Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Geita
Mhandisi Robert Gabriel mara baada ya uwekaji wa jiwe la msingi la
ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akicheza muziki na baadhi ya
viongozi wa Chato wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika Chuo cha
Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na wadau wa elimu(hawapo
pichani) waliohudhuria sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi
wa Chuo cha Ufundi Stadi Chato
…………..
Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia imetenga jumla ya Shilingi bilioni 10.7 kwa ajili ya ujenzi
wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato mkoani Geita.
Akizungumza wakati wa uwekaji wa
jiwe la msingi la ujenzi wa chuo hicho, Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema ujenzi wa chuo huo
unatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani.
“Nawapongeza viongozi wa
Halmashauri ya Chato kwa usimamizi mzuri kwani mpaka sasa mradi huu
umefikia asilimia 78 huku mkandarasi akiwa ameshalipwa asilimia 41 ya
pesa yote jambo linaloonyesha kwamba kuna fedha itabaki ambayo
itasaidia kuongeza majengo mengine,” amesema Waziri Ndalichako.
Aidha, Waziri Ndalichako
amewataka Wakandarasi na Washauri Elekezi wanaofanya kazi za Wizara ya
Elimu kuwa wazalendo na kuacha kuongeza gharama za miradi inayotekelezwa
na wizara hiyo.
“Tumegundua katika mikataba
mingi malipo ya washauri elekezi yanalipwa kulingana na kiwango
anacholipwa mkandarasi hivyo kufanya mkandarasi kuongeza gharama na
kutokukagua vizuri miradi hiyo,” ameelezea Profesa Ndalichako.
Waziri huyo amesema Wizara
inafanya mapitio hata kwa miradi iliyoishakamilika ili kujiridhisha na
gharama halisi za utekelezaji na kuwezesha kutoa fedha zinazolingana na
gharama na kuhakikisha miradi inakamika kwa viwango vinavyotakiwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Geita, Mhandisi Robert Gabriel amesema ujenzi wa chuo hicho cha kipekee
mkoani humo ni mwendelezo wa mageuzi makubwa yanayoshuhudiwa katika
sekta ya elimu kwa kipindi cha uongozi wa serikali ya Awamu ya Tano.
“Chuo cha VETA Chato kitakuwa
cha kwanza chenye ubora wa juu katika kanda ya ziwa kwa kuwa ni kikubwa
na kitakuwa na karakana zenye vifaa vya kisasa ambavyo vitawezesha
vijana wa Chato kuwa na ujuzi na maarifa,” amesisitiza Mhandisi Gabriel.
Aidha, Mbunge wa Chato ambaye
pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani ameishukuru serikaki
kwa kujenga chuo hicho na kuahidi kuhakikisha anahamasisha vijana wa
Chato kujiunga katika chuo hicho ili kupata ujuzi na maarifa ya
kuwawezesha kushiriki katika kukuza uchumi wa nchi kupitia viwanda.
Kalemani amemuomba mkandarasi wa
mradi huo kuongeza vijana wa Chato katika mradi huo ili uweze
kukamilika kwa wakati kama ilivyopangwa na hatimaye mafunzo yaanze
kutolewa Januari 2020.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt.
Pancras Bujulu amesema mradi wa ujenzi chuo hicho ni miongoni mwa miradi
40 ya ujenzi wa vyuo vipya vya ufundi stadi pamoja na upanuzi wa vyuo
vilivyopo lengo likiwa ni kutimiza azma ya serikali ya kuongeza
upatikanaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi na hatimaye kuongeza
udahili wa wanafunzi kutoka wanafunzi 200,000 ya mwaka 2016/17 hadi
700,000 ifikapo mwaka 2020.
“Mradi huu na mingine kama hii
inayotekelezwa nchini inachangia utekelezaji wa azma ya serikali ya
awamu ya tano ya kuhakikisha kuwa vijana wanapata ujuzi stahiki
utakaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri ili kushiriki kikamilifu katika
kukuza uchumi wa viwanda,” amesisitiza Bujulu.
Akitoa taarifa ya Mradi huo
Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya ziwa, Michael Ikongoli amesema mradi
huo unahusisha ujenzi wa majengo 27 ambayo ni pamoja na madarasa,
karakana, nyumba 4 za walimu, bwalo la chakula, jengo la utawala na
kwamba samani zote za Chuo hicho zitatengenezwa na Chuo cha VETA Mwanza
kwa gharama ya shilingi milioni 693.
0 comments:
Post a Comment