Mlezi wa Kikundi cha Wake wa
Viongozi cha New Millenium Women Group, Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary
Majaliwa akisoma hotuba yake wakati kikundi hicho kilipokabidhi majengo
ya madarasa manne na vyoo kumi kwa Kituo cha waotot wenye ulemavu cha
Buhangija wilayani Shinyanga Novemba 10, 2019. Kushoto ni Mgeni rasmi
katika makabidhino hayo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia,
Profesa Joyce Ndalichako na kulia ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta
Mboneko.
…………….
MKE wa Waziri Mkuu Mama Mary
Majaliwa ametoa wito kwa wazazi na walezi watoto wenye mahitaji maalumu
kutowaficha na kuwatelekeza na badala yake wawape nafasi ya kupata
elimu kwa sababu ni haki yao ya msingi.
Mama Majaliwa ambaye pia ni
Mlezi wa Umoja wa Wake wa Viongozi (New Mellenium Women Group), ametoa
wito huo leo (Jumapili, Novemba 10, 2019), wakati alipokabidhi majengo
ya madarasa manne na matundu ya vyoo kumi kwa Kituo cha Watoto Wenye
Ulemavu cha Buhangija mkoani Shinyanga yaliyojengwa na umoja huo.
Mama Majaliwa amesema si vyema
kuwatenga au kuwakatia tamaa watoto wenye ulemavu kwani wao pia ni
watoto sawa na watoto wengine, hivyo wanastahili kupewa haki zote bila
kubaguliwa.
Amesema hatua waliyochukuwa
akinamama wa umoja huo inaunga mkono jitihada za serikali ya Awamu ya
Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kuwapatia watoto
wa kitanzanai elimu bure na katika mzingira mazuri.
Mgeni rasmi katika
makabidhiano hayo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa,
Joyce Ndalichako ameupongeza umoja huo kwa shughuli mbalimbali za
kijamii ikiwemo kuwajali watoto wenye mahitaji maalumu.
Profesa Ndalichako amesema
katika kipindi cha mwaka 2019/2020 Serikali imetenga jumla ya sh
3,809,758,460.00 kwa ajili ya kununua na kusambaza vifaa vya
kufundishia na kujifunzia pamoja na vifaa visaidizi kwa ajili ya
wanafunzi wenye mahitaji maalum (wakiwemo Albino), katika shule
na vitengo vya elimu maalum.
Waziri huyo ameongeza kuwa
pamoja na juhudi hizo za Serikali, bado wanafurahi wanapopata
michango kama huo uliotolewa leo. “Wito wangu kwenu tusichoke
kuwasaidia hawa watoto wetu. Napenda kuwakumbusha na kusisitiza
kwamba Watu wenye Ulemavu wanahitaji msaada mkubwa kutoka kwenu.”
“Tuwasaidie na tushirikiane
kuwapatia mahitaji yao muhimu ikiwa ni pamoja na elimu, huduma
za afya na mazingira mazuri ya kuwawezesha kuishi bila ya
matatizo. Serikali kwa upande wake itaendelea kujitahidi kwa uwezo
kutoa fursa zinazojali mahitaji yao.”
Amesema madarasa pamoja na
vyoo alivyokabidhiwa leo kwa niaba ya uongozi wa kituo cha Buhangija
na Kikundi cha New Millenium ni tunu kwao na wananchi wa
Shinyanga na ni sadaka kwa watoto wa Buhangija, hivyo, ameutaka
uongozi wa Mkoa na Uongozi wa Kituo kwa pamoja washirikiane
kuyatunza vizuri ili yaweze kutumika kwa muda mrefu.
Akitoa taarifa ya ujenzi huo
kwa mgeni rasmi, Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela
amesema fedha zilizotumika kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne ni sh.
65m,884,523/= ambapo kila chumba cha darasa kimejengwa kwa wastani wa
sh. 16,471,130.
Amesema ujenzi wa vyumba kumi
vya vyoo unaendelea na ukikamilika utagharimu sh.26, 271,922.44 na
kwamba vyoo hivyo vitakuwa vya kisasa vikiwa na maji ndani pamoja na
masinki ya kunawia ili kukidhi mahitaji ya watoto wenye ulemavu.
0 comments:
Post a Comment