka viongozi waliopewa
dhamana ya kusimamia maeneo mbalimbali nchini wahakikishe wanatekeleza
majukumu yao ipasavyo na uwajibikaji wao uwe na tija.
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa watendaji wahakikishe suala la ukusanyaji wa mapato linapewa kipaumbele katika maeneo yao.
“Ukusanyaji wa mapato ni muhimu
kwa ajili ya maendeleo ya Taifa kwa sababu miradi ya maendeleo kama
ujenzi wa shule haiwezi kutekelezeka bila ya kukusanya mapato.”
Awali, Akisoma taarifa ya mkoa,
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi alisema mkoa huo umepewa zaidi ya sh.
bilioni saba kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za wilaya.
Alisema fedha hizo zimetumika kwa
ajili ya ujenzi wa hospitali kwenye Manispaa ya Iringa (98%),
Halmashauri ya wilaya ya Iringa (90%), Kilolo(99%), Mufindi (89%).
Mkuu huyo wa mkoa alisema mbali na
fedha hizo za ujenzi wa hospitali pia Serikali imetoa zaidi ya sh.
bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya.
Akizungumzia kuhusu uchaguzi wa
Serikali za mitaa, kiongozi huyo alisema wanaendelea na maandalizi.Mkoa
una vijiji 360, mitaa 222 na vitongoji 2,216
0 comments:
Post a Comment