WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka
Watanzania wanaoishi nje ya nchi wazingatie sheria za Taifa husika na
kamwe wasijihusishe na biashara haramu ya dawa za kulevya.
“Vita ya dawa za kulevya ni kubwa, hata
hivyo Serikali tunaendelea kupambana nayo. Nchi ilikuwa inapoteza vijana
ambao walikuwa wamejiingiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya.
Nawaomba msithubutu kuingia huko mtafungwa,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Jumatano, Machi 22, 2017) wakati akizungumza na Umoja wa Watanzania
wanaoishi nchini Mauritius katika mkutano alioutisha kwenye hoteli ya
Meridien mjini Port Louis.
Amesema katika kudhibiti biashara hiyo
haramu ya dawa za kulevya Serikali iliamua kuunda Mamlaka ya Kuzuia na
Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na inafanya kazi vizuri. “Na
tutakamata kila mtu anayejihusisha na biashara hiyo bila kujali cheo,
uwezo na mamlaka aliyonayo,”.
Amesema mamlaka hiyo inafanyakazi ya
kutafuta wazalishaji, watumiaji na wafanyabiashara, lengo likiwa ni
kuokoa vijana ambao wameshindwa kutimiza ndoto zao kutokana na madhara
waliyoyapata baada ya kutumia dawa za kulevya.
Katika hatua nyinngine, Waziri Mkuu
amewataka Watanzania hao walioko nchini Mauritius kujenga mshikamano wa
pamoja na wawe na uzalendo na nchi yao. Pia wawe mabalozi wazuri wa
kutangaza vivutio vya Taifa.
Amesema ni vema wakatumia fursa
walizonazo katika kutafuta wawekezaji na kuwashawishi waje nchini na
kuwekeza kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda, uvuvi, nishati na
utalii.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na
Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed
amewaomba Watanzania hao wazidishe mshikamano miongoni mwao kwa kuwa
umoja wao ndiyo nguzo yao.
“Mko hapa kwa ajili ya kutafuta elimu na
wengine mnafanya kazi, shughuli ambazo zitawasaidia kuboresha
maendeleo yenu na Taifa kwa ujumla, hivyo nawaomba mzingatie
kilichowaleta,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa muda wa Umoja wa
Watanzania waishio nchini Mauritius, Bw. Donald Kongwa ambaye ni Ofisa
wa benki ya Standard Chaetered nchini Mauritius amemuhakikishia Waziri
Mkuu kwamba kipato wanachokipata watakitumia kwa kuwekeza Tanzania kwa
lengo la kukuza uchumi wa Taifa.
Aidha, amesema wanaunga mkono na
kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika
kujenga uchumi wa viwanda, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, ujenzi
wa miundombinu ya kisasa, ununuzi wa ndege pamoja na kuimarisha
uwajibikaji na nidhamu kwa watumishi wa umma.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, MACHI 22, 2017.
0 comments:
Post a Comment