Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikata utepe kuashiria ufunguzi wa
ofisi mpya ya Uthibiti Ubora wa Shule ya Halmashauri ya Wilaya ya
Misungwi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Juma
Sweda (mwenye suti ya bluu) wakikagua ofisi mpya ya Uthibiti Ubora wa
Shule ya wilaya hiyo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akifurahi kwa kucheza kwaya na
baadhi ya viongozi wa wilaya ya Misunhwi mara baada ya kufungua ofisi
mpya za Uthibiti Ubora wa Shule ya Wilaya Misungwi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknojia Profesa Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na
wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi wilayani Misungwi.
Muonekana wa Ofisi mpya za uthibiti ubora wa shule ya Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi
……………….
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amefungua majengo ya ofisi mpya za
Uthibiti Ubora wa Shule za Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi na
Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Akizungumza baada ya ufunguzi wa
ofisi hizo Waziri Ndalichako amewataka wathibiti Ubora wa Wilaya kufanya
kazi kwa bidii na weledi na waone kuwa uwepo wa ofisi hizo uwe chachu
ya kuendelea kutoa taarifa za ukaguzi wa shule zenye ubora na kwa
wakati. Ndalichako amewataka kuhakikisha kuwa changamoto zinazoainishwa
katika kaguzi zao zinafanyiwa kazi ili kuinua ubora wa elimu hususan
katika taaluma na sekta ya elimu kwa ujumla katika wilaya hizo.
“Tumieni ofisi hizi kuwa chachu ya
kuwawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na kutoa taarifa za changamoto
zinazozikabili shule pamoja na sekta nzima ya elimu ili ziweze kufanyiwa
kazi kwa haraka,” amesema Profesa Ndalichako.
Prof. Ndalichako amesema serikali
itahakikisha changamoto zote zinazowakabili wathibiti ubora wa shule
nchini zinafanyiwa kazi kwa dhati ili kuzipunguza ama kuzimaliza kabisa
ikiwemo ukosefu wa ofisi na vitendea kazi.
Akizungumzia uboreshaji na ujenzi
wa miundombinu ya sekta ya elimu unaoendelea nchini, Profesa Ndalichako
amesema suala hilo ni endelevu na litakuwa likifanyiwa kazi muda wote
ili kuwezesha utoaji wa elimu bora kwa watoto wa Kitanzania.
Aidha, Waziri Ndalichako amewataka
wathibiti ubora wa shule kwa kushirikiana na Maafisa Elimu kufanya
tathimini za kina kila mara ili kubaini sababu halisi za mdondoko wa
wanafunzi wote wa kike na kiume.
“Tumeona hapa Misungwi takwimu
zinaonyesha mdondoko mkubwa zaidi upo kwa upande wa watoto, hivyo
fanyeni tathimini ili tujue sababu na kuacha kuegemea upande mmoja wa
mtoti wa kike na kwamba sababu ni mimba” amesema Profesa Ndalichako
Mkuu wa wilaya ya Misungwi, Juma Sweda ameishukuru serikali
kwa kuhakikisha wathibiti ubora wa shule wanapata ofisi za kisasa na
vitendea kazi na kuhaidi kuwa wilaya ya Misungwi itaendelea kusimamia
ubora wa elimu na kuongeza ufaulu katika ngazi zote.
“Sisi tutaendelea kusimamia utoaji
wa elimu bora kwa watoto wote wa hapa Misungwi pamoja na kupunguza
mdondoko wa wanafunzi kwa kuanzisha mpango wa kutoa chakula shuleni”
amesitiza Mkuu wa Wilaya.
Naye Mthibiti Mkuu wa Wilaya hiyo,
Faustine Sahala ameishukuru serikali kwa kuona changamoto zilizokuwa
zikiwakabili za ukosefu ofisi ambapo walipatiwa zaidi ya shilingi
milioni 152 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hizo.
Sahala amesema ujenzi wa ofisi hiyo umekamilika kwa asilimia 100
pamoja na ununuzi wa vitendea kazi ikiwemo mashine ya kurudufu
(photocopy), ufungaji mtandao wa internet, uwekaji samani, camera za
ulinzi (CCTV) na ujenzi wa vyoo vya nje.
Katika Mpango huu Serikali inajenga ofisi 100 za Wadhibiti Ubora wa shule katika Halmashauri 100 kwa shilingi bilioni 15.2
0 comments:
Post a Comment