Na.Mwandishi Wetu-DSM
Vijana wapewa elimu kuhusu
kuanzisha biashara ili kujikwamua na uchumi kwa kuchangamkia fursa
zilizoko kwenye maeneo yao na kujua umuhimu wa kodi katika biashara ili
kuwezesha taifa kupata mapato na wao kupata faida.
Akizungumza katika Semina ya
Vijana iliyoandaliwa na Umoja wa Vijana Tanzania (TYVA), Afisa Elimu na
Huduma kwa Walipa Kodi kutoka TRA, Isihaka Sharifu alisema kuwa Serikali
imerekebisha baadhi ya Sheria za kodi hususani kwa vijana wanaofungua
kampuni au biashara mpya.
Sharifu alisema kuwa kwa sasa
Sheria ya kodi imejikita kuwasaidia vijana wanaoanzisha kampuni na
biashara mpya kwani imeweza kugusa msamaha wa kodi kwa miezi sita
tofauti na awali ambapo biashara mpya zilikuwa zinalipiwa kodi baada ya
miezi mitatu.
“ Kwa sasa Sheria inasema ukiwa
unafungua biashara yako au kampuni mpya kwa sasa unatakiwa kulipa kodi
baada ya miezi sita, kwa hiyo hii itawasaidia vijana wengi ambao wanania
ya kuanzisha biashara, nawasihi vijana wenzangu tumieni Fursa hiyo
kujikwamua kiuchumi”, Alisema Sharifu.
Katika Semina hiyo ambayo kauli
mbiu yake ilikuwa ‘Nguvu ya Kodi’ Sharifu alipaeleza kuwa TRA
inatekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kuwakwamua vijana
hasa wajasiriamali wadogo ambao wanafanya biashara zao kwenye maeneo
mbalimbali hapa nchini.
Alisema kuwa kodi inayotozwa kwa
wafanya biashara wenye mauzo kuanzia milioni 0 hadi 100 imegawanyika
katika makundi manne ambayo ni mauzo kuanzia 0 mpaka milioni 4 ambao
hawatozwi kodi, mauzo ya milioni 4 mpaka 7.5 wanatozwa 100,000, milioni 7
mpaka 11 wanatozwa 250,000 na milioni 11 mpaka 14 wanatozwa 450,000
tofauti na hapo zamani ambapo walikuwa wanatozwa 546,000, kwa hiyo
vijana wanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo.
Kwa upande wake, Afisa Vijana
kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Anna Marika alisema kuwa vijana
wanatakiwa kuwa wazalendo kwa kutimiza wajibu wao kwenye suala la kulipa
kodi kama Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli anavyoagiza.
“Nimefurahi kwa Semina hii kwani
watoa mada wamekuja na Mada nzuri zinazoelimisha ulipaji Kodi, wito
wangu kwa vijana ni kwamba wanatakiwa kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi
kama Rais alivyoagiza kuchukua vitambulisho ili wasipate shida kwenye
maeneo yao ya kufanyia Biashara”, Alisema Marika.
Marika aliongeza kuwa kwa Wilaya
ya Temeke wamejikita zaidi katika kuwasaidia vijana, wanawake na
walemavu kujikwamua kimaisha kama Ofisi ya Rais –TAMISEMI ilivyoagiza
kuwa asilimia 10 ya mapato ya halmashauri ijikite kwenye kuwasaidia
vijana, wanawake na walemavu.
Alisema Wilaya ya Temeke imetanga
asilimia nne kwa vijana, asilimia nne kwa wanawake na asilimia mbili kwa
walemavu, huku wakilenga kuboresha utoaji wa huduma kwa kutoa vifaa vya
kazi kwa vikundi mbalimbali kama vile pikipiki, Chelehani,vifaa vya
mziki na magari ya kuzoa takataka na kusomba matofali.
Alitolea mfano wa kikundi cha
wanawake waliopewa chelehani 50 na wataanza kurejesha mikopo baada ya
miaka miwili na wakimaliza mkopo vifaa vile vinakuwa mali ya kikundi.
“Niombe sasa kwa wale vijana ambao
mnaisha Temeke, haijarishi unatoka Wilaya gani hapa Dar es Salaam au
mkoani, mkirudi kwenu kachangamkieni fursa hii ili kuwawezesha kujikimu
kimaisha na kupata faida kubwa ya kuendesha uchumi wenu”, Alisistiza
Marika.
0 comments:
Post a Comment