METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, October 21, 2019

WAZIRI HASUNGA NA MPANGO WA KUENDELEZA SEKTA YA KILIMO AWAMU YA PILI (ASDP II)

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb)

Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo, Kilimanjaro

SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ambayo ni utekelezaji wa Mpango wa Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo Nchini (TASFIP) unaolenga kukuza kilimo kwa asilimia 6 kwa mwaka.

Kwa kuzingatia hatua hizo, Wizara ya Kilimo imekusudia kuleta mageuzi ya kilimo kutoka mtazamo uliopo wa kilimo cha kujikimu hadi kufikia uendeshaji wa kilimo kwa mfumo wa kibiashara.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo Tarehe 21 Octoba 2019 wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa Programu ya kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani pamoja na uzalishaji bora wa mazao ya viungo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hotel ya Uhuru Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.

Mhe Hasunga ameyataja maeneo ambayo yanahitaji utekelezaji wa haraka. Mosi, Utekelezaji wa adhma ya serikali kuendeleza kilimo kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kwa kusimamia thabiti nguzo ya programu hiyo ikiwemo Usimamizi endelevu wa matumizi ya maji na ardhi.

Alisema kuwa Lengo la ASDP II ni kuleta mageuzi katika  Sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji na tija, kilimo cha kibiashara, kuongeza pato kwa wakulima hivyo nilazima kuwekwa mkakati madhubuti wa utekelezaji ili kufikia nalengo yaliyokusudiwa.

Vilevile, alisema kuwa serikali imekusudia Kuboresha mazingira wezeshi, uratibu, ufatiliaji na tathmini katika sekta ya kilimo hivyo wataalamu katika Wizara ya kilimo wanapaswa kuongeza kasi ya uwajibikaji ili kutimizi adhma hiyo.

Alisema Wizara ya kilimo itaweka mkakati madhubuti wa kuhakikisha kuwa bei ya Mazao inaimarika huku akisisitiza kuwa kwa ushirikiano na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji atahakikisha wakulima wanapata masoko ya mazao yao.

Amesema kuwa Wizara ya Kilimo imetayarisha Mkakati wa Taifa wa miaka 10 wa Usimamizi wa Mazao baada ya kuvunwa.

Alisema kuwa mkakati huo umeandaliwa ili kuendana na malengo endelevu ya Dunia ya kutokomeza njaa ifikapo 2030, kuhakikisha usalama wa chakula na lishe na kukuza kilimo endelevu kama lengo la pili la Umoja wa Mataifa kati ya Malengo 17.

Mkakati huo utakuwa Mwongozo kwa Sekta za Umma na Binafsi katika kukabiliana na changamoto ya upotevu wa Mazao baada ya mavuno. Aidha, Mkakati huo umezingatia mabadiliko yanayoendelea ya Kitaasisi na Kisera.


MWISHO.
Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2025 WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com