Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa
akizungumza wakati wa makabidhiano ya ujenzi wa mradi wa maji wa
Shilima, Wilaya ya Kwimba, Mkoani Mwanza. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi
Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Anthony Sanga.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi
MWAUWASA, Christopher Gachuma akizungumza wakati wa hafla ya
makabidhiano ya mradi wa Maji wa Shilima. Kushoto kwake ni Mbunge wa
Kwimba, Shanif Mansoor, Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa na Mkuu
wa Wilaya ya Kwimba, Senyi Ngaga
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa
(katikati) akichimba mtaro kwa ajili ya ulazaji wa bomba za maji
kuashiria kuanza rasmi kwa utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa maji wa
Shilima, Wilayani Kwimba ambao ulisimama kutokana na Mkandarasi
kushindwa kuutekeleza kwa wakati na hivyo ujenzi wake kukabidhiwa kwa
MWAUWASA.
Uchimbaji wa mtaro ukiendelea kwa ajili
ya kulaza bomba za maji mradi wa Shilima mara baada ya ujenzi wa mradi
huo kukabidhiwa kwa Mamlaka ya Maji Mwanza (MWAUWASA).
Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi
Anthony Sanga akizungumza mara baada ya kukabidhiwa ujenzi wa mradi wa
maji wa Shilima.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Shilima
na vijiji vya jirani waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya ujenzi wa
mradi wa maji wakimsikiliza Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa
(hayupo pichani).
…………………..
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa
amekabidhi ujenzi wa mradi wa maji wa Shilima Wilayani Kwimba kwa
Mamlaka ya Maji Mwanza (MWAUWASA) baada ya Mkandarasi Kampuni ya Palemon
Construction Ltd ya Mwanza kushindwa kukamilisha kwa wakati.
Makabidhiano hayo yalifanyika hivi
karibuni katika Kijiji cha Shilima na kushuhudiwa na watendaji
mbalimbali wa Serikali na mamia ya wananchi wa Shilima na maeneo ya
vijiji vya jirani.
Akizungumza kabla ya kukabidhi mradi,
Waziri Mbarawa alieleza kwamba ujenzi wake ulianza tangu mwaka 2013 na
kwamba ulipaswa kukamilika ndani ya miezi sita lakini hadi sasa mradi
huo haujakamilika.
Alisema Serikali iliamua kusitisha
mkataba na Mkandarasi ambaye alishindwa kutekeleza ujenzi wa mradi kama
ilivyo kwenye makubaliano.
Mara baada ya kuukabidhi mradi huo,
Profesa Mbarawa aliiagiza MWAUWASA kufanya kazi usiku na mchana ili
kuhakikisha ujenzi unakamilika ndani ya Siku 60 ili kuwaondolea mateso
ya muda mrefu wanachi wa maeneo hayo hasa ikizingatiwa kwamba mradi
ulipaswa kukamilika tangu mwaka 2013.
“Tunataka wataalam hawa wafanye kazi
usiku na mchana na baada ya miezi miwili wananchi wapate maji safi na
salama, uwezo tunao, tunaweza kumaliza tatizo la maji hapa kwa muda
mfupi sana,” alisema Profesa Mbarawa.
Aliongeza kuwa kuna miradi ipatayo 88
kote nchini ambayo ujenzi wake ulianza kati ya Mwaka 2010 hadi 2015
ambayo ilipaswa kuwa imekwisha kamilika lakini hadi hivi sasa bado
inasuasua na huku akiutolea mfano mradi huo wa Shilima.
Alibainisha kwamba Serikali kupitia
Wizara ya Maji imeamua kuwa na utaratibu mpya wa kuzikabidhi Mamlaka za
Maji miradi ambayo ujenzi wake una changamoto inayosababisha isikamilike
kwa wakati.
“Tumeamua kubadilisha utendaji wa Sekta
ya Maji, kila mahala tatizo ni maji, hili halikubaliki, tumejipanga na
tunadhamira ya dhati kuhakikisha kero hii inakuwa historia kote nchini,”
alisema Waziri Mbarawa.
Kuhusu utaratibu huo mpya, Profesa
Mbarawa alibainisha kuwa ni wa nchi nzima na kwamba wakandarasi
wanaoshindwa kutekeleza miradi waliyokabidhiwa kwa wakati hawatovumiliwa
na watanyanganywa na itakabidhiwa kwa Mamlaka za maji kwenye maeneo
husika.
“Tumeamua miradi yote yenye changamoto
tutaisimamia wenyewe na tutahakikisha inafanya kazi. Wananchi wamechoka
kuendelea kuisubiri miradi hii ikamilke, fedha nyingi zinapotea,
Serikali haitokubaliana na Mkandarasi anaechelewesha ujenzi wa mradi
tayari tumefanya hivi Rungwe na sasa tumefanya hapa Shilima,” alisema
Profesa Mbarawa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa
MWAUWASA, Mhandisi Anthony Sanga alisema wamepokea agizo hilo la
kutekeleza mradi huo ambao umesuasua kwa kipindi kirefu na kwamba
wataukamilisha kwa wakati kama ilivyoagizwa.
“Tunaahidi hadi kufikia Septemba 3, 2019
tutakuwa tumeukamilisha mradi kwani itakuwa tayari ni Siku 60 na
wananchi wataanza kupata majisafi na salama kutoka Ziwa Victoria,”
alisema Mhandisi Sanga.
Aidha, kwa mujibu wa Mhandisi wa Maji,
Wakala wa Maji Vijijini Wilaya ya Kwimba, Mhandisi Boaz Pius ni kwamba
mradi huo utakapokamilika utahudumia wakazi 16,675 kutoka vijiji vinne
ambavyo ni Shilima chenye wakazi 7,526, Mhande chenye wakazi 1,967,
Kasang’wa wakazi 2,730 na Kijiji cha Izizimba “A” chenye wakazi wapatao
4,452.
Mhandisi Boas aliongeza kwamba kukamilika
kwa mradi huo pia kutaweza kuhudumia vijiji vya Sangu, Gurumwa,
Mwalubungwe na Kikubiji, ambapo bomba kuu linapita.
0 comments:
Post a Comment