Na Lucas Mboje, Dar es Salaam
KAMISHNA Jenerali wa Magereza nchini,
Dkt. Juma Malewa(pichani) ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya
Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanikisha mchakato wa ununuzi wa
magari 450 ya Jeshi hilo ambayo yanatarajiwa kupokelewa muda wowote
kuanzia sasa.
Kamishna Jenereli Malewa ameyasema hayo
leo katika ufunguzi rasmi wa mkutano wa wakuu wa magereza yote Tanzania
Bara unaofanyika kwa siku moja katika Bwalo kuu la Maafisa magereza,
ukonga jijini Dar es Salaam.
Jenerali Malewa amesema kuwa upatikanaji
wa magari hayo utapunguza tatizo kubwa la uhaba wa magari kwa ajili ya
shughuli za uendeshaji na utawala pamoja uboreshaji wa utekelezaji wa
majukumu ya Jeshi hilo.
“Nichukue nafasi hii kumshukuru kwa
dhati Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na serikali yote kwa
ujumla kwa namna inavyoshughulikia utafutaji wa ufumbuzi wa changamoto
tulizonazo,” alisema Jenerali Malewa.
Aidha kuhusu madeni ya Watumishi wa
Jeshi hilo na wazabuni, Kamishna Jenerali Malewa amesema serikali imetoa
kiasi cha zaidi ya Bilioni 8 za pesa ya kitanzania kwa ajili ya kulipa
madeni hayo ambapo madeni yote yaliyokwisha kuhakikiwa tayari yameanza
kulipwa na wahusika wamekwishaanza kupata fedha wanazodai Jeshi hilo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya
Ndani, Mhe. Mhandisi Hamad Yusuph Masauni akizunguza katika ufunguzi wa
Mkutano huo ametoa rai kwa jeshi hilo kutumia vyema fursa zilizopo
katika katika maeneo mbalimbali ya jeshi hilo kwa kuanzisha na
kuimarisha viwanda vidovidogo vilivyopo ili kuongeza uzalishaji hivyo
kuchangia pato la taifa.
Masauni amesema kuwa Jeshi la Magereza
linazo fursa nyingi sana za uzalishaji yakiwemo maeneo makubwa yanayofaa
kwa kilimo, miradi ya ufugaji na miradi mengineyo ya kiuchumi.
“Nisisitiza kwamba wekeni mikakati yenye
lengo la kuongeza uzalishaji katika maeneo yenu kwani nataka kila mmoja
wenu katika gereza alilopo aweke malengo ya kuongeza uzalishaji
kulingana na fursa zilizopo,” alisema Mhe. Masauni.
Mkutano huu wa Wakuu wa Magereza yote
Tanzania Bara unajumuisha Maafisa Waandamizi kutoka Makao Makuu ya
Magereza na Wakuu wa vituo vya Magereza yote nchini ambapo lengo kuu ni
kujadiliana kwa kina hali halisi ya utendaji kazi magerezani na kuweka
mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizopo ili kuongeza tija na
ufanisi. Kauli mbiu ya mkutano huo ni JESHI LA MAGEREZA KATIKA JITIHADA
ZA KUFANIKISHA KUELEKEA TANZANIA YA UCHUMI WA VIWANDA.
0 comments:
Post a Comment