Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kuwawajibisha watumishi wote walioisababishia halmashauri hiyo kupata hati yenye shaka na kumpatia taarifa ya hatua alizochukua kwa watumishi hao ndani ya siku saba kabla ya mabaraza ya madiwani kuvunjwa.
Amesema kuwa kwa mujibu wa maelekezo ya Katibu Mkuu Ofisi ya Raisi Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) yaliyotolewa tarehe 24, April, 2020 kuhusu kushughulikia hoja na mapendekezo ya CAG, pamoja na mambo mengine imeelekezwa kuwa Halmashauri zilizopata Hati yenye Shaka zimepoteza sifa za kupatiwa fedha za utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika kipindi cha miaka mitatu ijayo na hivyo kuchelewesha maendeleo kwa wananchi.
“Kwa kupata hati yenye shaka, halmashauri ya wilaya ya Nkasi inapoteza sifa za kupatiwa fedha za utekelezaji wa miradi ya kimkakati ambayo lengo lake ni kupoteza mapato katika halmashauri, hii ni adhabu kubwa sana katika halmashauri yetu, haipendezi, pengine wengine walikuwa wanaichukulia kijuu juu, miradi ya kimkakati ni miradi mukubwa ambayo halmashauri zimepewa nafasi ya kubuni na kupatiwa fedha ya kutekeleza, kama ni stendi za mabasi, maghala au kumbi zamikutano,” Alisema.
Na kuongeza kuwa ,” Hawa waliotufikisha hapa, hawawezi kuachwa hivi hivi, ni lazima wachukuliwe hatua kali za kinidhamu na Mkurugenzi nimekupa siku saba, uwe umetoa adhabu hii, nipate taarifa ndani ya siku saba, iwe nimepata taarifa ya namna hawa watu watakavyoshughulikiwa kinidhamu, hatuwezi kuendelea namna hii watu wanafanya mzaha, wanafanya uzembe, halafu halmashauri inabeba mzigo wa hawa watu wachache wazembe kwanini?” Alikemea.
Wakati akieleza miongoni mwa sababu zilizosababisha halmashauri hiyo kupata Hati ya Mashaka kwenye hesabu za kuishia tarehe 30, Juni 2019 Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo alisema kuwa Ukaguzi wa mtiririko wa fedha (Cash Flows Statements) kwenye kitabu cha hesabu ulionesha kuwa na upungufu wa shilingi 2,528,347,000/=.
“Ukaguzi wa Mtiririko wa fedha kwenye kitabu cha hesabu ilibainika kuwa Halmashauri imeonesha mtiririko wa fedha uliotoka kuwa Shilingi 16,827,818,000 ikiwa ni mishahara, malipo ya vibarua na haki mbalimbali za watumishi, hata hivyo kwenye mchanganuo ilionekana madai ya watumishi yamepungua kwa Shilingi 383,690,000 hivyo kufanya madai ya watumishi kuoneshwa pungufu kwa jumla ya Shilingi 2,528,347,000/=,” Alifafanua.
Aliongeza kuwa kwa upande wa magari na pikipiki, mali za halmashauri, halmashauri ilionesha jumla ya Shilingi 554,292,000/= lakini baada ya daftari la mali za kudumu kupitiwa ilionesha jumla ya shilingi 612,940,420 na khivyo kuonesha upungufu wa Shilingi 58,648,420/=.
Kwa upande wake Afisa Serikali za Mitaa mkoa wa Rukwa Albinus Mgonya alisema kuwa kati ya Halmashauri 185 zilizokaguliwa kwa hesabu zilizoishia 30 Juni 2019, Halmashauri 176 zilipata Hati Inayoridhisha na Halmashauri 9 zilipata Hati yenye Shaka ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi huku hoja zilizoibuliwa kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019 ni hoja 32 na hoja za nyuma zilizokuwa bado hazijafungwa ni 52.
0 comments:
Post a Comment