METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, November 10, 2019

WIZARA YA UVUVI KUJA NA SHERIA MPYA YA UKUZAJI VIUMBE MAJI

Katibu Mkuu wa Uvuvi Dk.Rashid Tamatamah, kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.akizungumza wakati alipokuwa akifungua warsha ya kuimarisha kilimo na biashara ya mwani kwa wadau mbalimbali ikiwemo wabunge na makampuni yanayojishughulisha na zao hilo, iliyofanyika jijini Dodoma.
Meneja wa kampuni ya Mwani Mariculture Ltd, Hamil Said Soud,akitoa taarifa wakati wa ufunguzi wa warsha ya kuimarisha kilimo na biashara ya mwani kwa wadau mbalimbali ikiwemo wabunge na makampuni yanayojishughulisha na zao hilo, iliyofanyika jijini Dodoma.
Sehemu washiriki  wakifatilia warsha ya kuimarisha kilimo na biashara ya mwani kwa wadau mbalimbali ikiwemo wabunge na makampuni yanayojishughulisha na zao hilo, iliyofanyika jijini Dodoma.
……………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imesema ipo kwenye mchakato wa kuanzisha sheria mpya ya ukuzaji viumbe maji(Aquaculture Act) ambapo pamoja na mambo mengine kutakuwa na vipengele vinavyoratibu shughuli za uzalishaji na biashara ya zao la mwani.

Aidha, imewataka wadau wa zao la mwani kuhakikisha biashara ya zao hilo inafanyika kwa amani na uaminifu kwa kufuata sheria zilizopo ili iwe na tija kwa kila mmoja.

Hayo yameelezwa leo na Katibu Mkuu wa Uvuvi Dk.Rashid Tamatamah alipokuwa akifungua warsha ya kuimarisha kilimo na biashara ya mwani kwa wadau mbalimbali ikiwemo wabunge na makampuni yanayojishughulisha na zao hilo, iliyofanyika jijini Dodoma.

Amesema awali mafanikio makubwa ya zao hilo yalipatikana kwa haraka na kuipaisha Tanzania hususan Zanzibar kama mzalishaji mkuu wa zao hilo duniani ikifuatiwa na ufilipino.

“Mpaka kufikia mwaka 2006 walikuwepo wakulipa zaidi ya 300 Tanzania bara na zaidi ya 20,000 kwa Zanzibar, wengi wao wakiwa ni wanawake.Lakini kutokana na changamoto mbalimbali miaka ya hivi karibuni uzalishaji umeshuka na Tanzania sasa ni ya tatu baada ya Ufilipino na Indonesia,”amesema.

Ametolea mfano kwa upande wa Tanzania bara uzalishaji ulishuka hadi tani 918 katika mwaka 2018/19 ikilinganishwa na tani 1,329.5 mwaka 2017/18 na tani 1,197.5 mwaka 2016/17 au tani 1,500 zilizovunwa mwaka 2004/5.

“Upungufu katika uzalishaji uliojitokeza umesababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo mabadiliko ya hali ya hewa, ukosefu wa mitaji na wawekezaji makini, ununuzi wa mwani usiofuata taratibu na kutokuwa na soko la ndani,”amesema.

Kufuatia hali hiyo, Katibu huyo amesema serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kufanya tafiti zinazolenga kupunguza changamoto na kuwajengea uwezo wakulima ikiwa ni pamoja na fursa za mikopo na kuongeza kasi katika kutafuta masoko mapya.

Pia amesema kuanzishwa kwa Dawati la Sekta binafsi Wizarani mwaka 2018 kumesaidia kwa kiasi kikubwa kuziunganisha taasisi za fedha na wakulima na wafugaji kwenye tasnia ya ukuzaji viumbe maji kwa ajili ya upatikanaji wa mikopo na mitaji.

“Lakini pia tafiti zinazofanywa na taasisi yetu ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania(TAFIRI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam zimesaidia wakulima jinsi ya kukabiliana na kupunguza athari ya mabadiliko ya tabia nchi na kusaidia kuongeza uzalishaji wa zao la mwani,”amesema.

 Kwa upande wake, Meneja wa kampuni ya Mwani Mariculture Ltd, Hamil Said Soud, amesema masuala ya masoko ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili.

“Wawekezaji wawekewe mazingira wezeshi kwa kuwa uzalishaji unashuka, tunatakiwa kujiuliza ni kitu gani kinachoshusha uzalishaji? Tunatakiwa kuhakikisha wawekezaji wanapokuja wawekewe mazingira wezeshi kwa kuwa kuna nchi kama Kenya zimeanza uzalishaji baada ya sisi lakini zinakuja kwa kasi sisi uzalishaji unashuka,”amesema.

Naye, Mbunge wa Mchinga(CUF), Hamidu Bobali amesema changamoto kubwa wakulima wanakabiliwa na shida ya kamba ambapo kamba moja inauzwa Sh.10,000.

“Wawekezaji wanatakiwa kuhakikisha bei ya kamba inashuka inakuwa ya wastani na wahakikishe wakulima wanakuwa na kamba, kilimo hichi kinafanywa na watu wenye vipato vya chini hasa kina mama, pia wawekezaji wasaidie kuwepo na maeneo ya kuanikia mwani,”amesema.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com