Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula amesema bomoabomoa inayoendelea
katika baadhi ya maeneo nchini inatokana na ujenzi holela na kutofuata
ramani za mipango miji.
Mabula amesema sababu hizo ndizo zinawasababishia hasara wananchi ya kuvunjiwa makazi.
“Watu wengi wamejenga katika maeneo yasiyo rasmi hasa mjini,” alisema na kuongeza:
“Jambo hili linachangia vilio kwa kiasi kikubwa hasa unapofika wakati wa kuweka miundombinu ya maeneo husika.”
Naibu waziri huyo alisema hivyo akimaanisha vilio vinavyotokana na watu kubomolewa makazi yao.
“Wakati
huo wahusika kama Dawasco (Shirika la Majisafi na Maji taka Dar es
Salaam) au Tanroads (Wakala wa Barabara)hujikuta wanalazimika kuvunja
baadhi ya nyumba zilizopo katika maeneo yao ili waweze kufanya kazi
iliyokusudiwa,” aliongeza Mabula.
Sababu hizo za bomoabomoa alizitoa jana wakati wa maadhimisho ya siku ya makazi duniani iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Tayari
baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam waliojenga pembezoni mwa Barabara ya
Morogoro wamepoteza makazi yao baada ya Tanroads kubomoa nyumba ili
kupisha mradi wa barabara ya kisasa ya njia sita.
Katika
hotuba yake, naibu waziri huyo aliwaonya watu wanaoendelea kujenga
kiholela katika maeneo yaliyopangwa akisema urasimishaji unaoendelea
nchini hauwatagusa wale ambao tayari maeneo yao yana mipango kabambe.
Alisema kuwa urasimishaji huo usiwe chachu ya watu kuendelea kujenga holela kwa kufikiri wizara itarasimisha makazi yao.
Pia,
alisisitiza kwamba hawatarasimisha maeneo ambayo tayari yana mpango
kabambe wa uendelezaji mji (master plan), hivyo watakaojenga bila
kufuata utaratibu na bomoabomoa ikiwakuta hawatahangaika nao.
Mwenyekiti
wa Chama cha Ushirika cha Ujenzi wa Nyumba Mwenge, Hilary Mdaki alisema
mbali na kuzingatia ujenzi wa nyumba katika maeneo yaliyo ndani ya
mipango miji, changamoto mbalimbali zimekuwa zikiwakwamisha katika
kufikia malengo yao ikiwamo ugumu wa upatikanaji wa ardhi.
0 comments:
Post a Comment