
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa
(kulia), akipeana mkono na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji (Mb), baada ya uzinduzi wa Jengo la Ofisi ya Taifa ya
Takwimu (NBS), jijini Dodoma.

Muonekano wa Jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Jijini Dodoma, lililozinduliwa na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa
(kulia), akimkabidhi Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji (Mb), kitabu cha matokeo ya viashiria muhimu vya utafiti
wa mapato na matumizi ya Kaya binafsi kwa Tanzania Bara wa mwaka
2017/18, jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wa sita kulia) na viongozi wengine wakiwa
wamenyanyua kitabu cha matokeo ya viashiria muhimu vya utafiti wa
mapato na matumizi ya Kaya binafsi kwa Tanzania Bara wa mwaka 2017/18,
jijini Dodoma
*******************
Na. Josephine Majura na Peter Haule, WFM, Dodoma
Kiwango cha umaskini nchini
Tanzania kimepungua kwa asilimia mbili, ikiwa ni matokeo ya juhudi za
Serikali ya Awamu ya Tano ya kupunguza umasikini kwa wananchi hasa wa
hali ya chini.
Hayo yamebainishwa wakati Waziri
Mkuu Mhe. Kassimu Majaliwa, akizindua ripoti ya matokeo ya viashiria
muhimu vya utafiti wa mapato na matumizi ya mwaka 2017-18 na jengo la
Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Mkoani Dodoma.
Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa,
amewataka Watakwimu nchini kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia
sheria, taratibu na miongozo mbalimbali wakati wa kutekeleza majukumu
yao hususan kuzalisha na kusambaza takwimu zenye viwango vya kitaifa
na kimataifa ili kuisaidia Serikali kujua mahitaji yaliyopo.
“Serikali inayoongozwa na Mhe.
Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, inatambua umuhimu wa takwimu
zenye ubora, kwa kuwa ndiyo macho na masikio ya Serikali katika
kufuatilia na kutathmini mipango ya maendeleo ya nchi”, alieleza Mhe.
Majaliwa.
Mhe. Majaliwa, alisema kuwa
takwimu bora hutoa fursa kwa Serikali kufanya mapitio ya sera, mipango
na mikakati kulingana na hali ilivyo kwa wakati husika na pia kupima
ilikotoka, ilipo na kutabiri inakoelekea hivyo kupima mwenendo wa
jitihada za Serikali.
Aidha aliiagiza Ofisi ya Taifa
ya Takwimu Nchini (NBS), kuhakikisha Halmashauri zote nchini zinakuwa
na Afisa Takwimu ili kurahisisha upatikanaji wa takwimu kwa wakati ili
kuweza kusaidia maendeleo nchini.
Kwa upande wake Naibu wa Waziri wa
Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, amesema kuwa Wizara yake imepewa
jukumu la kusimamia Uchumi wa Taifa, lakini haiwezi kusimamia uchumi
bila kuwa na takwimu rasmi na sahihi.
“Katika kipindi cha takribani
miaka mitatu na nusu tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani,
umaskini nchini umepungua hadi kufikia takribani asilimia 26 kutoka
asilimia 28, ikiwa ni sawa na kupungua kwa asilimia mbili”, alisisitiza
Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji alisema kuwa
matokeo ya tafiti yaliyozinduliwa na Mhe. Kassim Majaliwa, yameonesha
kupungua kwa umaskini wa watanzania waishio vijijini kwa asilimia 3.1
kati ya mwaka 2011/12 na mwaka 2017/18.
Alieleza kuwa hayo ni matunda ya
uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya
Kiongozi wake, Mhe. Rais, Dkt. Magufuli.
Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa
Serikali Dkt. Albina Chuwa, alisema kuwa utafiti wa mwaka 2017/2018
umetumia teknolojia ya kisasa inayojulikana kama Survey Solution ambayo ni tofauti na njia ya awali ya kutumia madodoso yaliyochapishwa hivyo kupunguza gharama za kufanya tafiti za kijamii.
Wawakilishi wa Mashirika ya
Kimataifa akiwemo Mwakilishi wa Benki ya Dunia Bw. Denis Biseko,
wameipongeza Serikali kwa kupunguza kiwango cha umasikini kwa takribani
asilimia 2, na pia wamepongeza matokeo ya utafiti huo ambao umezingatia
usawa wa kijinsia hivyo kuwa chachu ya maendeleo kwa kuwa ni moja ya
lengo la mashirika hayo.
0 comments:
Post a Comment