METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, September 5, 2020

SERIKALI YASIMAMIA BIL 20.1 KULIPWA WAKULIMA WA KAHAWA KAGERA-WAZIRI HASUNGA

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga Leo tarehe 5 Septemba 2020 akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera kuhusu hali ya malipo ya wakulima waliokuwa wanavidai vyama vikuu vya Ushirika KCU na KDCU vilivyokusanya kahawa yao. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga Leo tarehe 5 Septemba 2020 akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera kuhusu hali ya malipo ya wakulima waliokuwa wanavidai vyama vikuu vya Ushirika KCU na KDCU vilivyokusanya kahawa yao

Sehemu ya Viongozi wa Wizara ya Kilimo kadhalika Bodi ya Kahawa wakifatilia mkutano wa Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga Leo tarehe 5 Septemba 2020 na waandishi wa habari katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera kuhusu hali ya malipo ya wakulima waliokuwa wanavidai vyama vikuu vya Ushirika KCU na KDCU vilivyokusanya kahawa yao

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga Leo tarehe 5 Septemba 2020 akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti kuhusu hali ya malipo ya wakulima waliokuwa wanavidai vyama vikuu vya Ushirika KCU na KDCU vilivyokusanya kahawa yao

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Kagera

Makusanyo ya kahawa Mkoani Kagera yamefikia kilo milioni 64.013 zenye thamani ya shilingi bilioni 76.8 (Malipo ya awali kwa mkulima). hivyo mpaka sasa wakulima wanadai jumla ya shilingi bilioni 20.1

Hadi kufikia tarehe 04 Septemba, 2020 fedha zote za deni la wakulima zimepatikana, hivyo wakulima wote wanalipwa fedha zao, ndani ya siku tatu.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ameyasema hayo Leo tarehe 5 Septemba 2020 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera kuhusu hali ya malipo ya wakulima waliokuwa wanavidai vyama vikuu vya Ushirika KCU na KDCU vilivyokusanya kahawa yao.

“Kwa kumaliza deni hilo, kwa sasa vyama vinaendelea kukusanya kahawa kutoka kwa wakulima. Napenda tu kuwakikishia wakulima kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha kahawa yote inayokusanywa sasa na vyama vya ushirika malipo yanafanyika kwa wakati bila kucheleweshwa” Amekaririwa Waziri Hasunga

Katika Mkoa wa Kagera pekee, mfumo unaotumika ni tofauti na mikoa mingine kutokana na kwamba Vyama Vikuu vya Ushirika yaani KDCU na KCU vimeruhusiwa kukopa benki. Lengo ni kuhakikisha kwamba kahawa inapotoka kwenye AMCOS na kufika kwenye Vyama Vikuu (KDCU & KCU), vyama vikuu kwa kutumia fedha walizokopa waweze kuwalipa wakulima malipo ya awali, na pindi watakapouza kahawa ya wakulima kwa faida waweze kuwalipa malipo ya nyongeza.

Aidha, mategemeo ni kwamba fedha hizo ambazo vyama vikuu vinakopa kutoka kwenye mabenki vitakuwa vinazizungusha kwa kuwalipa wakulima na wakati huo huo vinauza kahawa waliyokusanya na kurudi kuendelea kuwalipa wakulima wanaoendelea kukusanya kahawa zao.

Waziri Hasunga amesema kuwa kilichotokea msimu huu wa ununuzi wa kahawa Mkoani Kagera ni kwamba, Vyama vikuu vilifanikiwa kupata mikopo benki ambapo KCU walikopeshwa na TADB shilingi bilioni 13 na KDCU walikopeshwa shilingi bilioni 17. Baada ya kupokea fedha hizo, vyama viliendelea na zoezi la kuwalipa wakulima.

Ameitaja Changamoto ambayo imejitokeza baada ya vyama vikuu kushindwa kuuza kahawa zilizokusanywa kutoka kwa wakulima kwa wakati na hivyo kupelekea wakulima wengi kutolipwa fedha zao. Hadi tarehe 02 Septemba, 2020 chama kikuu cha KCU kilikuwa kinadaiwa na wakulima shilingi bilioni 6.7 na KDCU ilikuwa inadaiwa shilingi bilioni 12.8.

Waziri Hasunga amesema kuwa suala la wakulima kupeleka kahawa zao kwenye vyama vikuu na wamekaa wanadai karibu Mwezi na zaidi, Serikali ikasema si sawa, haiwezekani. Nilipofika hapa Mkoani Kagera na kufanya kikao na KCU, niliwaagiza kuwa ndani ya siku tatu wawe wamekamilisha zoezi la kulipa deni lote la wakulima la shilingi bilioni 6.7 katika kutekeleza hili nimejulishwa kuwa tayari KCU wamepokea shilingi bilioni 2.09 kutoka kwa kitengo chao cha KCU Moshi Export na wanaendelea kuwalipa wakulima” Amesema Hasunga

Aidha, Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imekiongeza chama cha KCU mkopo wa shilingi bilioni 5 ambapo mpaka jana asubuhi walikuwa wameshapokea shilingi bilioni 2.4, na hivyo wakulima sasa wanaendelea kulipwa fedha zao ipasavyo.

Kwa upande wa KDCU ambao wao walikuwa wanadaiwa na wakulima shilingi bilioni 12.8, hadi kufikia jana tarehe 04 Septemba, 2020 walikuwa na fedha katika akaunti yao shilingi bilioni 1.7. Aidha, Serikali kupitia TADB imekiongeza chama cha KDCU mkopo wa shilingi bilioni 7, ambapo shilingi bilioni 1.2 zilishaingia tangu tarehe 31 Agosti, 2020; shilingi bilioni 5.8 iliyokuwa imebaki imeingia kwenye akaunti za KDCU jana asubuhi na tayari wakulima wanalipwa fedha zao kwa kasi kubwa.

Vilevile, Waziri Hasunga amesema kuwa siku ya jana tarehe 04 Septemba, 2020 KDCU wamepokea shilingi bilioni 3 ambazo walikuwa wanadai kwa wanunuzi wao wa kahawa. Hivyo, kwa sasa hali ya malipo ni shwari na wakulima wanaendelea kufurahia fedha zao.

KDCU pia wanatarajia kupokea kiasi cha shilingi bilioni 4.5 mnamo tarehe 09 Septemba, 2020 kutoka kwa wanunuzi wao ambapo Kampuni ya TOUTON italipa shilingi bilioni 3 na kampuni ya DRK italipa shilingi bilioni 1.3.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia amewashukuru na kuwapongeza wakulima wa kahawa mkoani humo kwa kufanya kazi kwa bidii na tija hivyo kuweka rekodi ya uzalishaji wa kahawa kwa wingi nchini.

Ametoa Mwito kwa wakulima kote nchini na wadau waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa zao la kahawa kuzingatia ubora ili kuendelea kupata masoko ndani na nje ya nchi.

Amewataka wakulima na wananchi kwa ujumla kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali ili kuendelea kutoa taarifa kuhusu watu wasiokuwa waaminifu wanaotorosha kahawa kwenda nje ya nchi.

MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com