
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa
kijiji cha Sindeni katika eneo la Shamba la Miti la Korogwe lililopo
Handeni aliposikiliza malalamiko yao ya mpaka kati yao na Wakala wa
Huduma za Misitu Tanzania jana. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya
ya Handeni Godwin Gondwe.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza baada ya kukagua
ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Muheza unaofanywa na Shirika la
Nyumba la Taifa jana usiku akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya
ujenzi inayofanywa na Shirika hilo katika mkoa wa Tanga. Kulia kwa Naibu
Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mhandisi Mawanaasha Tumbo.
******************************
|
||||
|
Na Munir Shemweta, WANMM HANDENI
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewatuliza wananchi wa
kijiji cha Sindeni kilichopo Tarafa ya Sindeni wilayani Handeni mkoani
Tanga kufuatia mgogoro kati yao na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS)
kuhusu mpaka baina ya kijiji cha Sindeni na Shamba la Miti la Korogwe.
Dkt Mabula aliwatuliza
wananchi hao baada ya kufika katika shamba la Miti la Korogwe lililopo
wilayani Handeni kukagua maendeleo ya Ujenzi wa ofisi na Nyumba za
Watumishi za TFS zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) akiwa
katika ziara yake ya siku mbili katika mkoa wa Tanga.
Dkt Mabula ametaka idara ya
ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Handeni ikisimamiwa na Ofisi ya
Ardhi Kanda ya Kaskazini kuhakikisha inafanya uhakiki wa mpaka kati ya
TFS na kijiji cha Sindeni na kuweka alama ili kukomesha mgogoro huo
unaozuka mara kwa mara.
‘Kitakachofanyika ni uhakiki
wa mipaka ya kijiji chenu kinaishia wapi, TFS wanaishia wapi, NARCO
wanaishia wapi, tutaheshimu mipaka na nyaraka zilizoanzisha vijiji
vyenu’’ alisema dkt Mabula.
Uamuzi wa Dkt Mabula kutoa
maagizo hayo unafuatia wananchi wa kijiji hicho kulalamika mbele ya
Naibu Waziri kuwa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) uliongeza eneo
inalomiliki katika shamba hilo kwa kuingia ndani ya eneo la kijiji cha
Sindeni jambo linalochochea mgogoro kati ya pande hizo.
Ally Mhina mkazi wa kijiji cha
Sindeni alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi kuwa, TFS iliacha eneo lake la
asili na kuongeza eneo lingine kuingia kijiji cha Sindeni wilaya ya
Handeni mkoani Tanga.
Kwa upande wake Meneja wa
Shamba la Miti la Korogwe Pregreen Mushi alisema, wenyeji wa Sindeni
walivamia eneo la Wakala wa Huduma za Misitu huku wale wa Kwamatuko na
Kwaingoma wakiuza maeneo ya hifadhi kwa jamii ya wafugaji na Mkuu wa
Wilaya ya Handeni alishatoa agizo wote waliovamia kuondoka eneo la
hifadhi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni
Godwin Gondwe alisema alishashughulikia mgogoro huo na kuwataka
wasioridhika wasioridhika na utatuzi wake kwenda mahakamani na kufafanua
kuwa katika jitihada zake za kutafuta suluhu ya mgogoro huo baadhi ya
wananchi walikubali kuwepo msitu huo na sasa wananufaika kwa kupatiwa
huduma mbalimbali ikiwemo ujenzi wa shule.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri
ya Wilaya ya Handeni Mustafa Beleko alisema pamoja maagizo ya Naibu
Waziri kuhusiana na uhakiki wa mpaka kati ya kijiji cha Sindeni na TFS
lakini wao kama halmashauri watachukua ramani ya kijiji wakati wa
uhakiki mipaka ili kukomesha kuibuka kwa mgogoro huo mara kwa mara.
Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliagiza pia kuweka alama za mpaka kati ya
Wakala wa Huduma za Misitu na NARCO kufuatia suluhu ya mpaka kati ya
taasisi hizo mbili za serikali kushindikana kutekelezwa kwa madai kuwa
NARCO ilikaa kimya katika utekelezaji makubaliano ya kuchangia gharama
za ubainishaji mipaka.
0 comments:
Post a Comment