METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, June 4, 2020

MIRADI YA ULGSP YAWA KIVUTIO KWA WAGENI KATIKA MJI WA SUMBWANGA

Barabara iliyotengezwa kupitia Mradi wa ULGSP mjini Sumbawanga

Waziri wa OR – TAMISEMI Mh. Suleiman Jafo 


Waziri wa OR – TAMISEMI Mh. Suleiman Jafo (kulia) akizindua mradi wa barabara yenye urefu wa Km 11.577 yenye thamani ya Shilingi 18,752,478,714.03 wakati alipofanya ziara yake mjini Sumbawanga.


 Waziri wa OR – TAMISEMI Mh. Suleiman Jafo katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali pamoja na Kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa ikiongozwa na mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo (kuliani mwa Waziri).


Katika kuhakikisha maendeleo ya nchi yanamgusa kila mwananchi katika mikoa, Wilaya na Halmashauri nchini, Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imepewa dhamana ya kusimamia programu ya uimarishaji miji (Urban Local Government Support Program – ULGSP) kwaajili ya kuimarisha halmashauri 18 za miji na manispaa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.

Hivi karibuni (2.6.2020) Waziri wa OR – TAMISEMI Mh. Suleiman Jafo ametembelea miradi mitatu inayotekelezwa na program ya ULGSP yenye thamani ya Shilingi 26,998,770,878.66/= ambapo alikagua mradi wa Kituo cha Malori kilichopo Utengule kata ya Lwiche, kuweka jiwe la msingi katika kituo cha Mabasi kilichopo Katumba Azimio kata ya Pito pamoja na kuzindua mradi wa barabara za kilometa 11.577 zilizozunguka katika mitaa kadhaa ya mji wa Sumbawanga.

Katika kusifia mabadiliko ya mji wa Sumbawanga kutokana na utekelezwaji wa miradi hiyo Mh. Jafo alisema kuwa Sumbawanga ya miaka mitano iliyopita siyo Sumbawanga ya sasa kwani barabara zilizotapakaa katika mji huo zimeng’arisha mji na hivyo kuwapongeza wanasumbawanga kwa kuwa na mji unaovutia na kuwatanabahisha kuwa kuna miji ambayo inatamani kuwa na barabara kama hizo lakini hawana.

“Barabara zilizofungwa na mataa, tena barabara zenu sio za ‘Double Surface Dressing’ sio barabara za Lami nyepesi hapana, mmepata barabara zilizotengenezwa na lami nzito, wanasumbawanga mnabahati sana sana, katika watu ambao Mheshimiwa Rais amewapendelea wapate mafanikio makubwa katika ujenzi wa miundombinu ya barabara ni watu wa manispaa ya Sumbawanga, barabara zenu ikifika usiku ni kama utalii, mji wa sumbawanga usiku unameremeta,” Alisema.

Na kuongeza kuwa hapo zamani watumishi wengi wa serikali walikuwa wanagoma kupangiwa Sumbawanga tofauti na sasa ambapo mji umependeza na watumishi waliopo hawatamani kuondoka, kwa kuwa mji huo umekuwa wa kitalii kwa wageni wanaoingia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alipokuwa akisoma taarifa ya mkoa kwa Waziri huyo alisema kuwa, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga inatarajia kutekeleza programu ya TACTIC (Tanzania, Cities Transforming Infrastructure and Competitiveness) utakaosimamiwa na OR – TAMISEMI utakaofadhiliwa na Benki ya Dunia, ukitarajiwa kuwa na thamani ya Shilingi Bilioni 35.26.

“Katika programu hii mradi mbalimbali inatarajiwa kutekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 35.26 ambayo ni ujenzi wa Soko la Mazao eneo la Kanondo, Ujenzi wa Dampo la Kisasa kule Mbalika na ujenzi wa barabara zenye urefu wa Km. 13, barabara hizo zitakuwa kwa kiwago cha lami, ile lami ya Zege inayoitwa ‘Asphalt Concrete’. Ni matarajio yetu kuwa fedha hizo zitakuja kwa wakati ili tuweze kutekeleza miradi hiyo kwa haraka,” Alisema.

Awali wakati akitoa taarifa ya miradi hiyo ya ULGSP Mratibu wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijiji (TARURA) Mhandisi Suleiman Mziray alieleza madhumuni ya miradi hiyo kuwa ni kuhakikisha halmashauri inaongeza vyanzo vya mapato, kuongeza fursa za biashara kwa wananchi wanaoishi karibu na miradi hiyo kwa kuanzisha miradi midogo midogo kama migahawa, maduka na nyumba za kulala waeni na hivyo kuongeza ajira na kipato cha mwananchi mmoja mmoja. 
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com