Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lenye
dhamana ya kuratibu ukuzaji na uendelezaji wa sekta ya Sanaa nchini
litatoa tuzo kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini waliofanya
vizuri kitaifa katika masomo ya Sanaa za Muziki, Ufundi na Maonyesho
kwenye matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne uliofanyika mwezi
Oktoba,2016 na matokeo yake kutoka hivi karibuni. Aidha, sambamba na
kutunuku vyeti na Zawadi za fedha taslimu kwa wanafunzi hao BASATA
litatambua mchango wa walimu wa masomo husika na shule zilizofanya
vizuri katika mchepuo wa Sanaa.
Hafla hiyo ambayo itawakutanisha
wanafunzi hao, walimu wao pamoja na wadau mbalimbali wa Sanaa itafanyika
siku ya Jumatatu tarehe 27/03/2017 saa 4:00 asubuhi katika Ukumbi wa
BASATA ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.
Ili kutambua,kuibua na kukuza vipaji vya
Sanaa kutoka ngazi za chini na kuamsha ari ya masomo ya mchepuo wa
Sanaa katika mitaala yetu ya elimu sambamba na kujenga weledi katika
tasnia ya Sanaa kwa ujumla wake Baraza limeamua kurejesha programu hii
ya utoaji wa tuzo kwa wanafunzi wa shule za sekondari kila mwaka ambao
wanashika nafasi za juu kitaifa katika masomo ya sanaa husasan Sanaa za
Ufundi, Maonyesho na Muziki
Itakumbukwa kuwa BASATA limekuwa na
mwendelezo wa programu mbalimbali za Sanaa kwa watoto zilizoanza tangu
miaka ya 1980 ambazo zimepata kuibua na kukuza vipaji vya wasanii.
BASATA linachukua fursa hii kuwaalika wananchi na wadau wote wa sanaa
kufika kwa wingi kushuhudia utoaji wa tuzo hizi.
Sanaa ni kazi, tuipende, tuikuze na kuithamini
Godfrey Mngereza, Katibu MTENDAJI. 23 MACHI, 2017
0 comments:
Post a Comment